Huwezi kugawa mimba moja kwa wanawake tisa ili upate mtoto ndani ya mwezi mmoja.

Ili mimba ikamilike na upate mtoto, inahitaji miezi sita. Huo ndiyo muda wa mimba kukomaa na mtoto kutoka akiwa vizuri.

Mtoto atakayezaliwa kabla ya miezi 6 ya mimba hawezi kuishi, hiyo ni kwa sababu viungo vingi vya mwili wake vinakuwa havijakamilika kuweza kuendelea na maisha.

Mtoto anayezaliwa baada ya miezi sita ya ujauzito anaweza akaishi, lakini atahitaji gharama kubwa za madawa na mazingira ya joto kwa sababu viungo vya mwili wake vinakuwa havijakomaa kuweza kujitegemea mwenyewe.

Lakini mtoto aliyefikisha miezi sita ya mimba, anatoka akiwa amekomaa kuweza kuyaendesha maisha yake.

Kwenye mfano huu halisi wa maisha yetu wanadamu, asili inatufundisha kitu kikubwa mno, kwamba ukamilifu wa kitu unahitaji sana muda na hakuna njia ya mkato kwenye hilo.

Lakini dunia imekuwa inatuhadaa, kwa sababu kuna njia za mkato kwenye mambo mengi, pia tunadanganywa kuna njia ya mkato kwenye kufikia ukuu au ubobezi. Hicho ni kitu kisichokuwepo kabisa.

Ukuu na ubobezi ni zao la ujuzi, juhudi na muda. Lazima ujifunze na kujua kweli na kwa uendelevu maana huwezi kufika mahali na kusema umeshajua kila kitu. Lazima uweke juhudi kubwa kwenye hatua unazochukua na ufanye kwa ubora wa hali ya juu. Na lazima ujipe muda, kwa kila unachojifunza na juhudi unazoweka, zinajikusanya na kuja kuzalisha matokeo makubwa baadaye.

Kama ilivyo kwa ujauzito, muda sahihi unapofika, uchungu unakuja na mtoto anazaliwa. Kadhalika kwenye ukuu na ubobezi, muda sahihi unapofika, matokeo makubwa yanapatikana na hakuna anayeweza kuyazuia.

Wewe fanyia kazi yale yaliyo ndani ya uwezo wako, jifunze, weka juhudi na jipe muda. Swala la matokeo usihangaike nalo, yatakuja yatakapokuwa tayari.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha