Ni mara ngapi umefanya kazi au jambo ambalo umeridhishwa nalo kweli kweli. Unajivunia kwamba umeweza kufanya kitu ambacho ni tofauti na mazoea, zaidi ya ambavyo umekuwa unafanya.
Lakini baadaye mtu mwingine anakuja na kukosoa kile ulichofanya na kukuambia hakuna ulichofanya kabisa, ni kitu cha hovyo.
Unakubaliana naye, unajidharau, unaamini kweli hakuna ulichofanya na kukata tamaa hata ya kujaribu tena.
Hivi ndivyo dunia ilivyo na hivyo ndivyo ndoto za wengi zinazikwa.
Kila mtu amewahi kupitia hali hiyo, wengi walikata tamaa kabisa baada ya kudharauliwa na wengine na hao wameishia kubaki chini.
Lakini kuna wachache ambao hawakukata tamaa, ambao waliendelea kujiamini, iwe ni kwa hasira au kutaka kuwaonesha waliowadharau hawapo sahihi, waliendelea, na leo wameweza kupata mafanikio makubwa.
Leo napenda kukushirikisha hili muhimu, kama wewe mwenyewe umeridhishwa na kile ulichofanya, inatosha, hata kama wengine watakudharau na kukukatisha tamaa, hayo ni maoni yao, siyo ukweli.
Wajibu wako wewe ni kufanya kadiri ya uwezo wako, na kila wakati kukazana kufanya kwa ubora zaidi ya ulivyofanya wakati uliopita. Wakati unakazana kuwa bora, puuza wote ambao wanakudharau na kukukatisha tamaa, maana wanachofanya ni kukulinganisha wewe na watu wengine, wakati hamfanani kabisa.
Hii haimaanishi usiwasikilize kabisa wengine, wanaweza kukosoa mambo ambayo yana mchango ukiyafanyia kazi. Hivyo angalia katika kukosoa kwao nini unaweza kuboresha zaidi, lakini kule kukatisha tamaa, achana nako kabisa.
Lakini pia ujumbe hasi huwa una nguvu mara nne ya ujumbe chanya, hata kama ndani ya ukosoaji wa mtu kuna kitu chanya, akili zetu huwa zinaona zaidi hasi kuliko chanya. Hivyo kwa baadhi ya watu, ni vyema kuchagua kuacha kuwasikiliza kabisa kama sehemu kubwa ya ujumbe wao kwako ni dharau na kukatisha tamaa.
Wewe mwenyewe unapaswa kuwa mshauri wako wa kwanza na mtu pekee wa kukupa moyo kuendelea kupiga hatua zaidi. Na njia bora ya kufanya hivyo ni kila wakati kukazana kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa huko nyuma. Kila unachofanya, jiulize wakati uliopita ulikifanyaje, kisha kifanye kwa ubora zaidi wakati huu kuliko ulivyofanya wakati uliopita. Kwa kwenda hivi, utajisukuma na kuwa bora zaidi.
Kama ulichofanya kimekuridhisha kwa sasa, na umekifanya kwa ubora kuliko wakati uliopita, huku ukijipanga kufanya kwa ubora zaidi wakati ujao, uko kwenye njia nzuri ya kufanikiwa, bila ya kujali wengine wanakuchukuliaje au kusemaje.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha
LikeLike