
Kama kuanzia leo utajitolea kufanya yale ambayo walofanikiwa wanafanya bila shaka utapata matokeo sawa na wao. Watu wengi wanachokikosea ni kuwa hawafanyi yale ambayo yanafanywa na waliofanikiwa na wakati huo huo wanataka kufanikiwa. Mafanikio kwa mfumo huu si kama ajali hutokea bali hutengenezwa na mtu kwa kuamua na kuchukua hatua sawa na wengine walofanikiwa. Hiki ndicho kinamsukuma mwandishi Tommy Newberry tujifunze masomo saba ya kutusaidia kuanza mchakato wa kuelekea kwenye mafanikio makubwa.
Mafanikio ni hali endelevu ya kutambua thamani na mchango wako kwa wengine. Ni hali ya kutumia ulichonacho kufanya maisha ya watu wengine yawe bora na mafanikio ni safari ya kugundua upana wa maisha uanziao ndani na kwenda nje. Watu waliofanikiwa hujua kuwa ili kufanikiwa lazima ujue kuwa maisha yanaongozwa na sheria. Sheria hizi kwa kuzifuata vizuri wanakuta mafanikio yakiwafuata. Sheria mojawapo ya mafanikio ni ya utoaji. Hii ikiwa ina maana ya kadri unavyotoa thamani kupitia ujuzi, maono, biashara kwa watu wengine ndivyo unavyoweza kufanikiwa zaidi.
Mafanikio yanatengenezwa na ni matokeo ambayo huwa yanatarajiwa kwa vile mtu anavyopanda. Ni sawa na mkulima shambani asivyoweza kutegemea mavuno pasipo kupanda. Mafanikio yako hivyo hivyo hayatokei tu kama ajali bila kutengenezwa na mtu mwenyewe. Kuna nafasi na wajibu mtu hupaswa kufanya ili aweze kufanikiwa kiuchumi, kiafya, kifikra hata kiroho. Kuna majukumu ya kubeba na kufanya ili mafanikio yawe matokeo yanayotarajiwa.
Mafanikio huja kwa kufikiri vyema na uchukuaji hatua sahihi. Kuchukua hatua ni mbegu unayopanda ya mafanikio unayoweza kuvuna. Ukiangalia leo maisha yako utaona wewe ni matokeo ya fikra zako na hatua ulizochukua siku za nyuma. Kila kitu unachofikiri na kufanya katika maisha yako huhesabika kuchangia mafanikio yako. Watu wanaokuzunguka, taarifa au maarifa unayoyapata, tabia zako vyote kwa pamoja vinahusika katika mafanikio ya mtu. Iwe katika kuyapata au kuyakosa.
Unapoweka visingizio vingi na kughairisha mambo katika maisha ndivyo unavyopishana na mafanikio. Watu waliofanikiwa walijua jambo hili mapema kuwa visingizio au kughairisha huua ndoto zao. Kusingizia vitu kama sina fedha, sina muda, sina mtandao wa watu ni njia ya kujichelewesha kwa mtu kufanikiwa. Maana wapo watu ambao walianza vitu pasipo fedha, muda ulikuwa una vitu vingi, na walianza bila kufahamiana na watu. Unapoweka mbali visingizio unayakaribisha mafanikio yaje kwako haraka.
Dunia hugawanya makundi mawili ya watu linapokuja suala la mafanikio. Kuna watendaji na wale wenye kujihisi wamefanikiwa. Kundi la kwanza linajua mafanikio huwezi kuyapata bila kuchukua hatua. Kundi la pili hujihisi wamefanikiwa kwa kuwa na ndoto tu bila kuchukua hatua yoyote ile kuelekea ndoto zao.
Mafanikio ni kuchagua unataka kuwa nani katika maisha. Unapofika ngazi ya kutambua nini unachokitaka maishani basi mafanikio humfuata mtu huyo. Hili ni swali la kujikagua wewe mwenyewe kuwa nini unachokitaka maishani na unataka kuwa nani. Ukijua unataka kuwa nani inakupa nafasi ya kuandaa malengo ambayo yatakusaidia kufikia ngazi hiyo. Hili litakupa uzito wa kuchukua hatua na kutumia muda wako vizuri ukiyaishi malengo madogo madogo na makubwa. Anzia ulipo kujiuliza unataka kuwa nani au u nani sasa. Je nini ndoto zako, upekee wako ni upi na kitu gani kinachokusukuma maishani kuamka asubuhi au kukifanya bila kuchoka. Huu utakuwa mwanzo mzuri wa kutengeneza njia ya kufanikiwa.
Kupanga malengo kwa kuyaandika ni kuruhusu kujihamasisha mwenyewe kuyafuatilia. Yaandike malengo yako kwa kuanza kuyagawa kidogo kidogo. Haya malengo yanakusaidia kukupa uwazi juu ya maisha gani unayotamani kuwa nayo. Ukishakuwa umeyaandaa katika notibuku yako au mfumo mwingine wowote ule mshirikishe mtu unayemwamini. Kitendo hiki cha kumshirikisha ni kukupa usimamizi wa karibu wa kuona kama kweli unajitoa kuyafanikisha malengo ulojiandikia. Ukiwa na malengo unakuwa unaishi kwa kujua wapi uendako kuliko mtu asiye na malengo ya kusimamia.
Muda ni muhimu katika safari ya mafanikio. Malengo na ndoto zote unazotaka kuzitimiza lazima zitumie muda. Hivyo jukumu la kutumia vizuri muda ni la msingi sana kufanya ufanikiwe. Hutaweza kuongeza muda ukishapita. Machaguzi unayofanya kila siku na maisha yako yategemee na kule unakotaka kwenda. Kuna machaguzi ambayo unapofanya bila utulivu huwa yanagharimu muda wako na hatimaye ushindwe kufanikisha baadhi ya malengo yako. Masaa yako 24 yatumie kwa namna kila jambo unalolifanya basi liwe linakusogeza katika maisha unayoyataka.
Udhibiti wa hisia zako ni kuweza kudhibiti maisha yako. Hisia hasi humwondosha mtu katika kufanya kazi kwa ufanisi au kufanikisha malengo yake. Jitahidi kusimamia hisia zako zisiwe kuathiri safari yako ya mafanikio. Zuia hisia hasi kutawala siku yako maana zitakuharibia hamasa kuelekea kufikia mafanikio. Jisemeshe lugha ya mafanikio kuliko kushindwa. Ondoa imani zinazokukwamisha kuona mafanikio na jenga picha chanya akilini mwako kuhusu maisha na mafanikio. Ukiweka mfumo huu katika fikra zako utaweza kuepusha msongo wa mawazo ambao kwa watu wengi unawapotezea fokasi ya kufanikisha malengo yao.
Kitabu hiki ni kizuri sana na haya ni machache katika kujifunza. Mafanikio si ajali bali hutengenezwa. Kubali kufuata mchakato wa kuyatengeneza nayo yatakufuata.
Mchambuzi,
Dkt.Raymond Nusura Mgeni
+255 676 559 211.