Kama unataka ushindi kwenye maisha, basi wasaidie wengine kushinda.
Kwa wengine kushinda, watakufanya na wewe upate ushindi pia, tena ushindi ambao utadumu.
Kwa chochote unachofanya, angalia ni kwa namna gani wengine wananufaika kwanza kabla hujaangalia wewe unanufaikaje. Weka maslahi ya wengine mbele kama unavyoweka yao, lakini anza kwa kuangalia maslahi yao kisha yako.
Hii ina maana kwamba, kwa chochote unachofanya, angalia kwanza wengine wananufaikaje, ukishaona kuna manufaa wengine wanapata, basi angalia na wewe unanufaikaje.
Lazima ushindi uwe kwa wote.
Ukiangalia maslahi yako tu na kutokujali wengine wananufaikaje, unaweza kushinda, lakini hautadumu kwenye ushindi huo na anguko lako litakuwa kubwa.
Ukiangalia maslahi ya wengine bila kujali yako utawanufaisha, lakini hutaweza kufanya hivyo kwa muda mrefu, utachoka na kushindwa.
Lazima pande zote ziwe zinapata ushindi, na kadiri ushindi unaowapa wengine unavyokuwa mkubwa, ndivyo ushindi wako unakuwa mkubwa pia.
Iwe ni kazi au biashara unafanya, angalia wale unaowalenga wananufaikaje, wafikirie kwa namna wanavyonufaika na kila mara angalia fursa za kuwapa ushindi.
Hilo litapelekea ushindi mkubwa zaidi uje kwako pia. Usihofu kwamba wengine watajinufaisha kupitia ushindi unaowapa, wewe jua ushindi mkubwa zaidi utarudi kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,