Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, huwa hatuwezi kuwa na utulivu tukiwa peke yetu. Tunapata amani na utulivu tunapojua ni sehemu ya jumuia fulani.
Ndiyo maana ni rahisi vijana wanaobalehe kuingia kwenye makundi yenye ushawishi mbaya kwao. Wanakuwa kwenye kipindi cha mabadiliko kwenye maisha yao, ambapo wanataka kuondoka chini ya uangalizi wa wazazi na kujiamulia mambo yao wenyewe.
Katika kipindi hicho, kuwa kwenye kikundi cha wengine ambao wanaonekana kufanya kile wanachoamua wenyewe na kinachopingana na mamlaka nyingine, inaonekana ni jambo sahihi kwao.
Sasa tunaweza kuwashangaa vijana hao wanaokua, lakini hata watu wazima wana tabia hiyo. Kuna vikundi na jumuia mbalimbali umejiunga nazo, ili tu kutimiza hitaji lako la kuwa ndani ya jumuia, lakini hazina manufaa kwako.
Mfano unaweza kuwa na marafiki ambao huwa mnakutana kufanya starehe tu. Au kwenye eneo la kazi au biashara mna kama kikundi cha kujadili na kufuatilia maisha ya wengine.
Unaweza ukawa sehemu ya vikundi vya aina hiyo bila ya wewe kujua, kwa sababu ni hitaji la ndani, unajikuta umelikamilisha bila kujua.
Kwa kujua uhitaji mkubwa tulionao wa kuwa kwenye vikundi na jumuia, tunapaswa kuwa makini ni vikundi au jumuia gani tunachagua kujiunga navyo.
Kama tunavyojua, wale tunaotumia nao muda wetu mwingi wana ushawishi mkubwa kwetu. Hivyo tunapaswa kujihusisha na watu ambao watatusaidia kufika kule tunakotaka kufika.
Kama hakuna jumuia ya aina hiyo ya kujiunga nayo, anzisha yako, chagua wale ambao mnaendana na wenye kiu ya kupiga hatua kubwa kwenye maisha, kisha pendekeza mpango wa kuwa na kikundi au jumuia. Ukiwa na pendekezo zuri, lenye manufaa kwa wote, mtaweza kuwa na jumuia iliyo bora na yenye manufaa kwa kila mmoja.
Epuka sana kutekwa na kuingia kwenye vikundi au jumuia zisizo na mchango katika kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha, najifanyia tathimini kila jumuia na vikundi nilivyonavyo ili kuchagua vikundi na jumuiya yenye manufaa kila mmoja wetu.
LikeLike
Vizuri Tumaini.
LikeLike
Kweli kocha napaswa kuchagua jumuia sahihi ambayo ina manufaa kwa wote
LikeLike