Karibu kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa tunayotaka.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kuinuka na kuendelea na safari baada ya kuanguka kwenye kujiajiri.

Kabla ya kupata ushauri huo, tupate maoni ya msomaji mwenzetu ambaye ametuandikia kuomba ushauri kwenye hilo.

Niliacha kazi nilioajiriwa ili niweze kujiajiri kwenye Kilimo na Ufugaji, toka 2017 lakini mambo mwanzo yalienda sawa ila ,kwa sasa 2020 Nimeanguka kwenye kilimo na mtaji kwa ujumla. Naomba ushauri nifanyeje? – Mdachi K. J.

Msomaji mwenzetu ametushirikisha changamoto yake ya kuanguka kwenye kujiajiri baada ya kuachana na ajira, ambapo mwanzoni mambo yalikwenda vizuri ila baadaye yakabadilika.

Hii ni changamoto ambayo kila ambaye amewahi kupambana kufanikiwa ameshaipitia na ni sehemu ya kupikwa ili uweze kupokea mafanikio makubwa zaidi baadaye.

Anguko ambalo mwenzetu amepata ni darasa kubwa sana kwake kwenye safari ya mafanikio na hasara aliyopata ni ada ya kupata darasa hilo.

Kwa sasa anajua mambo gani akifanya ataanguka na hivyo anapaswa kuepuka kufanya mambo hayo.

Hivyo ushauri wa kwanza na muhimu kabisa kwa yeyote ambaye anapitia magumu au kuanguka ni kutokukata tamaa wala kuangalia kama kitu kibaya. Badala yake ona ni darasa umepitia na kukomazwa ili kuyapokea mafanikio makubwa zaidi baadaye.

Waswahili wanasema kufanya kosa siyo kosa, bali kurudia kosa. Kuna mengi ambayo mtu unakuwa umefanya mpaka ukaanguka. Pia ipo kauli inayosema ujinga ni kufanya jambo lile lile kwa namna ile ile kisha kutegemea matokeo tofauti.

Kwa kuwa hujakata tamaa, unaendelea na kile ambacho ulikuwa umechagua kufanya. Kwa sababu ukilipa ada, lazima uendelee na masomo. Lakini usiendelee kwa kurudia makosa ambayo umeyafanya, ukifanya hivyo utakuwa umepoteza ada yako.

Ushauri wa pili kwenye hili ni kukaa chini na kutafakari kila ulichofanya kwenye mradi wako ulioshindwa. Anza na yale uliyokuwa unafanya wakati mambo yanakwenda vizuri. Kisha nenda kwenye yale ambayo ulikuwa unafanya na mambo yakaenda vibaya. Kisha jua ni mambo gani ambayo hutarudia tena kuyafanya unapoanza mradi wako upya.

Kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja huwa ni chanzo cha kushindwa kwenye yote. Kila kitu kipya unachoanzisha kinakuhitaji mno hasa mwanzoni. Sasa kama unafanya mambo mengi, unatawanya sana nguvu zako na hivyo kila jambo halipati umakini wa kutosha kitu kinachopelekea kushindwa.

Ushauri wa tatu hapa ni kuchagua kitu kimoja tu ambacho utaanza nacho na kuweka umakini wako wote kwenye kitu hicho. Achana na mengine yote, acha kuhangaika na kila fursa inayokuja kwako na kushawishiwa ni bora zaidi. Sikiliza rafiki yangu, fursa bora kwako ni ile uliyoichagua na uko tayari kuifanyia kazi kwa moyo wako wote.

Kama umeamua kulima kitunguu, lima hicho, achana na hadithi kwamba nyanya zinalipa zaidi na kufanya kitunguu na nyanya kwa wakati mmoja. Kama umeamua kufuga kuku fanya hivyo, achana na kelele kwamba sungura au bata mzinga wanalipa zaidi.

Unapokuwa chini, hiyo ndiyo sehemu pekee unayoweza kuanzia. Na uzuri ukiwa chini huna tena pa kuangukia.

Ushauri wa nne hapa ni kuanzia pale ulipo, kuanzia chini kabisa, kuanza kwa hatua ndogo kabisa unayoweza. Kwa kuwa umeshapoteza kila kitu na kwa kuwa umeamua kuanza na kitu kimoja, anza na chochote kilicho ndani ya uwezo wako kwa sasa. Hata kama ni kidogo kiasi gani, wewe anza na pambana kukua kwa kuanzia hapo. Usisubiri mpaka upate uwezo mkubwa wa kuanza, anzia popote pale ulipo sasa. Kama utaanza na sehemu ndogo ya kulima fanya hivyo, kama utaanza na ufugaji kidogo fanya hivyo. Anza kidogo na utazidi kuona fursa za kukua zaidi.

Maisha lazima yaendelee na kama umeanguka kabisa, kuna machaguo mawili, kurudi kwenye ajira itakayokupa msingi wa kuanza tena au kuishi kama mtawa ili kuweza kupambana hapa mwanzoni.

Ushauri wa tano ni kuamua maisha yako yataendeleaje, kwa kuwa umepoteza kila kitu, ina maana hata gharama za kuyaendesha maisha yako huwezi kuzimudu. Hapa unaweza kuchagua kurudi tena kwenye ajira ili upate fedha ya kuendesha maisha yako huku ukijijengea msingi imara zaidi. Au unaweza kuchagua kuishi kama mtawa, kwa kipindi cha mwanzo ambacho unaanza upya, punguza kabisa gharama zako za maisha. Yaani gharamia yale ya msingi tu, mfano chakula na cha kawaida kabisa. Hapa hununui kitu chochote kile cha anasa, yaani ambacho siyo muhimu kabisa. Kwa kufanya hivi unapunguza sana gharama za maisha yako huku pia ukipata muda mwingi wa kuweka kwenye kile unachofanya.

Usimamizi wa uhakika na wa karibu kwenye kitu chochote kile ni muhimu ili kiweze kukua. Kitu chochote kinachoshindwa huwa kinakosa usimamizi na udhibiti mzuri.

Ushauri wa sita ni kuhakikisha unakuwa na usimamizi na udhibiti wa karibu wa kile unachofanya. Yaani hakikisha upo kila wakati na kwa kila hatua inayochukuliwa. Usimuamini yeyote, hata kama anakushawishi na kukuridhisha kiasi gani. Jua kwenye jambo lolote lile, mhusika ana uchungu zaidi na hivyo atafanya maamuzi sahihi zaidi kuliko ambaye ni mjumbe tu. Kama utakuwa na wasaidizi ni vizuri, ila hapa mwanzoni, hakikisha upo mwenyewe kwa kila hatua. Baadaye utaweza kuweka mfumo mzuri, lakini mwanzoni, kila kitu ni wewe.

Maarifa sahihi kwenye kile unachofanya ni muhimu, kuna makosa mtu unaweza kuwa unafanya bila ya kujua na yanakukwamisha na kukuangusha. Wengi huwa wanafanya kwa mazoea kitu kinachokuwa kikwazo kwao.

Ushauri wa saba ni kupata maarifa sahihi juu ya kile unachofanya, chagua vitabu sahihi kusoma kwenye kile ulichochagua kufanya. Kama ni kilimo soma vitabu vya kilimo hicho, kadhalika kwenye ufugaji. Epuka sana maarifa ya kusisimua yanayoshirikisha mitandaoni, wewe nenda kwenye vitabu, jifunze kwa kina na jua hatua sahihi za kuchukua. Pia soma vitabu vinavyokupa maarifa ya jumla na hamasa ili upate nguvu ya kuendelea na safari yako, kwa sababu haitakuwa rahisi kwako.

Kama upo kwenye ajira na unafanya biashara pia au unataka kuanza, soma kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA, kitakupa mwongozo sahihi wa kuanzisha na kukuza biashara au mradi wowote ukiwa kwenye ajira. Changamoto za ufanye nini, muda wako uutumieje na wakati gani wa kuacha ajira zimejibiwa kwa kina kwenye kitabu hiki.

Pia soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA ambacho kinakupa mwongozo wa kuanzisha na kukuza biashara yako. Kitabu kinaigawa biashara kwenye vitengo vyake na kukuonesha yale muhimu kuzingatia kwenye kila kitengo.

Na muhimu zaidi, soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, kwenye kitabu hiki utajifunza umuhimu wa kuwa na akiba ya dharura kitu ambacho kitakukinga usianguke kabisa kwa chochote unachofanya. Hata kama utapata hasara kabisa, utakuwa na mahali pazuri pa kuanzia.

Kupata vitabu hivyo vitatu, wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa vitabu ulipo.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp