Watu wengi wamekuwa hawaielewi vizuri dhana ya jehanamu.

Wanachoelewa ni kwamba kama utafanya uovu au dhambi, utakapofika mwisho wa dunia basi utahukumiwa kwenda jehanamu na kuteseka milele. Mateso ya huko yameelezewa kuwa mengi na makali, ikiwepo kuchomwa moto.

Dhana ya jehanamu ni adhabu ambayo mtu unaipata pale unapokuwa umefanya uovu fulani. Na hiyo haihitaji usubiri mpaka siku ya mwisho, kwani jehanamu unaishi nayo sasa.

Jehanamu ambayo watu wanaishi nayo ni msongo na kukosa furaha. Na hivyo humtokea mtu pale anapovunja maadili yake mwenyewe, pale anapofanya kitu anachojua siyo sahihi kufanya.

Unapofanya hivyo, nafsi yako inakusuta kwa kile ulichofanya, unakuwa na msongo na hilo linapelekea usiwe na furaha. Hata kama hakuna mwingine aliyekuona ukifanya kitu hicho, bado ndani yako unajua siyo sahihi na hilo litakuumiza sana.

Utulivu na furaha kwenye maisha huwa ni matokeo ya kuyajua maadili unayoyasimamia na kutokuyavunja. Kutokufanya kitu chochote ambacho siyo sahihi. Siyo kwa sababu unaogopa wengine watakuona, bali kwa sababu unajua ukifanya kisichokuwa sahihi utakuwa umechagua kuishi kwenye jehanamu yako hapa duniani.

Katika kutafuta mafanikio, wengi wameshawishika kutumia njia zisizo sahihi, wanapata pesa na mali lakini haziwapi utulivu na furaha. Mafanikio yao yanawapa msongo mkubwa na kuwanyima furaha. Na ndiyo maana wengi wakiwaangalia wanasema mafanikio hayaleti furaha.

Hakuna kitu chochote duniani kinachompa au kumnyima mtu furaha, bali namna mtu anavyofanya na kuchukulia kitu hicho ndiyo kunafanya apate au kukosa furaha.

Unapoyasimamia maadili yako, unapunguza sana msongo na ukishakuwa na utulivu lazima utayafurahia maisha. Hilo lipo ndani ya uwezo wako, bila ya kujali uko kwenye hatua gani ya maisha yako.

Yajue maadili yako na yasimamie kwa gharama yoyote ile, kwa sababu kuishi kwenye jehanamu ya hapa duniani ni kugumu na kunaumiza kuliko ugumu wa kuyaishi maadili yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha