Wanaojua sana huwa hawaongei na wanaoongea sana huwa hawajui, hii ni kauli iliyotolewa miaka mingi iliyopita na mwanafalsafa wa China aliyeitwa Lao Tzu.
Ungeweza kufikiri watu wangekuwa wamejifunza kuhusu hilo, lakini ni udhaifu wetu binadamu, tunajikuta tukiongea sana pale ambapo hatujui na kuwaamini wale wanaoongea sana.
Na hapa swala siyo kuongea sana, bali kuonesha kwamba tayari unajua kila kitu.
Watu wanaamini wanajua kila kitu ni watu hatari sana, kwa sababu huwa hawana nafasi ya kujifunza. Na haijalishi wanajua kiasi gani, mambo yanabadilika na hivyo kujikuta wanarudi nyuma.
Kwa miaka ya nyuma, kulikuwa na wanafalsafa walioamini wamesoma vitabu vyote vilivyokuwa vimeandikwa kwa kipindi chao. Lakini leo hii atakayesema hivyo atachekwa, vitabu vipya vinavyochapwa kwa siku moja tu, hakuna anayeweza kuvisoma na kuvimaliza hata kama atapewa miaka 100 na kazi yake iwe ni hiyo ya kusoma tu.
Hivyo katika maisha, tunapaswa kuwa wanyenyekevu, bila ya kujali tunajua kiasi gani, kwa kujua kuna mengi tusiyojua, kuna mengi mapya yanakuja kila siku, tuwe tayari kujifunza.
Lakini pia kwa wale tunaoona tunajua kuliko wao, hatupaswi kuwadharau kwa kuona hatuna cha kujifunza kwao, kuna mengi ya kujifunza kwa kila mtu, hata kama ni yale ambayo hatupaswi kuyafanya.
Pale unapoanza kujiona unajua kila kitu, ndiyo wakati unaopaswa kuchukua tahadhari kubwa na kurudi kwenye unyenyekevu mkubwa na kujua kuna mengi hujui.
Na pale unapofanya kwa mazoea kwa kujiambia ndivyo umekuwa unafanya, ni wakati wa kupitia upya kwa namna unavyofanya kisha kujifunza upya mabadiliko ambayo yameshatokea kwenye kile unachofanya.
Ogopa kuwa anayejua kila kitu, jifunze kila wakati na utajua ni kwa kiasi gani kuna mengi hujui na hivyo kulazimika kuwa mnyenyekevu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Hakika sijui kila kitu. Nitatumia mtazamo huu kujifunza kila siku.
Asante sana Kocha.
LikeLike
Vizuri Datius
LikeLike