Hendry Ford, mtu wa kwanza kugundua na kuzalisha magari kwa wingi alikuwa na msimamo wa kuzalisha magari ya rangi nyeusi tu.

Alipoulizwa kwa nini asisikilize maoni ya watu na kuzalisha magari ya rangi za machaguo yao? Ford alijibu kama angeuliza maoni ya watu wakati wa kugundua gari, wangemjibu hawataki gari, bali wanataka farasi wenye kasi zaidi.

Kabla ya ujio wa magari, usafiri pekee ulikuwa wa kutumia farasi, ndivyo watu walivyozoea kusafiri, hivyo hata kama ungeomba ushauri au kusikiliza maoni yao, wangesema wanachotaka ni farasi wenye kasi zaidi.

Lakini Ford alikuja na kubadili kabisa mchezo, hakuleta farasi wenye kasi zaidi, bali alileta usafiri mpya kabisa, ambao haujawahi kuwepo. Na hilo lilimfanya afanikiwe mno.

Chagua mtu yeyote aliyefanikiwa sana, na utaona kuna namna alibadili mchezo. Aliwakuta watu wanacheza mchezo fulani, yeye akaja na mchezo wa tofauti kabisa na kunufaika wakati wengine wakishangaa na hata kumpinga.

Kwa chochote unachofanya, iwe ni ajira au biashara, jiulize ni kwa namna gani unaubadili mchezo uliozoeleka na wengine, namna gani utakuja na mchezo mpya ambapo utawapoteza wakiwa wanakushangaa na kukupinga. Wanapokuja kustuka ndiyo wanajua kwamba umeshawaacha nyuma sana.

Badili mchezo, hiyo ndiyo njia pekee ya kufikia mafanikio makubwa. Huwezi kufanikiwa sana kwa kufanya kile kinachofanywa na kila mtu kwa namna wanavyokifanya, bali utafanikiwa kwa kufanya kitu cha tofauti, chenye uhitaji mkubwa, lakini hakuna anayejua jinsi ya kukipata.

Kwa mfano wa Ford tulioanza nao, watu walihitaji sana usafiri wa uhakika, lakini hawakuwa na njia nyingine ya kuupata zaidi ya farasi. Ford akaja na njia mpya ya usafiri, akaubadili kabisa mchezo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha