Watu huwa wanapenda kuficha matatizo, ili wengine wasiyajue au kuyaona, kwa kudhani wanawalinda kwa kufanya hivyo.

Lakini watu siyo wajinga, wanakuwa wanajua pale mambo yanapokuwa hayaendi sawa, hivyo kuwaficha ni kujidanganya mwenyewe.

Watu watakuheshimu zaidi kama utakuwa muwazi, mkweli, mwaminifu na unayeshirikisha mkakati wa kutatua tatizo lililotokea. Watakuwa tayari kukuunga mkono katika kukusaidia kwenye hilo.

Lakini yote hayo ni kama utaacha kuyaficha matatizo na kuyaweka wazo kwa wale ambao yanawahusu na kuwagusa moja kwa moja.

Kuficha matatizo hakusaidii kuyatatua, badala yake kunaibua tetesi na maneno ya chini chini, ambayo yanalichochea zaidi tatizo husika.

Hii ni kwenye uongozi, kazi, biashara, mahusiano na katika kila hali inayohusisha watu. Hata kwenye biashara, usijaribu kuwaficha wateja wako tatizo linalokuwepo kwenye biashara, kwa sababu watakuwa wanajua wazi kuna kitu hakipo sawa.

Binadamu wana namna ya kipekee ya kuhisi pale mambo hayaendi sawa, na wanapokuwa hawapewi maelezo ya kutosha, huwa wanatengeneza maelezo yao wenyewe, ambayo huwa siyo sahihi.

Maelezo hayo yasiyokuwa sahihi huwa yanasambaa kwa kasi kubwa sana na kufanya tatizo lizidi kuwa kubwa. Hatua ya kwanza ya kukabiliana na tatizo na kulizuia lisikue ni kutokulificha, kulielezea kwa uwazi kwa wote linaowahusu na kujenga ushirikiano mzuri katika kulitatua.

Watu wapo tayari kwenda hatua ya ziada, kufanya kazi zaidi, kulipa gharama kubwa zaidi kukusaidia kutatua tatizo unalokuwa unapitia. Wanachohitaji ni uwazi na ushirikiano wako tu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha