Msingi wa kitu chochote kile, unapaswa kuwa imara, ili kuweza kubeba uzito unaoambatana na kitu hicho.

Hivyo uimara wa msingi ndiyo unaopima ukubwa kiasi gani unaweza kufikiwa.

Ukichukua mfano wa mimea, miti mikubwa na inayodumu kwa muda mrefu, huwa ina mizizi mikubwa na mirefu, hiyo ndiyo inaipa nguvu, kwa kuhakikisha maji na madini muhimu yanaendelea kupatikana hata nyakati zinapokuwa ngumu.

Ukija kwenye mfano wa nyumba, msingi wa ghorofa ni tofauti kabisa na msingi wa nyumba ya kawaida. Kadhalika msingi wa ghorofa tano ni tofauti na wa ghorofa ishirini.

Kwa kujua hili, tunapaswa kuwa makini na msingi tunaojijengea kwenye maisha, kabla hata hatujaanza kukuza kile tunachofanya. Kwa sababu kama msingi siyo imara, utakuwa kikwazo kwa ukuaji unaoweza kufikiwa.

Moja ya njia ya kupima misingi unayoiishi kwenye maisha yako ni uwezo wa kukabiliana na magumu ambao lazima utakutana nayo.

Unaweza kuwacheka wale wanaokata tamaa au kukosea kwenye maisha na kujiambia hutafanya kama wao ukipata nafasi kama zao, lakini ukipata unaishia kufanya kama wao.

Tatizo siyo kushindwa, tatizo ni msingi gani ambao umejijengea. Kama msingi siyo imara, ukikutana na mtikisiko mkubwa, unavunjika.

Kwenye kila eneo la maisha yako, jijengee misingi ambayo ni ya kudumu, misingi ambayo haiwezi kuangushwa na chochote kile.

Kwa mfano msingi mkuu wa Upendo ambao tunauishi kwenye KISIMA CHA MAARIFA, hakuna kinachoweza kuuangusha, hakuna hali ambayo haiwezi kufanywa kuwa bora na upendo na hakuna ugumu unaoweza kuangusha upendo.

Kadhalika kwenye nidhamu, uadilifu na kujituma, ukiyasimamia hayo kila wakati bila ya kutetereka, utaweza kukabiliana na kitu chochote unachokutana nacho kwenye maisha yako.

Kwenye fedha msingi wa matumizi yako kuwa madogo kuliko mapato na kuweka akiba pamoja na kuwekeza maeneo yanayozalisha zaidi ni msingi imara ambao hauwezi kuangushwa na chochote.

Kwenye kazi na biashara msingi wa kutoa thamani zaidi, wa kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora kupitia kile unachofanya ni msingi ambao utakubeba kwenye kila hali na hauwezi kushindwa na chochote.

Kwenye mahusiano msingi wa kupenda, kujali na kutoa muda wako kwa wale wa muhimu kwako ni msingi ambao unayafanya mahusiano yoyote yale kuwa imara. Hata yapitiwe na mitikisiko ya aina gani, kama msingi huo upo, yatazidi kuwa imara.

Kwenye eneo lolote la maisha yako ambalo unasumbuka na kuanguka, usihangaike kuangalia yale yanayokuangusha, bali angalia msingi uliojijengea na unaoishi kwenye eneo hilo.

Kama nyumba yako imeanguka kwa tetemeko, hutalichukia tetemeko, badala yake utaangalia uimara wa nyumba.

Kadhalika kwenye maisha, eneo lolote unaloyumba, usihangaike na yanayokuyumbisha bali hangaika na msingi unaoiishi kwenye eneo hilo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha