Kanuni za kisayansi, hasa kanuni za fizikia, ni kanuni ambazo zinatokana na asili.

Hiyo ina maana kwamba kanuni hizo zinafanya kazi kila mahali na kwa kila hali.

Moja ya kanuni hizo ni kuhusu mwendo, ambayo inasema kitu kilichosimama kitaendelea kusimama na kilicho kwenye mwendo kitaendelea na mwendo mpaka nguvu ya nje ibadili hali ya kitu husika.

Japokuwa kanuni hiyo inaongelea mwendo, lakini inatumika kwenye kila kitu kinachohusu maisha yetu.

Na leo tunakwenda kuitumia kwenye kujua nini unapaswa kufanya.

Kama kwa sasa hujui unapaswa kufanya nini na hivyo hufanyi, utaendelea kubaki kwenye hali hiyo hiyo ya kutokufanya.

Na kama kuna kitu unafanya, utaendelea kwenye hali hiyo hiyo ya kufanya.

Tuchukue mfano labda unataka kuingia kwenye biashara, lakini hujui ni biashara gani ufanye, utabaki kwenye hali ya kutokuingia hivyo hivyo. Lakini kama utaamua kwamba ufanye biashara yoyote, utakuwa kwenye hali ya kufanya na utaendelea kwenye hali hiyo na uzuri ni kwamba hali hiyo ya kufanya itakufikisha kwenye biashara sahihi kwako kufanya.

Kwa chochote unachopanga kufanya lakini kwa muda mrefu hufanyi, chagua kuanza kufanya kwa namna yoyote ile. Ni kupitia kufanya ndiyo utajua kipi sahihi kwako kufanya.

Mara nyingi unaweza kuwa na mpango mzuri wa nini unafanya, lakini unapokuja kuanza kufanya unagundua siyo sahihi hivyo unapaswa kubadili na kuboresha. Hivyo usikae bila kufanya kwa sababu hujui nini unapaswa kufanya, anza kufanya chochote na hilo litakufikisha kwenye kilicho sahihi.

Mkwamo wowote ule unaweza kutatuliwa kwa mtu kuanza kufanya chochote, hivyo unapojikuta umekwama, angalia kipi unaweza kuanza kufanya na anza na hicho.

Hata kwenye uandishi, kama umejiambia utaandika kila siku na ikatokea siku unaona huna cha kuandika, anza kuandika kwa nini huna cha kuandika na haitakuchukua muda utajikuta tayari una mengi ya kuandikia.

Safari moja huanzisha nyingine, mwendo huzaa mwendo, mara zote hakikisha unakuwa kwenye mwendo badala ya kujikwamisha kwa sababu hujui mwendo upi sahihi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha