Huo unaweza kuwa uhuru wa juu kabisa kwenye maisha yako.

Uhuru huu huwa hautokei tu, bali unatengenezwa.

Na njia kuu ya kuutengeneza ni kufikia uhuru wa kifedha kwanza.

Iko hivi rafiki, kitu kinachopelekea ufanye usichotaka kufanya ni kwa sababu ya fedha.

Umewahi kufanyika utafiti fulani, ambapo matapeli maarufu waliulizwa iwapo wanatambua wanachofanya siyo sahihi, wengi walikiri kujua siyo sahihi, ila walieleza njaa haina adabu. Kama huna fedha, kipaumbele cha kwanza kwako kinakuwa fedha, usahihi au la siyo kipaumbele kikubwa.

Hivyo unapokuwa huna fedha au unategemea mtu mwingine akupe fedha, ambayo unaitegemea sana, huna budi bali kufanya kile anachotaka ufanye, hata kama hutaki kufanya kitu hicho.

Ndiyo maana ni muhimu sana kujijengea uhuru wa kifedha, kuwa na kiasi cha fedha cha kutosha kuyaendesha maisha yako hata kama huingizi moja kwa moja kwa kufanya kazi.

Wamarekani wanaita kiasi hicho cha fedha F*ck You Money, wakiwa na maana kwamba ni kiasi cha fedha ambacho ukiwa nacho unaweza kumkatalia yeyote chochote usichotaka. Hata kama ni bosi wako, upo tayari kumwambia ‘usinizingue’ bila ya kuogopa atachukua hatua gani, kwa sababu unajua hatua yoyote atakayochukua haitakuathiri.

Kuwa na uhuru wa kifedha haimaanishi kuwa na dharau kwa wengine, bali kunamaanisha kuyaishi maisha yako kwa namna unavyochagua wewe.

Kama ambavyo nimewahi kukushirikisha kwenye barua za mafanikio, tuna mahitaji makubwa mawili, uhuru na furaha. Ukiangalia kwa undani, mahitaji hayo mawili yanakuwa moja ambalo ni furaha na ili uwe na furaha unahitaji kuwa na uhuru.

Hivyo kama huna uhuru, huwezi kuwa na furaha, utajikuta unalazimika kufanya vitu usivyotaka, kitu kitakachopelekea uwe na malalamiko wakati unafanya na unapolalamika huwezi kuwa na furaha kwenye maisha yako.

Kufanya kile unachotaka, kwa wakati unaotaka huku ukizungukwa na watu unaowataka ni uhuru wa juu kabisa kwenye maisha. Unaambatana na kutokufanya kile ambacho hutaki kukifanya. Utaweza kufikia huu kwa kuanza na uhuru wa kifedha. Tuweke kazi kufikia uhuru wa kifedha, unatupa uhuru mwingi ambao unafanya tuwe na furaha.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha