Kwenye kila unachofanya kwenye maisha yako, kuna jukumu ambalo ni kuu na muhimu kwako kutekeleza, halafu kuna majukumu madogo madogo.

Jukumu lililo kuu huwa ni gumu na matokeo yake hayaonekani haraka.

Majukumu madogo madogo huwa ni rahisi kufanya na matokeo yake ni ya haraka.

Lakini mafanikio makubwa huwa yanatokana na kutekeleza jukumu lililo kuu.

Ila kwa kuwa watu hawapendi mambo magumu na wanataka kuona matokeo ya haraka, huwa wanahangaika na majukumu madogo madogo na kuacha jukumu kuu.

Wewe hupaswi kufanya hivyo, kwa kila unachojihusisha nacho, jua jukumu lako kuu ni lipi na kisha weka mpango wa kulitekeleza. Kabla hujahangaika na majukumu madogo madogo, hakikisha kwanza umekamilisha jukumu kuu.

Kama wewe ni mwandishi, jukumu kuu kwako ni kuandika yale yenye manufaa kwa wengine kama ulivyolenga. Mengine nje ya hapo ni usumbufu kwako, hivyo weka vipaumbele vyako vizuri.

Kama unafanya biashara, jukumu lako kuu ni kuhakikisha biashara inakwenda kwa kuwahudumia vizuri wateja na kukua zaidi.

Kwa kazi yoyote uliyoajiriwa au kujiajiri kufanya, lijue jukumu lako kuu na lipe kipaumbele jukumu hilo. Utaona wengi wanakimbizana na majukumu madogo madogo na hata kuonekana ni wachapa kazi kweli kweli. Lakini usidanganyike, weka kipaumbele kwenye jukumu kuu, baadaye utazalisha matokeo makubwa sana.

Unapotekeleza jukumu kuu, weka nguvu na umakini wako wote kwenye jukumu hilo na usikubali usumbufu wowote uwe kikwazo kwako. Hili ni muhimu mno kuzingatia kwenye zama tunazoishi sasa, zama zenye usumbufu wa kila aina.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha