Watu wengi wanapenda umaarufu, ila huwa hawajali ni umaarufu wa aina gani, una manufaa gani na changamoto zipi zinakuja na umaarufu.

Umaarufu tunaweza kuugawa kwenye makundi mawili, feki na halisi.

Umaarufu halisi ni ule unaotokana na ubobezi ambao mtu amefikia katika kile anachofanya, na ambacho kina manufaa makubwa kwa wengine. Umaarufu huu unachukua muda mrefu wa kujenga, kwa sababu mtu anakuwa anaanzia chini na kuweka kazi kwa muda mrefu mpaka watu waje waone thamani ya kile anachofanya. Umaarufu huu unahitaji uvumilivu kwa sababu kile ambacho mtu anaanza nacho huwa haeleweki mwanzoni. Pia umaarufu huu siyo wa kulazimisha, unakuja wenyewe, mtu hafanyi kitu ili awe maarufu, bali anafanya kwa sababu ndiyo muhimu kwake kufanya na kadiri kinavyokuwa na manufaa kwa wengi anajikuta akifika kwenye umaarufu.

Umaarufu feki ni ule unaotokana na ujinga, ambapo mtu anakuwa maarufu kutokana na ujinga au upuuzi ambao anakuwa ameufanya. Umaarufu huu unakuja haraka na hauhitaji kazi, lakini huwa ni umaarufu usio na manufaa, hauongezi thamani yoyote kwa mtu na pia haudumu na mtu muda mrefu. Umaarufu huu huja haraka na kuondoka haraka na huharibu kabisa sifa ya mtu. Hata kama mtu atanufaika na kujulikana, huwa ni kwa njia isiyo na manufaa makubwa kwake.

Katika zama tunazoishi sasa, zama za mitandao ya kijamii, imerahisisha sana watu kupata umaarufu feki, kufanya mambo ya kijinga yanayofanya wajulikane na kila mtu lakini hakuna manufaa makubwa ambayo mtu anapata.

Na kwa kuwa ni asili yetu binadamu kupenda vitu rahisi, wengi wameingia kwenye mtego wa kujenga umaarufu feki kwenye mitandao hiyo ya kijamii.

Ya nini uweke miaka kumi kwenye kazi ambapo hakuna anayekutambua kwa miaka yote hiyo wakati unaweza kuweka picha ya uchi mtandaoni na ndani ya siku moja kila mtu akajua kuhusu wewe? Ya nini uhangaike kujenga biashara imara kwa kuwajali wateja wako na kuwauzia kilicho sahihi kwao wakati unaweza kuwasumbua na matangazo yenye ushawishi na kuwalazimisha kununua?

Unaweza kuona hapo kwa nini ubobezi unashuka sana kwenye zama hizi, kwa sababu njia za kufikia umaarufu feki ni nyingi na rahisi kutumia hivyo kila mtu anakimbilia kuzitumia.

Kwetu sisi wanamafanikio tunapaswa kuepuka sana njia hiyo. Kwanza kumbuka lengo letu kubwa ni uhuru, siyo umaarufu au kingine chochote. Kukimbizana na umaarufu ni njia ya uhakika ya kujinyima uhuru. Utafanya mambo ambayo baadaye yanakuwa kikwazo kwako.

Hivyo tuachane kabisa na dhana ya kuhangaika na umaarufu, badala yake tuhangaike na kile tunachotaka kubobea, kile tunachotaka kukifanya kwa sababu ndiyo namna pekee tunaweza kuishi hapa duniani.

Tuwe tayari kujenga misingi sahihi, misingi ambayo itatunufaisha kwa muda mrefu hata kama hakuna anayetuona na kutusifia sasa. Muhimu kwetu ni kufanya kile kinachotoa thamani kubwa kwa wengine na siyo kinachotupa tu sifa zisizo na tija.

Waache wengi wakimbizane na umaarufu feki, sisi tunakwenda kuweka kazi, tukiwa tumejipa muda, tunakwenda kubobea zaidi kwenye kile tunachofanya na umaarufu utajijali wenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha