Kitu kinapokuwa muhimu kwa mtu, hufanya uwekezaji wa kutosha kwenye kitu hicho ili apate matokeo mazuri kwenye kitu hicho.

Angalia pale mtu anapoumwa, atafanya awezavyo ili apate matibabu sahihi na aweze kupona.

Angalia kwenye harusi, hata kama mtu ni masikini kiasi gani, atapambana awezavyo harusi iweze kwenda vizuri. Atahakikisha gharama za kukamilisha zinapatikana, kwa kuwasumbua watu wake wote wa karibu.

Kadhalika kwenye kitu kingine chochote mtu anakitaka kweli, ambacho anaona maisha yake hayawezi kwenda bila ya kuwa na kitu hicho, atapambana awezavyo mpaka akipate.

Kwa kujua hili, tunakuwa na uhakika kabisa kwamba kama mtu hafanyi uwekezaji kwenye kitu, basi hakitaki hasa, siyo kitu ambacho maisha yake hayawezi kwenda bila ya kuwa nacho.

Hapa tunajifunza njia nyingine ya kutupa nguvu ya kupambana kufikia ndoto zetu kubwa, kuona hakuna maisha mengine ila ndoto hizo na hivyo kuwa tayari kuwekeza kila tunachopaswa ili kuzifikia.

Kuweka kazi zaidi, muda zaidi na gharama nyingine ni hitaji kubwa kwenye kufikia ndoto kubwa kwenye maisha. Kama ni ndoto ya kuazima, ndoto ambayo hata usipoifikia hutaumia, hutapata nguvu ya kukusukuma. Lakini ndoto inapokuwa yako kweli, inapokuwa kitu ambacho huwezi kuishi bila kukifikia, utapata msukumo wa kuwekeza zaidi.

Ndiyo maana kauli muhimu ya kujiambia kwamba; “NITAFIKIA NDOTO ZANGU AU NITAKUFA NIKIZIPAMBANIA” ni kitu unachopaswa kujiambia kila siku na kukimaanisha kweli, kwa kuyaona maisha yako yakitegemea sana ndoto kubwa uliyonayo.

Yaani ona hakuna uwezekano wa kuendesha maisha yako nje ya ndoto kubwa uliyonayo. Kisha weka kila unachopaswa kuweka ili kufikia ndoto hiyo, kwa sababu ndiyo maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha