Kuna sababu kuu tatu za kufanya kazi,
Ya kwanza ni uhai, unafanya kazi ili uweze kuishi, upate fedha ya kuyaendesha maisha yako. Hapa unakuwa huwezi hata kumudu mahitaji yako ya msingi bila kufanya kazi.
Ya pili ni kuwa na akiba ya kuweza kuyaendesha maisha yako kwa siku zijazo. Hapa unakuwa umeshaweza kumudu mahitaji yako ya msingi, lakini unajenga uhakika zaidi wa baadaye.
Ya tatu ni kutoa mchango kwa wengine, kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Hapa unasukumwa na uhitaji wa wengine au changamoto ambazo wengine wanazo na kuzitatua.
Sababu mbili za kwanza ni za kibinafsi na mara nyingi huwa zinampa mtu ukomo. Kwa kuwa mahitaji ya mtu siyo makubwa sana, yakishatimia hapati tena msukumo mkubwa. Na wakati mwingine hata yakitimia, tamaa zaidi inaongezeka kwake.
Sababu ya tatu siyo ya kibinafsi, ni sababu ambayo inawaangalia wengine kabla mtu hajajiangalia mwenyewe. Sababu hii haina ukomo kwa sababu mahitaji ya wengine hayana ukomo. Unazidi kuzioa fursa nyingi zaidi kadiri unavyosukumwa kuwasaidia wengine.
Sababu ya tatu ndiyo huwa inazalisha mafanikio makubwa, kwa sababu haina ukomo, watu huweza kufanya makubwa sana.
Hata kama uko kwenye hali ya chini, ambapo huwezi kumudu mahitaji yako, ukisukumwa na sababu ya tatu, hutasumbuka tena na mahitaji yako binafsi. Japokuwa utasukumwa na kutoa mchango wako kwa wengine, utalipwa kwa kiwango kikubwa kuliko ambavyo ungelipwa kwa kuangalia mahitaji yako binafsi.
Kwa chochote unachofanya, acha ubinafsi ya kujiangalia wewe unapata nini, badala yake angalia unatoa mchango gani kwa wengine, hilo litakusukuma kufanya makubwa zaidi na kupata manufaa makubwa zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha
LikeLike
Karibu.
LikeLike