Sisi binadamu huwa hatuwezi kutulia kama hatujapata maelezo kuhusu kitu kinachotuhusu. Akili yetu hairuhusu kuwa njia panda bila ya kuwa na maelezo.

Hivyo kuna njia mbili za kupata maelezo ya kitu, kupitia ukweli na kupitia hadithi.

Ukweli ni jinsi kitu kilivyo, hivyo pale ukweli unapoulikana, watu huchukua huo.

Hadithi ni maelezo ambayo watu huyatengeneza pale ukweli unapokosekana. Pale watu wanapokosa maelezo ya kweli kuhusu kitu, wanatengeneza maelezo yao wenyewe kwa namna wanavyoelewa wao.

Hivi ndivyo uongo, majungu, umbeya na ushirikina unavyotengenezwa. Kwa watu kuja na maelezo yao wenyewe kuhusu jambo ambalo ukweli haujajulikana.

Chukua mfano mzuri wa magonjwa, mtu akiumwa ugonjwa ambao vipimo vimeweza kuonesha, ukweli unakuwa wazi na kila mtu anajua anaumwa nini. Mtu akipata degedege na akapimwa akakutwa ana malaria, huo ndiyo ukweli, degedege imesababishwa na malaria. Lakini mtu akapata degedege na kupimwa kila kitu kikaonekana hakuna, watu hawawezi kuridhika, watakuja na hadithi zao. Na wengi hukimbilia kusema mtu kalogwa au kupatwa na pepo.

Tunapojua hili, tunapaswa kuzingatia mambo matatu;

Jambo la kwanza chunguza kila maelezo unayopewa kuhusu mambo mbalimbali, jiulize kama ndiyo ukweli uliothibitishwa au ni hadithi za watu ambazo watu wametengeneza au kuzipokea. Sehemu kubwa ya mambo yanayopokelewa na kuaminika kwenye jamii siyo ukweli, bali ni hadithi za kutengenezwa.

Jambo la pili ni kuzuia mhemko wako wa kukimbilia kutengeneza hadithi kwa mambo ambayo hujayathibitisha kuwa kweli. Mfano umemsalimia mtu na hakuitika, ni rahisi kukimbilia kusema kwamba amekununia au hakupendi. Lakini hiyo ni hadithi uliyotengeneza mwenyewe, huenda hakusikia, huenda amevurugwa na mambo mengine, kabla hujajipa maelezo yoyote, jua ukweli kwanza.

Jambo la tatu ni kuwaeleza watu ukweli ulivyo, pale unapokuwa kwenye nafasi ya uongozi au wengine kukutegemea kwa mambo fulani, jijengee utaratibu wa kuwaeleza ukweli wa mambo ulivyo. Usipowaeleza ukweli, wao watatengeneza hadithi zao na hazitakuwa kweli, kitu ambacho kinaweza kuleta sitofahamu kubwa. Hili ni muhimu sana hasa kwenye uongozi, usipokuwa na utaratibu wa kuwaeleza watu ukweli, watatengeneza hadithi ambazo zitafanya uongozi usiaminike.

Ukweli au hadithi? Jua kabla hujapokea na kuamini chochote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha