Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa The Almanack of Naval Ravikant: A Guide to Wealth and Happiness kilichoandikwa na Eric Jorgenson.

Hiki ni kitabu chenye mkusanyiko wa mafunzo na hekima za Naval Ravikant ambazo amekuwa akitoa kwa njia mbalimbali, kwa sehemu kubwa ikiwa mahojiano mbalimbali (podcasts) na mitandao ya kijamii (twitter).

Naval Ravikant ni Mjasiriamali mwekezaji ambaye amejizolea sifa kubwa kama mwanafalsafa wa zama hizi. Amekuwa akishirikisha hekima mbalimbali kupitia mtandao wa intaneti ila hajaziandika kwa mfumo wa kitabu.

Eric Jorgenson aliiona fursa ya kuzikusanya pamoja hekima zote za Naval kwa mfumo wa kitabu ili wengi zaidi waweze kunufaika nazo. Matokeo yake ndiyo kitabu hiki cha The Almanack of Naval Ravikant ambacho kina mkusanyiko wa hekima zote za Naval ambazo amekuwa anatoa kwa njia mbalimbali.

Eric Jorgenson ameandika kitabu hiki kwa kumnukuu Naval kama anavyoandika mitandaoni au anavyohijiwa kwenye vipindi mbalimbali.

Hekima za Naval zimegawanyika kwenye makundi makuu mawili; UTAJIRI na FURAHA. Hivyo kitabu hiki ni mwongozo wa mtu kuweza kufikia utajiri na furaha kwenye maisha yako.

Uchambuzi wa kitabu utakuwa na sehemu mbili, sehemu ya kwanza itagusa eneo la utajiri na sehemu ya pili itagusa eneo la furaha.

Karibu kwenye uchambuzi uweze kupata mwongozo wa kufikia utajiri mkubwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako.

Utangulizi kutoka kwa Tim Ferriss

Maneno ya utangulizi kwenye kitabu hiki yameandikwa na Tim Ferriss ambaye ni mwandishi na mwekezaji mkubwa ambaye pia ni rafiki wa Naval. Tim anasema miaka mingi iliyopita alifikia uamuzi wa kutokuandika utangulizi kwenye kitabu cha mtu yeyote yule. Ila kwa kitabu cha Naval, imebidi aende kinyume na maamuzi yake hayo kwa sababu maarifa ya kitabu hiki yana manufaa kwa wengi na yeye ni mmoja wa watu wanaomjua Naval kiundani.

Tim anamuelezea Naval kama mtu mwenye akili na ujasiri ambaye amewahi kukutana naye kwenye maisha yake. Naval siyo mtu wa kufuata kundi, bali mtu wa kuutafuta ukweli na kusimama nao hata kama kila mtu anaukataa ukweli huo. Msimamo huo ndiyo umeweza kumletea mafanikio makubwa kwenye maisha yake.

Tim anaendelea kueleza kwamba anawajua watu wengi waliofanikiwa, lakini Naval anatofautiana na wengi wao kwa sababu ni mtu mwenye msimamo. Ni mtu unayeweza kumtegemea afanye jambo sahihi mara zote bila ya kukuangusha. Amekuwa anamuona Naval akipitia vipindi mbalimbali, rahisi na hata vigumu, lakini mara zote hakuvunja msimamo wake.

Naval ambaye ni mkurugenzi wa mfumo wa uwekezaji unaoitwa AngelList, mmoja wa waanzilishi wa makampuni ya Vast.com na Epinions, ambayo baadaye yaliingia kwenye soko la hisa kama Shopping.com, mwekezaji kwenye makampuni makubwa ya teknolojia kama Twitter, Uber, Yammer, OpenDNS, na mengine mengi pia ni mwanafalsafa, ambaye amekuwa akijifunza, kutafakari na kisha kushirikisha hekima anazozipata na kuziishi. Hekima ambazo amekuwa anashirikisha kwa njia mbalimbali, zimekuwa msaada kwa wengi.

Tim anasema vitu vinavyomfanya amwamini na kumkubal Naval ni hivi;

1. Anahoji karibu kila kitu, siyo mtu wa kukubali tu yale anayopewa au kuaminishwa.

2. Anafikiria kwa msingi wa kwanza (haangalii kinachofanyika sasa, anaangalia kama kungekuwa hakuna kinachofanyika ingefanyikaje, yaani kama ndiyo mtu ungekuwa unaanza, ungefanyaje.)

3. Anajaribu vitu mwenyewe kujihakikishia.

4. Anaepuka sana kujidanganya yeye mwenyewe.

5. Anabadili mawazo na misimamo yake pale anapojifunza na kujua kilicho sahihi zaidi au anapogundua amekosea.

6. Ni mtu anayecheka sana.

7. Huwa anafikiri kiujumla (holistically)

8. Huwa anafikiri mambo ya muda mrefu na siyo muda mfupi.

9. Na muhimu zaidi, huwa hajichukulii ‘siriazi’ sana, ni mtu wa utani pia.

Tim anahitimisha utangulizi huu kwa kusema kwamba japo hekima za Naval ni nzuri na zenye manufaa, hupaswi kuzimeza kama kasuku, badala yake unapaswa kuzitafakari, kuhoji na kuzichambua kwa namna unayoweza kuzitumia kwenye maisha yako na ukapiga hatua kubwa.

Siyo lazima ukubaliane na kila anachosema, bali unaweza kutumia kile anachosema kufikiri kwa upana zaidi na kupata majibu ya chochote unachopitia kwenye maisha yako.

Utangulizi kutoka kwa Eric Jorgenson

Kwa kipindi kirefu, Naval amekuwa akishirikisha hekima zake kwa mamilioni ya watu akiegemea kwenye kujenga utajiri na kuishi maisha ya furaha. Wengi wamekuwa wakifuata ushauri wake na kunufaika nao.

Naval Ravikant amekuwa alama ya utamaduni wa kijasiriamali kutoka eneo la Silicon Valley nchini Marekani, eneo linalosifika kwa wajasiriamali walioanzisha makampuni yaliyoibadili kabisa dunia kwa upande wa teknolojia.

Amekuwa mwanzilishi wa makampuni mbalimbali na sasa ni mwekezaji mkubwa kwenye makampuni makubwa na madogo pia.

Kwa maelezo yake na ushauri anaotoa, Naval ni mtu aliyeweza kufikia yale anayofundisha, yaani kuwa na utajiri mkubwa na pia kuwa na furaha kwenye maisha yake.

Watu wengi wamekuwa wakimfuatilia Naval na kupokea ushauri wake kwa sababu ni mmoja ya watu wachache ambao wana mafanikio makubwa na furaha. Kwa walio wengi, vitu hivyo huwa haviendi pamoja na imekuwa inachukuliwa kama kawaida kwamba waliofanikiwa sana hawana furaha. Ila Naval ni wa tofauti, ana mafanikio makubwa na pia ana furaha kwenye maisha yake.

Naval amekuwa anapata hekima anayoshirikisha kupitia kujifunza na kuweka kwenye matendo na kisha kupata matokeo mazuri. Naval ni mtu wa kujifunza mno, amekuwa akisoma vitabu maisha yake yote tangu akiwa mtoto, akipata maarifa mazuri na kuyafanyia kazi.

Kitabu hiki kina mkusanyiko wa hekima ambazo Naval amekuwa akishirikisha kwa njia mbalimbali, ambazo ukizijua na kuweza kuzitumia kwenye maisha yako, utaweza kufikia utajiri na furaha kwenye maisha yako.

Eric anatueleza kwamba kupitia Naval amejifunza mengi ambayo yamembadili mtazamo wake wa jinsi anavyoiona dunia. Kwa kujifunza na kuishi hekima za Naval, ameweza kupata kujiamini na utulivu kwenye safari yake ya kufanikiwa na kuwa na furaha.

Baada ya kujifunza na kuona manufaa ya hekima za Naval, Eric aliona fursa ya kuziweka pamoja hekima hizo kwa mfumo wa kitabu. Kitabu hiki kina mkusanyiko wa hekima za Naval kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, kama alivyokuwa akishirikisha kwenye blogu yake, mtandao wa twitter na mahojiano mbalimbali ambayo amewahi kufanya.

Kupitia kitabu hiki, tunapata nafasi ya kujifunza hekima za Naval na kuweza kuziweka kwenye maisha yetu, ili tuweze kufanikiwa na kuwa na furaha pia.

Wasifu mfupi wa Naval Ravikant

1974 – Kuzaliwa huko New Delhi, India

1985 – Akiwa na miaka 9 – Wanahama kutoka New Delhi kwenda Queens, New York, Marekani.

1989 – Akiwa na miaka 14 – Anaenda shule ya Stuyvesant High School

1995 – Akiwa na miaka 21 – Anahitimu chuo cha Dartmouth (alisomea sayansi ya kompyuta na uchumi)

1999 – Akiwa na miaka 25 – Anaanzisha na kuwa CEO wa Epinions

2001 – Akiwa na miaka 27 – Anakuwa mbia mwekezaji kwenye August Capital

2003 – Akiwa na miaka 29 – Anaanzisha mtandao wa Vast.com, ambao ulikuwa unauza matangazo.

2010 – Akiwa na miaka 34 – Anaanzisha AngelList

2010 – Akiwa na miaka 34 – Anawekeza kwenye kampuni ya Uber

2018 – Akiwa na miaka 43 – Anatajwa kuwa mwekezaji wa mwaka. (Angel Investor of the Year)

Utangulizi kutoka kwa Naval Ravikant

Naval anatushirikisha kwamba alilelewa na mama pekee, ambaye alikuwa na watoto wawili huku akiwa anafanya kazi. Hilo liliwalazimu kuanza kujitegemea mapema kwa sababu mara nyingi walilazimika kuwa nyumbani peke yao.

Walitokea familia ya kimasikini, baba yake akihama kutoka India kwenda Marekani, ambapo ujuzi wake wa Famasia haukupokelewa, hivyo alilazimika kufanya kazi ngumu na familia kuvunjika.

Pamoja na magumu mengi waliyopitia kwenye maisha, Naval anaeleza kwamba mama yao aliwapenda mno na hicho ndiyo kiliwapa nguvu ya kukabiliana na ugumu wa maisha.

Kwa kuwa eneo walilokuwa wanaishi halikuwa salama sana, na kwa kuwa mama yao alikufa anafanya kazi, ilikuwa siyo salama wanapotoka shule kurudi nyumbani na kuwa peke yao. Lakini pia mama yao hakuweza kumudu kulipa ada ya kitu cha kulelea watoto ambapo wangeweza kumsubiria mpaka atoke kazini.

Hivyo walilazimika kwenda maktaba kila wanapotoka shule mpaka pale mama yao alipotoka kazini na kuwapitia. Hiyo ndiyo ikawa ratiba ya kila siku, akitoka shule anaenda maktaba na kukaa mpaka jioni sana. Zoezi hilo lilimfanya asome vitabu vingi tangu akiwa mdogo, kitu ambacho kilimjengea tabia ya kupenda kujisomea lakini pia kumwezesha kuziona fursa mbalimbali.

Lakini pia kwa sababu walikuwa wahamiaji Marekani, hakuwa na marafiki, hivyo muda wake mwingi aliutumia kusoma vitabu. Anaeleza kwamba kwenye utoto wake, marafiki zake pekee walikuwa ni vitabu. Anaeleza kwamba wale walioandikwa kwenye vitabu alivyosoma ndiyo walikuwa washauri wake, wakimpa hekima alizozihitaji sana.

Akiwa na miaka 15 alikuwa tayari ameshafanya kazi mbalimbali za kujiingizia kipato, ikiwa ni pamoja na kusambaza magazeti, kuosha vyombo kwenye migahawa na kusambaza chakula kwenye gari. Alilazimika kufanya kila aina ya kazi ili kupata fedha kwa sababu hali ya maisha ya familia ilikuwa ngumu sana.

Pamoja na kufanya shughuli hizo, aliendelea kujisomea kwa bidii, kitu kilichompa ufaulu mzuri na kuweza kudahiliwa chuo kikuu, akisomea sayansi ya kompyuta na uchumi.

Anatuambia kwa sasa ni mwekezaji, ambaye amewekeza kwenye makampuni zaidi ya 200, huku akiwa mshauri kwa makampuni mengi pia na mjumbe wa bodi wa makampuni mengine mengi.

Pamoja na hayo kwa sasa amekuwa akitafiti na kuwekeza kwenye fedha za kidijitali (cryptocurrencies)

Naval anatushuhudia kwamba alizaliwa kwenye familia masikini na duni, ila kwa sasa ni tajiri mkubwa na mwenye furaha kubwa. Yote hayo yametokea kwa sababu ameyafanyia kazi.

Naval anatuambia; “kuna mambo ambayo nimejifunza kwenye maisha, misingi ambayo naiishi. Najaribu kushirikisha misingi hiyo kwa namba ambayo wengine pia wanaweza kujifunza, lakini mtu anapaswa kuchagua mwenyewe kujifunza, maana siwezi kumfundisha mtu chochote. Ninachoweza ni kukuhamasisha na kukupa baadhi ya misingi ambayo unaweza kusimamia.”

Karibu kwenye uchambuzi.

Karibu usome uchambuzi kamili wa kitabu hiki, ambao una sehemu mbili; sehemu ya kwanza ikielezea mwongozo wa kujijengea utajiri na sehemu ya pili ikielezea mwongozo wa kuwa na furaha.

Uchambuzi kabili wa kitabu hiki cha The Almanack of Naval Ravikant unapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kuweza kuusoma karibu ujiunge na channel hii ambayo ipo kwenye mtandao wa Telegram. Kujiunga na channel fungua kiungo kisha bonyeza JOIN CHANNEL, kiungo ni hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.