Tunaishi kwenye zama ambazo hadithi za mafanikio ni nyingi kuliko mafanikio yenyewe.
Kila mtu anapenda kujua hadithi ya wale waliofanikiwa sana.
Pamoja na uwepo wa hadithi hizo, bado wanaofanikiwa ni wachache kati ya wengi wanaotaka kufanikiwa.
Na tatizo kubwa ni kwamba hadithi hizo zimekuwa haziwasaidii watu, kwa sababu wamekuwa hawajifunzi kupitia hadithi hizo, bali wamekuwa wanaziiga.
Unaweza kuuliza kwani tofauti ni nini? Nikuambie tu, tofauti ni kubwa sana.
Kuiga ni pale unapofanya kama alivyofanya mwingine wakati kujifunza ni kuielewa misingi na kisha kutumia ulichoelewa kufanya vizuri.
Huwezi kufanikiwa kwa kuiga wengine, hakuna ambaye amewahi kufanikiwa sana duniani kwa kuiga kile ambacho wengine wamefanya.
Hata mtu aliyefanikiwa, kama angekuwa anaanza upya leo na akarudia kila alichofanya, bado hataweza kufanikiwa kama alivyofanikiwa awali.
Hii ni kwa sababu mambo yanabadilika, nyakati zinabadilika na kila wakati unatokea mara moja.
Unachohitaji kwenye hadithi za mafanikio ni kujifunza ile misingi ambayo watu hao waliishi, jinsi walivyoweza kufanya maamuzi sahihi, jinsi walivyoweza kuziona fursa ambazo wengine hawakuwa wanaziona na jinsi walivyoweza kuwa wavumilivu na ving’amg’anizi wakati wengine wanakata tamaa.
Kwa kujifunza na kuielewa misingi, itakusaidia wewe kujijengea misingi ambayo itakusaidia sana.
Usiwe kama kasuku, leo unasikia waliofanikiwa sana wanalala saa nane usiku, unaanza kufanya hivyo. Kesho unasikia wanaamka saa kumi alfajiri, unaanza kufanya hivyo. Unasikia wanakula hivi na wewe unakula kama wao, au wanavaa hivi na wewe unavaa kama wao.
Kuiga kwa namna hiyo, hata ungeiga kwa miaka mingapi, hakutakuwezesha kufanikiwa. Ni kujifunza, kutafakari na kujijengea msingi sahihi kwako ndiyo kutakuwezesha kufanikiwa sana kwenye maisha yako.
Na kumbuka wewe ni wa tofauti na wa kipekee, hakuna mwingine kama wewe, hivyo kuhangaika kuiga wengine ambao hawapo kama wewe, ni kupoteza muda wako. Kuna vitu wengine wanafanya na kufanikiwa ila wewe ukifanya huwezi kufanikiwa. Kadhalika kuna vitu wengine wamefanya wakashindwa ila wewe ukifanya utafanikiwa.
Jifunze kuelewa na kuchukua hatua sahihi zinazoendana na wewe na siyo kuiga kile wanachofanya wengine.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,