Wakati mambo ni mazuri, mtu anaweza kuahidi na kufanya kama anavyoahidi.

Kama ilivyo kwa bahari tulivu, kila nahodha anaonekana ni mahiri.

Au hali ya uchumi inapokuwa nzuri, kila mtu anaonekana anafanya vizuri.

Lakini pale mambo yanapokuwa magumu, ndipo tunapata nafasi ya kujua nani kweli yuko vizuri na nani anaigiza.

Warren Buffett amewahi kunukuliwa akisema pale mawimbi yanapotulia ndiyo tunajua nani anaogelea uchi. Akimaanisha kwenye uwekezaji wakati uchumi ni mzuri, kila mtu anaonekana ni mahiri, ni pale wimbi la uchumi mzuri linapoondoka ndiyo tunajua kwa uhalisia nani mwekezaji mahiri na nani siyo mahiri.

Hili linakwenda kwenye kila eneo la maisha yetu, hata kwenye falsafa, imani na misingi tunayoishi.

Umewahi kuona mtu anajinadi ni wa imani nzuri kulingana na dini yake, anasali vizuri na kuamini Mungu ndiye mlinzi wake. Halafu anajipatwa na changamoto kubwa, labda ya afya, ambayo anajaribu kila njia lakini haitatuliki. Baadaye anashauriwa aende kwa mganga ambaye ataweza kuitatua, kumbuka hapo kwenda kwa mganga inapingana na imani yake, lakini kwa kuwa anataka sana kutatua shida hiyo, anavunja imani yake na kwenda kwa mganga. Sasa iwe atapona au la, kitendo cha kushindwa kusimamia imani yake inaonesha ni jinsi gani mtu huyo au imani yake siyo imara.

Wakati mambo ni mazuri ni rahisi kusimamia chochote unachochagua, ni pale mambo yanapokuwa magumu ndiyo unaweza kujua nani kweli anasimamia kile anachosema.

Hivyo unapopitia nyakati ngumu, ndiyo wakati mzuri kwako kujua kipi unaamini na kusimamia kweli.

Kadhalika kwa wengine, kama unataka kujua kile wanachoamini na kusimamia kweli, angalia namna wanavyokabiliana na magumu wanayokutana nayo.

Magumu huwa yanakuja kupima msimamo wetu, kama unataka kufanikiwa, lazima uwe na msimamo usiovunjwa na chochote. Maana ukishayumbishwa, huwezi kukabiliana na ugumu uliopo kwenye safari ya mafanikio.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha