
Kila mtu huwa anakosea kwenye maisha. Unapanga hivi lakini unafanya mengine. Unajua unachopaswa kufanya lakini hukifanyi. Hakuna asiyekosea. Lakini kukosea mara moja siyo kikwazo cha mafanikio, bali kukosea kwa kujirudia rudia ndiyo kikwazo. Makosa uliyofanya jana usiyaruhusu yaendelee leo. Badala yake yatambue na kisha leo chukua hatua sahihi. Wanasema kosa siyo kufanya kosa, bali kurudia kosa. Hivyo ni muhimu kujitathmini kila siku, kujua makosa uliyofanya kwenye siku husika ili usiyarudie kwenye siku inayofuata. Mfano kama jana ulitumia fedha kwa jambo lisilo sahihi, haitaleta madhara makubwa, lakini kama utaendelea na leo, kesho na siku zijazo ndiyo inakuwa na madhara. Usikubali kurudia kosa lolote mara mbili, maana hapo utajenga tabia na itakuwa kikwazo kwako. Tambua kila kosa unalofanya na usilirudie tena. Pia usijihukumu sana kwa kukosea mara moja, ukijihukumu utaona ni sawa kuyarudia tena. #NidhamuUadilifuKujituma #AfyaUtajiriHekima #KaziUpendoHuduma