Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa Economics in One Lesson kilichoandikwa na Henry Hazlitt.

Toleo la kwanza la kitabu hiki lilitoka mwaka 1946 na kugusia makosa mengi ya kiuchumi ambayo huwa yanafanywa na serikali mbalimbali katika kutunga na kutekeleza sera za kiuchumi.

Miaka 30 baadaye, mwaka 1978, mwandishi alitoa toleo la pili, ambapo bado changamoto na makosa ya kiuchumi yamekuwa ni yale yale. Hapo somo kubwa likiwa ni kwamba serikali za mataifa mbalimbali huwa hazijifunzi hata kwa makosa yao wenyewe.

Kwenye kitabu hiki, mwandishi anatupa somo moja la uchumi na kisha kuonesha kwa mifano jinsi watu na hasa serikali imekuwa inafanya makosa ya kukiuka somo hilo na kuleta madhara makubwa kiuchumi.

Wengi tumekuwa tunaona uchumi ni kitu kikubwa na kilicho nje ya uwezo wetu, hivyo hatujisumbui kujua misingi yake. Lakini sera na mipango mbalimbali ya kiuchumi inaathiri maisha yetu moja kwa moja.

Hivyo kwa kujua somo hili na kupata mifano iliyolifafanua, utaweza kujua madhara ya kila sera na jinsi ya kuhakikisha hayawi kikwazo kwako. Kupitia kitabu hiki tutaona jinsi sera za kiuchumi za kila taifa humgusa mtu mmoja mmoja na matokeo yake kuwa tofauti na ilivyotegemewa.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu, tujifunze somo kuu la uchumi na kuona madhara yake kupitia mifano mbalimbali.

Utangulizi.

Kitabu hiki ni uchambuzi wa makosa ya kiuchumi ambayo yamekuwa yanajirudia rudia kiasi cha kuchukuliwa kama ni kawaida.

Licha ya kuwepo kwa shule mbalimbali za kiuchumi na kuwa zinakinzana inapokuja kwenye sera mbalimbali, bado kila upande umekuwa unafanya makosa kwenye sera inazotetea.

Makundi hayo huwa yanatofautiana kwenye kukubali makosa yao na kubadili msimamo, kuna ambao huwa wanawahi na wengine huchelewa, lakini kwa ujumla, wote huwa wanakosea.

Hakuna serikali yoyote ile duniani ambayo sera zake za kiuchumi haziathiriwi na makosa ya kiuchumi ambayo yamezoeleka. Hivyo ili kujua vizuri jinsi uchumi unavyokwenda, ni vyema kwa kuyajua makosa hayo ya kiuchumi na kuona madhara yake.

Hivyo kupitia kitabu hiki, mwandishi anatushirikisha somo kuu la uchumi, kisha kuonesha kwa mifano jinsi kukiuka somo hilo kumeleta madhara mbalimbali ya kiuchumi duniani.

Mwandishi anaeleza wazi kwamba makosa haya siyo mapya, yamekuwepo tangu kuwepo kwa mifumo ya kiuchumi. Pamoja na madhara yake, bado yamekuwa yanarudiwa.

Kitabu hiki kimeandikwa zaidi ya miaka 60 iliyopita, ungeweza kufikiri dunia itakuwa imejifunza na kubadili sera za kiuchumi, lakini sivyo. Kama ambavyo tutaona kwenye uchambuzi, makosa yale yale yamekuwa yanajirudia mpaka sasa.

Sehemu Ya Kwanza; SOMO.

Sura Ya I; Somo.

Uchumi unaandamwa na makosa (fallacies) mengi kuliko tasnia nyingine yoyote. Na hii ni kwa sababu uchumi ni moja ya masomo magumu na linaloathiriwa zaidi na hisia za watu kuliko masomo mengine kama hisabati, fizikia au sayansi nyingine.

Kwenye uchumi huwa kuna makundi mbalimbali ambayo yanapingana, huku kila kundi likilinda maslahi yake na kuonesha maslahi ya kundi jingine siyo sahihi.

Kuna wakati maslahi ya makundi mbalimbali huwa yanaingilia na hapo makundi hayo hukubaliana.

