Mijadala inayohusu dini, siasa, michezo na mapenzi, huwa haina mwisho au watu kufikia muafaka.

Hiyo ni kwa sababu watu huingia kwenye mijadala hiyo wakiwa tayari wana upande, na upande waliopo umebeba sehemu ya utu na maisha yao.

Mtu anapoingia kwenye mjadala au mabishano yanayohusu dini, tayari anakuwa upande fulani wa dini. Hivyo habishani kujifunza, bali anabishana kutetea upande anaoamini yeye.

Hivyo kujihusisha kwa namna yoyote ile na mijadala ya aina hii ni kupoteza muda wako bure. Kwa sababu haijalishi utatoa ushahidi mzuri kiasi gani, hutambadili mtu akubaliane na wewe.

Tatizo jingine la mijadala hiyo ni kwamba kila mtu yuko sahihi, kulingana na mtazamo wake, kwa sababu ndiyo kitu anachoamini. Kitu kikishakuwa imani, watu huwa wanakibeba jinsi kilivyo bila ya kuhoji.

Kubadili imani ya mtu ni kitu kigumu, kwa sababu hivyo ndivyo anavyojiona yeye kama mtu. Ukiondoa imani hiyo, hawezi kujitambua yeye tena kama alivyo sasa. Ndiyo maana watu wapo tayari kufa kutetea imani zao.

Hivyo kwa namna yoyote ile, usijihusishe na mijadala au mabishano ya aina hiyo, kwa sababu hakuna chochote utakachonufaika nacho, hutambadili yeyote na wewe mwenyewe hakuna kitakachokubadili.

Kama unataka kuwa na mjadala kuhusu kitu, basi hakikisha kuna njia ya uhakika ya kuweza kufika kwenye ukweli na watu hawabebi kitu hicho kwa imani.

Sayansi imeweza kukua kwa sababu hii, ina njia ya wazi ya kujadiliana na kubishana mpaka kufika kwenye ukweli. Kwenye sayansi unaweza kuja na wazo lolote, kisha ukalifanyia utafiti kwa kukusanya taarifa sahihi, kupata majibu na kisha kuhitimisha. Kama mtu hakubaliani na hitimisho lako, anakwenda kufanya tafiti, kupata majibu na kuja na hitimisho lake.

Hivi ndivyo sayansi imeweza kukua na kuleta maendeleo makubwa, kwa sababu hakuna kitu kimoja sahihi na mtu halazimishwi kuamini, kila kitu kipo wazi kuhojiwa.

Imani na falsafa nyingi zimekuwepo kabla ya sayansi lakini hazijakua kwa sababu hazitoi nafasi ya wazi kwa watu kuhoji na kuufikia ukweli zaidi.

Kwenye sayansi kila kitu kinapingika na hakuna atakayekuona msaliti kwa kukataa wazo fulani linalokubaliwa na wengi, watakachotaka ufanye ni kuwaonesha ushahidi kwa nini unakataa wazo hilo.

Hivyo pia ndivyo unavyopaswa kuyaendesha maisha yako, kwa kuwa tayari kuhiji na kudadisi chochote, kujifunza zaidi ili kuufikia ukweli na kuhakikisha kila unachoamini umeweza kukithibitisha kweli.

Using’ang’ane na chochote ambacho umebebeshwa tu, ambacho hujatumia njia sahihi kufika kwenye ukweli.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha