Kuanza kitu kipya ni rahisi, unakuwa na hamasa kubwa na unaona njia ilivyo wazi ya kufanikiwa.
Unakuwa unaona upande mmoja tu wa mafanikio, huoni upande wa pili wa changamoto ambazo lazima zipo.
Angalia hadithi nyingi za fursa, mfano kilimo cha matikiti maji ambacho kimekuwa kinatumika kuwahadaa wengine.
Mtu anaambiwa kilimo hicho kinalipa sana, heka moja inaweza kuzalisha matunda elfu 5, kama ukiuza kwa bei ya chini kila tunda elfu moja, unakuwa umepata milioni tano. Gharama za kuhudumia heka moja mpaka kuvuna ni milioni moja na inachukua siku 70 tu kuvuna.
Hapo kichwa cha mtu kinapata moto, uweke milioni moja na kuvuna milioni tano ndani ya miezi mitatu pekee? Hapo akili haiwezi kuingiza kitu kingine chochote, inaona faida kubwa tu inayopatikana.
Na ukweli ni wapo ambao wanapata faida hizo, lakini kuna kitu hujui kuhusu wao, siyo mara ya kwanza kwao kufanya kitu hicho. Wameshafanya kwa miaka mingi, wameshapitia changamoto nyingi, wamejifunza na kuwa bora na ndiyo wameweza kupata matokeo hayo.
Sasa aliyepata moto kwa kuona faida kubwa anaondoka kwenda kuanza kilimo, anachoona yeye ni faida kubwa tu. Anapoanza anakutana na changamoto ambazo hakuzitarajia, mara mazao yanapatwa na ukungu, mara maji siyo ya kutosha, mara wafanyakazi siyo waaminifu. Anapambana kweli kweli, bado ndoto ya faida ipo kwenye akili yake.
Anafikia muda wa kuvuna, matunda ni madogo kuliko alivyotegemea, ile ndoto ya kuuza tunda moja kwa elfu moja haipo tena. Anajipa moyo kwamba hata akiuza mia tano bado hatapata hasara. Anatafuta wa kumuuzia kwa bei hiyo hapati. Kila anayeyaona anamwambia labda uniuzie yote kwa laki 5.
Hapo anachanganyikiwa zaidi, gharama alizotumia ni milioni moja, mauzo aliyotegemea ni milioni tano, anayokuja kuambiwa atapata ni laki 5! Haamini anachosikia, lakini pia muda unakwenda, hana la kufanya hivyo anauza kwa bei ya hasara kubwa.
Kinachotokea ni mtu huyo hajaribu tena kilimo hicho, anakimbia na kuona hadithi alizosikia siyo za kweli na amelaghaiwa.
Ukweli ni hajadanganywa wala kulaghaiwa, ila tu hajaelezwa ukweli wote, alipewa sehemu moja tu ya ukweli ambayo ni ya faida, hakupewa sehemu ya pili ambayo ni changamoto.
Lakini asichojua ni kwamba, wale wanaoingia na kutoka kwenye kila aina ya biashara au kilimo ndiyo wanawanufaisha wakongwe walio kwenye biashara hiyo.
Mfumo mzima wa biashara na uchumi unajengwa na wale wanaoingia na kutoka, wale wanaokuja, wanawekeza, wanapata hasara na kukimbia. Wale wakongwe ambao wapo miaka na miaka ndiyo huwa wanachuma faida mara zote.
Hivyo kama unataka kufanikiwa kwenye jambo lolote lile, usijaribu kuona kama utapata faida uendelee au utapata hasara uache. Kuwa na uhakika chochote unachokwenda kuanza utapata hasara.
Hivyo chagua kuingia kwenye kitu ambacho utakifanya kwa muda mrefu, utajifunza kwa kina kupitia changamoto na hasara utakazopata na kujijengea mfumo utakaokuzuia usianguke na kushindwa kabisa.
Usiwe mtu wa kuingia na kutoka, kuwa mtu wa kuingia na kudumu kwenye kile unachochagua. Kabla hujafanikiwa, utashindwa kwenye mengi.
Nimewahi kukushirikisha hapa kiwango cha mafanikio cha simba kwenye uwindaji, ni kidogo mno, siyo hata asilimia 50. Yaani pamoja na ukali na uimara wake, simba anashindwa kwenye mawindo mengi anayojaribu, lakini hakati tamaa. Anaendelea kuwinda mpaka apate chakula.
Huo ndiyo msimamo unaopaswa kuwa nao, hujaribu, bali unafanya mpaka upate unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha, tuwe na focus kama ya Simba akiwa mawindoni ndipo tutakuwa na mafanikio makubwa
LikeLike
Karibu
LikeLike
Kuna tofauti ya kufanya na kujaribu, tunahitaji kufanya kweli kwa kudhamiria
LikeLike
Kabisa
LikeLike
Msimamo unalipa kwenye kila jambo tunaloamua kufanya.
Ubarikiwe sana Kocha.
LikeLike
Asante
LikeLike
Asante kocha napaswa kuendelea kufanya jambo moja kwa muendeleo bila kukata tamaaa kwa changamoto ninazokutana nazo
LikeLike
Karibu.
LikeLike