Baadhi ya sera za kiuchumi huwa zinayanufaisha makundi yote kwenye jamii, lakini sera nyingine hunufaisha kundi moja na kuumiza kundi jingine. Na katika makosa haya, kuna sera ambazo zinaishia kuyaumiza makundi yote.

Changamoto nyingine kubwa ya makundi ya uchumi ni mtazamo ambayo yanakuwa nayo. Kuna kundi linaangalia matokeo ya muda mfupi na kupuuza ya muda mrefu, huku kundi jingine likisisitiza matokeo ya muda mrefu yazingatiwe.

Kwa kuangalia vitu hivyo viwili, maslahi na mtazamo, tunaweza kuwagawa wachumi kwenye makundi mawili, wazuri na wabaya.

Wachumi wazuri ni wale wanaoangalia maslahi ya wote na kuangalia matokeo ya muda mrefu ya sera husika. Wachumi wabaya ni wale wanaoangalia maslahi ya kundi moja na kupuuza ya makundi mengine, huku wakiangalia matokeo ya muda mfupi na kupuuza yale ya muda mrefu.

Kuwa mchumi mzuri inaonekana rahisi kusema, lakini kwenye utekelezaji ni ngumu, kwa sababu inakwenda kinyume na mazoea yetu binadamu. Fikiria jinsi mlevi anavyoweza kutumia pombe kwa kiwango kikubwa, huku akijua kabisa kwamba akishalewa atauumiza mwili zaidi. Au mtu mwenye kipato kidogo ila matumizi ni makubwa, akijua kabisa hilo linazidi kumwangusha kwenye umasikini.

Kwa haya tuliyojifunza hapa, tunalipata somo kuu la uchumi ambalo ni; sanaa ya uchumi ni kuzingatia maslahi ya makundi yote na siyo kundi moja pekee na kuangalia matokeo/madhara ya muda mrefu na siyo ya muda mfupi pekee.

Sera nzuri ya kiuchumi ni ile inayozingatia maslahi ya makundi yote yanayoguswa na sera hiyo, huku ikiangalia matokeo au madhara ya muda mrefu ya sera hiyo.

Tisa ya kumi ya matatizo yote ya kiuchumi duniani yanatokana na kupuuza somo hili la msingi kabisa kuhusu uchumi. Makosa hayo huwa yanatokana na kuangalia maslahi ya kundi moja na kupuuza ya makundi mengine, na kufuatilia matokeo ya muda mfupi huku ikipuuza matokeo ya muda mrefu.

Sera nyingi za kiuchumi huwa zinatungwa kwa lengo la kusaidia kundi fulani ambalo linaonekana kutokunufaika. Na matokeo yanayoangaliwa huwa ni ya muda mfupi. Lakini sera inapotekelezwa, makundi mengine yanaathirika na matokeo ya muda mrefu yanakuwa ni kinyume na matokeo ambayo sera ilitegemewa kuzalisha.

Kinachopelekea makosa haya ya kiuchumi kuendelea kuwepo ni wachumi wabaya ambao huweka maslahi yao mbele, huku wakitetea sera zao mbaya kwa lugha yenye ushawishi kuliko wachumi wazuri wanavyoweza kupinga sera hizo.

Wachumi hao huwa na ushawishi mkubwa kwa sababu hawaoneshi uhalisia wote, bali wanaonesha sehemu ya uhalisia inayowashawishi watu. Wanaonesha matokeo ya muda mfupi ambayo yatakuwa mazuri kwa kundi moja, lakini hawaoneshi matokeo ya muda mrefu ambayo yatakuwa mabaya kwa makundi yote.

Ukweli wa kila sera ya kiuchumi ni kwamba inaweza kuwa na matokeo mazuri kwa kundi husika ndani ya muda mfupi, lakini kwa muda mrefu, inakuwa na matokeo yasiyo mazuri na makundi yote kuathirika. Kuelezea hilo kwa namna ya kuweza kueleweka na umma ni vigumu na ndiyo maana sera mbaya za kiuchumi zimekuwa zinakubaliwa.

Baada ya kulipata somo kuu la uchumi, sasa twende tukapate mifano itakayotusaidia kulielewa vizuri, ili tuweze kujua madhara ya kila sera ya uchumi inayopitishwa.

Kupata uchambuzi wa makosa hayo ya kiuchumi yanayofanywa kwenye sera za serikali mbalimbali, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.