Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa Ten Arguments for Deleting Your Social Media Accounts Right Now kilichoandikwa na Jaron Lanier.

Tunaishi kwenye zama za maarifa na taarifa na mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya kusambaa kwa haraka kwa taarifa mbalimbali.

Lakini pia mitandao hii imekuwa na madhara mengi ukilinganisha na faida zake, imeharibu maisha ya watu kuanzia binafsi, mahusiano, kazi, biashara na hata mataifa na dunia kwa ujumla.

Mtaalamu wa teknolojia na mmoja wa waanzilishi wa mtandao wa intaneti Jaron Lanier anatupa hoja kumi kwa nini tunapaswa kuachana kabisa na mitandao hiyo mara moja.

Kumbuka huyu ni mtu ambaye amehusika kwenye kuanzisha mtandao wa intaneti na ana uelewa wa ndani wa jinsi mitandao hii inavyoendeshwa na madhara yake. Hivyo ni mtu sahihi tunayepaswa kumsikiliza kwa hoja kumi anazotushirikisha kupitia kitabu chake.

Kuhusu mwandishi.

Jaron Lanier (Kuzaliwa Mei 3, 1960) ni mwanasayansi wa kompyuta, mwandishi na mwanamuziki wa nchini Marekani. Jaron ni mmoja wa waanzilishi wa matumizi mbadala ya mtandao wa intaneti ambapo mwaka 1985 alishiriki kuanzisha kitengo cha utafiti wa uhalisia wa kutengenezwa (virtual reality).

Miaka ya 1990 mwishoni alishiriki kwenye kuboresha mtandao wa intaneti na kuufanya uwe wazi kwa matumizi ya watu wote. Awali mtandao wa intaneti ulikuwa unatumika na serikali pekee, ni mpaka miaka ya 1990 ndipo ulikuwa wazi kutumika na kila mtu.

Amefanya kazi na makampuni mengi makubwa ya teknolojia ikiwepo kampuni ya Microsoft. Na hilo limempa nafasi ya kuwa na uelewa mkubwa kwenye teknolojia hiyo.

Nje ya teknolojia amekuwa mwandishi wa vitabu na muziki na pia mkusanyaji wa sanaa na vitu adimu. Mwaka 2010 jarida la TIME lilimweka Lanier kwenye orodha ya watu 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.

Vitabu vingine ambavyo Jaron ameandika ni Dawn of the New Everything, Who Owns the Future?, You Are Not a Gadget: A Manifesto na Wenn Träume erwachsen werden (When Dreams Grow Up).

Kazi zake nyingi za uandishi zimekuwa na lengo la kuwasaidia watu kuepuka changamoto na madhara ya mtandao wa intaneti na teknolojia kwa ujumla.

Uzoefu wa mwandishi na msukumo wa kuandika kitabu hiki.

Mwandishi anatushirikisha uzoefu wake kuhusu mitandao ya kijamii kabla hata ya kuwepo kwa mitandao ya kijamii tuliyoizoea sasa.

Jaron anasema alianza kutumia kompyuta na intaneti miaka ya 1970, kipindi hicho hakukuwa na mitandao ya kijamii iliyopo sasa, ila kulikuwa na mifumo rahisi ya kuwasiliana kwa kushirikisha maoni pamoja.

Alipoanza kutumia mfumo huu wa mawasiliano, aligundua kitu ambacho hakikuwa sahihi. mara kwa mara kuliibuka mabishano baina ya watu katika mijadala wanayofanya pale ambapo walishindwa kuelewana kwenye kitu fulani. Mabishano hayo yalipelekea ugomvi na watu kutukanana.

Anasema hali hiyo ilianza kuzoeleka lakini kwake aliona siyo sawa. Siku inaweza kuanza vizuri watu wakiwa wanashirikiana kwenye shughuli zao, lakini inapotokea watu wameshindwa kuelewana kwenye kitu kidogo basi mabishano makali yaliibuka na kuivuruga siku kabisa.

Kwa kuwa mijadala hiyo ilikuwa inafuatiliwa na watu wengi, watu walijikuta wakibishana ili tu kushinda hata kama haina maana. Lakini pia alijikuta ndani yake akisukumwa kuigiza ni mpole ili asiingie kwenye mabishano ya aina hiyo. Na hapo ndipo alipoiona hatari, kuishi maisha ya maigizo.

Kwa kuona hatari hiyo alichagua kutokutumia tena huduma hiyo ya mijadala, kwa sababu kila alipoitumia hakujisikia vizuri, hakujisikia akiwa yeye halisi.

Miaka ya 1990 watu marafiki zake walikuja na mfumo mwingine wa kutengeneza jumuia kwenye mtandao, walimtengenezea akaunti lakini hakuwahi kuitumia, kwa sababu hakutaka kurudi kwenye kile alichoona mwanzo.

Miaka ya 2000 mwanzoni, Arianna Huffington alishawishi awe anaandika makala kwenye blog yake ya Huffington Post. Alikubali na makala zake zilikuwa na wasomaji wengi, lakini tena akajikuta anarudi kule kule kwenye mashindano ambayo hakuyataka. Alijikuta akisukumwa kuandika siyo kwa sababu anataka, ila kwa sababu wasomaji ndiyo wanasoma zaidi vitu fulani. Alijikuta akifuatilia zaidi maoni ya wasomaji wa makala zake na kuangalia wengine wanaandika nini. Alijiona akianza kuishi maigizo na hapo akaacha mara moja kuandika makala kwenye blog hiyo iliyokuwa maarufu.

Jaron anasema asichotaka kwenye maisha ni maigizo, hataki kuigiza kwamba ni mtu mwema, anachotaka ni kuwa mwema kiuhalisia na siyo kutaka kuonekana au kuwaridhisha wengine. Lakini amegundua ni vigumu sana kuwa mwema kiuhalisia kupitia mtandao wa intaneti. Ndiyo maana mpaka leo hatumii mtandao wowote wa intaneti, iwe ni Facebook, Twitter, WhatsApp, Instagram, Snapchat au mingine.

Anasema ukiingia kwenye mtandao wa Twitter, kuna akaunti inaitwa @RealJaronLanier lakini siyo yeye na hamjui anayeitumia.

Jaron anasisitiza kwamba hajioni yeye ni bora kuliko wengine kwa sababu hatumii mitandao ya kijamii, ila anajua hawezi kuhimili misukosuko ya mitandao hiyo. Na kwa namna anavyoona maisha ya wengine yanavyobadilika, anashawishika wengi zaidi hawawezi kuihimili, ndiyo maana anashauri kila mtu anayetaka kuwa na maisha bora na tulivu basi anapaswa kuacha kutumia mitandao hiyo mara moja.

Jaron anaeleza kitabu hiki ni zao la swali ambalo waandishi wengi walikuwa wanamuuliza pale alipokuwa anazungumza nao kuhusu kitabu chake kilichotoka kabla ya hiki. Waandishi walimuuliza anaona upi mchango wa mitandao ya kijamii katika kuiharibu zaidi dunia, alikuwa akiwajibu lakini aliona ipo haja ya kuziweka vizuri hoja hizo kwa kuonesha madhara ya mitandao hiyo.

Hivyo alikusanya hoja kumi muhimu zinazobeba madhara yote makubwa ya mitandao ya kijamii na kuziwasilisha kupitia kitabu chake. Na msisitizo wake ni mmoja, mitandao ya kijamii haiwezi kubadilishwa kwa namna ilivyo sasa, inapaswa kusukwa upya na njia pekee ya kushinikiza hilo ni kuacha kuitumia mara moja.

Waandishi wengi wamekuwa wanashauri mtu ajidhibiti kwenye matumizi, lakini kwa jinsi Jaron alivyoonesha madhara yake, hilo haliwezi kusaidia. Kitu pekee cha kufanya anasema ni kuacha kuitumia kabisa, mara moja, sasa hivi bila ya kusubiri.

Karibu kwenye uchambuzi, tuzipate hoja hizo kumi na kisha kufanya maamuzi sahihi kama bado mtu hujaachana na mitandao hiyo ya kijamii.

Kupata uchambuzi wa kitabu hiki, kuzijua hoja kumi kwa nini uachane na mitandao ya kijamii kabisa, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kujiunga fungua; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.