Mitandao ya kijamii huwa inahitaji kuwa na watumiaji wengi ndiyo iingize faida. Kadiri watu wanavyotumia mtandao kwa muda mrefu, ndivyo mtandao huo unavyonufaika kwa sababu faida yake ni muda wa watu.

Kwa kuwa inategemea sana wingi wa watu ndiyo faida iwe kubwa, mitandao hii imekuwa inatumia njia mbalimbali kuwatega na kuwanasa watu kwenye mitandao hiyo.

Njia moja kubwa ni kuteka hisia za watu na kuwafanya watake kuitembelea muda wote ili kuona nini kinaendelea kwenye maisha ya wengine. Tunaweza kusema hisia moja kuu inayokuza mitandao hii ni wivu, ule msukumo wa mtu kutaka kuona maisha ya wengine yakoje na yeye kuonesha maisha yake ni bora zaidi.

Njia nyingine kubwa ambayo mitandao hii imekuwa inatumia kwenye kuwatega na kuwanasa watu ni kwenye umaarufu. Mitandao hii imewaaminisha watu kwamba kadiri unavyokuwa na wafuasi wengi kwenye mitandao hiyo, ndivyo unavyokuwa maarufu na kufanikiwa zaidi.

Hivyo kinachotokea ni kila mtu kukimbizana na kukuza wafuasi wake kwenye mitandao hiyo, kutafuta ‘likes’ nyingi zaidi kutoka kwa wengi. Watu wamejikuta mpaka wanafanya mambo ya ajabu ili tu kupata wafuasi kwenye mitandao hiyo ya kijamii.

Lakini huo ni mchezo usio na manufaa yoyote, wafuasi wengi kwenye mitandao ya kijamii hawatakusaidia chochote kama huna kitu cha tofauti unachoweza kufanya kwa wengine.

Umaarufu wa kupata kwa kuwa na wafuasi wengi mtandaoni, ambao ni feki, huwa hauna manufaa na haudumu. Lakini mitandao hiyo haitaki wewe ujue hilo, kwa sababu itapoteza wafuasi na kukosa faida.

Kama unataka umaarufu, anza na kile unachofanya, kuwa bora kwenye kazi au biashara yako, toa huduma bora kabisa kwa wengine na wao watakuzungumzia wewe mitandaoni na penginepo. Hapo utapata umaarufu wenye manufaa bila hata ya kutumia nguvu kubwa mitandaoni.

Chukua mfano wa picha ya Monalisa, ni picha maarufu kwenye mitandao ya kijamii. Lakini huyo Monalisa hayupo, hata aliyechora picha yake hayupo, ila kwa sababu ni picha bora, inawekwa na kusambazwa mitandaoni.

Kadhalika watu maarufu wengi mitandaoni, siyo wale wanaoshinda wakitafuta wafuasi, bali wale ambao kuna makubwa wameyafanya nje ya mitandao hiyo.

Kama kila siku unatumia saa moja mitandaoni kutafuta wafuasi, ibadili saa hiyo na itumie kuboresha kile unachofanya, kuwasiliana na wateja au wapokeaji wa kazi unayoifanya, kujifunza zaidi kuhusu unachofanya.

Baada ya muda, hutakuwa hata na uhitaji wa kutumia nguvu, matokeo unayozalisha yatakutangaza kwa nguvu kuliko kutumia muda kutafuta wafuasi mtandaoni, ambao wengi huishia kuwa feki.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha