Gereza kubwa ambalo mtu anakuwa amefungiwa maisha yake yote, huwa amelitengeneza yeye mwenyewe.

Gereza hilo huwa linatokana na matarajio ambayo mtu anakuwa nayo kwenye maisha yake.

Kinachowafungia watu kwenye gereza hilo ni nguvu kubwa mbili, maumivu na raha.

Watu hufanya vitu vinavyowapa raha na kuepuka vitu vinavyowapa maumivu.

Jamii nzima imejengwa kwenye nguvu hizo mbili, kuwapa watu raha pale wanapofanya vitu fulani na kuwaadhibu pale wanapofanya vitu ambavyo jamii haitaki.

Watu hudhani kwa kupata raha na kuepuka maumivu ndiyo watakuwa na furaha kwenye maisha yao, lakini hilo halitokei.

Njia pekee ya kuepuka gereza hilo la maisha na hata kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha ni kutokujali kuhusu raha au maumivu. Pale vitu hivyo vinapokuja kwako, vipokee kama vinavyokuja bila ya kuonesha tofauti yoyote.

Kama kuna mazuri umefanya na raha ikaja, ipokee kama inavyokuja, usitamani ije kwa wingi au ikae na wewe muda wote, jua ni kitu cha muda tu.

Na kama umefanya makosa na maumivu yakaja, yapokee kama yanavyokuja, usitamani yaondoke haraka, jua yataondoka kwa wakati wake.

Unachopaswa ni kuweka umakini wako kwenye wakati uliopo, kukabiliana na kilicho mbele yako kwa wakati huo na siyo kuhangaika na matamanio fulani.

Falsafa mbalimbali na hasa ya Ustoa, zinatufundisha vizuri jinsi ya kutekeleza hili, la kutokujali kuhusu maumivu wala raha, bali kujali kuhusu kile kilicho mbele yetu kwa wakati husika.

Tunashindwa kuyafurahia maisha yetu kwa sababu tunahangaika na mengi ambayo hatuna uwezo wa kuyaathiri. Kama kuna kitu muhimu kuhangaika nacho, basi ni kile kilicho mbele yetu kwa wakati husika, kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya.

Kwa kufanya hivyo, hutasumbuka na maumivu wala raha, kwa sababu havitapata nafasi ya kukusumbua, utakuwa umetingwa kweli kweli na kilicho mbele yako hivyo hutaacha mwanya wa yasiyokuwa muhimu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha