Utajiri ni utambuzi wa fikra kwanza kabla ya kupatikanika katika maumbile yake. Wale wanaotambua hili basi huanza na kubadili kufikiri kwao kisha utajiri unaweza kuvutwa kirahisi. Fedha ni sehemu tu ya aina za utajiri ambazo watu wengi wanajua. Lakini kuna aina za utajiri mbali na fedha ambazo si wengi wana utambuzi huu. Karibu tuone hatua 22 za safari ya kutambua utajiri na maisha ya furaha.

1. Kwanza kabisa lazima utambue wale ambao wanaweza kufanya makubwa maishani huwa wana utambuzi wa namna Dunia ifanyavyo kazi au vitu vinavyofanya kazi “how things work”. Kisha kwa kujua huko wanaendana na huo mfumo wa mambo ulivyo. Utambuzi wa Dunia inavyofanya kazi ni maarifa makubwa ambayo yamefanya watu wengi waje na ugunduzi, ubunifu na kutengeneza utajiri mkubwa tofauti na wale wasio na utambuzi huo.

2. Ufahamu wa muda unatenganisha watu katika kuyaelewa maisha. Muda ni kiinimacho “Time is illusion” kwa watu wengi. Ukiondoa fikra basi umeondoa uwepo wa muda. Hivyo muda pekee ambao ni halisi ni sasa. Kwa wanaopanga malengo basi kwa kujua hili hupanga malengo yao kama yameshakuwa sasa

3. Maisha ni ujenzi wa picha akilini mwa mtu. Fikra na hisia za mtu zinapoumba picha ndivyo mtu anavyovuta maisha yaliyo sawa na picha anazoruhusu ziwe katika fikra zake.

4. Kufikiri huzalisha mawazo na mawazo ni nguvu yenye umbo. Mara ngapi jambo uliloliwaza halafu baada ya muda likatokea ?. Basi hii ndiyo nguvu ya uvutano ya mawazo na kutokea kwa kitu katika umbo. Wenye utambuzi huu hudhibiti mawazo yao wakijua mawazo ni maumbo yanayoweza kutokea.

5. Watu wengi hawana ufahamu wa kina wa kupanga malengo yanayoendana sawa na Dunia inavyofanya kazi na hivyo kujikuta hawapati matokeo sawa na malengo yao. Wenye utambuzi wa kuyahusianisha malengo na ulimwengu unavyofanya kazi basi huwa wanapata matokeo wanayoyataka.

6. Ili uweze kuumba kitu lazima kwanza uruhusu uwe (State of being). Ili upate utajiri lazima kwanza ujione ndani yako utajiri kisha uchukue hatua za malengo ya kukufanya uwe utajiri kisha upate utajiri kwa kuuona katika umbo. (Formula ni kuwa, kufanya na kupata). Lazima upitie (TO, BE & HAVE). Ila wengi hupuuza hii formula ndo maana kutengeneza maisha mazuri au utajiri ni safari ngumu kwao.

7. Bila kuchukua hatua huwezi kupata ulichokifikiri. Kuchukua hatua ni kuruhusu kitu kiweze kutokea. Hata kama utafikiri vizuri, utapanga malengo vizuri na ukakosa kuchukua hatua hakuna utakachokipata.

8. Lazima uwe na utambuzi kuwa ulimwengu una utele kuliko uhaba. Uhaba ni vile fikra zako zilivyo.

9. Sheria ya asili ya kupanda na kuvuna kadri unavyoweza kuitambua utakuwa unajua namna ya kutengeneza matokeo utakayo kwa kuangalia upande nini ili uvune nini. Hii ni sheria mama ya kutengeneza utajiri na maisha ambayo ungependa yawe kwa uzuri.

10. Kuna watu hukosea pale wanapoangalia utajiri kuwa una mazingira fulani pasipo kujua ni kitu kinachotengenezwa tokea ndani.

11. Mafanikio na kufeli ni pande moja ya shilingi. Kufeli ndio njia ya kujua usahihi wa jambo na ukafanikiwa. Wenye utambuzi huu basi huona kila hatua ya kufanikiwa kwao kufeli ni sehemu ya mafanikio pia.

12. Kuna vitu ambavyo huangusha watu kuwa na utajiri na furaha. Na hili lazima uliepuke ( ndani ya kitabu hiki tutajifunza namna ya kufanya hivyo )

13. Swali la nini kusudi la maisha yangu ? Nipo naishi ili iweje ni muhimu sana kujiuliza. Kitabu hiki kimejibu vizuri kiasi cha kushibisha kiu yako.

14. Utoaji ni njia ya utajiri. Wenye utambuzi huu wanajua ili ufanikiwe na kujifahamu wewe ulivyo basi kwa njia ya kujitoa kuanzia vipaji, muda wako ndivyo utakavyoweza kujifahamu zaidi.

15. Watu wengi wanadharau nguvu iliyopo katika kushukuru. Kushukuru kuna Nguvu kubwa ya kuvuta maisha bora.

16. Utambuzi (Consciousness) ndio kikwazo cha watu wengi washindwe kupata baadhi ya vitu maishani hata kama vipo. Kadri unavyokua ki utambuzi utaona Dunia ina utele na sio uhaba tena kama uonavyo sasa.

17. Wewe ni mjenzi wa kwanza wa maisha ulonayo. Wewe ni kisababishi cha matokeo unayoyapata nje. Kama hivyo maisha mazuri na mabaya yapo kwako mtengenezaji.

18. Kila kitu kinahusiana na vyote vipo katika umoja. Wale wanaojua hili basi wanatambua namna kwa jambo dogo linaweza kuumba matokoe makubwa.

19. Dunia ni tele na wewe ni sehemu ya utele huu. Ndani yako kuna uwezo usioweza kupimwa ukaisha.

20. Ili ufanikiwe na kuwa na furaha lazima urejee katika asili yako na hapo ndipo chimbuko la furaha na utajiri wako.

21. Fedha ni kiinimacho na ijue fedha halisi ni ipi itakupa hatua za juu sana katika maisha.

22. Unapojua haya basi wasaidie wengine kujua na uwafundishe kujua ndivyo utajiri unavyoweza kusambaa kwa wengi.

Huu ni mwanzo wa safari ya kitabu hiki. Hakika hutakuwa ulivyokuwa. Hebu chukulia uzito katika haya na maisha yako hayatakuwa yalivyokuwa.

1. Ulimwengu na maelezo ya vitu vyote kama nishati yenye maumbo mbalimbali.

Unapokuja kuelewa Dunia na vyote vilivyomo unaweza kuelewa kwa ngazi rahisi ya kuwa kila kitu ni nguvu/nishati yenye maumbo tofauti tofauti.

Ukianza na wewe ulivyo. Mfumo wako wa mwili umejengwa kwa nguvu au nishati. Unapokula chakula kilichotengenezwa na mwanga wa jua ambao ni nishati. Hata mfumo wa mwili kwa maana ya viungo, tishu hadi chembe chembe zote zinafanya kazi sababu ya uwepo wa nguvu/nishati.

Ufahamu huu wa namna nishati ndio kiini cha uumbaji wa maumbo mbalimbali kuanzia mtu hadi vitu ndio unaofanya wengine waone namna Dunia ina utele wa ajabu unaofanya mambo yawezekane kutokea.

Fizikia ya Dunia inaonyesha namna Dunia ina uwezekano mkubwa wa kutokea kwa kitu chochote kwa namna nyingi. Dunia inavyofanya kazi ni zaidi ya muda na nafasi (Time, space & matter).

Ni sisi ndio tunaona umbali katika muda na nafasi katika utokeaji wa vitu. Ndo maana watu wanapopanga malengo wanayaweka mbali na muda na nafasi. Lakini ulimwengu haupo hivyo katika utendaji wake wa mambo usozuilika katika muda na nafasi.

Ulimwengu upo katika kuruhusu vitu vitokee sasa bila kujali muda na nafasi. Ndo maana kuna malengo unaweza kupanga yatokee mwaka 2030 ukakuta yamewezekana hata sasa.

Nishati huzunguka katika maumbo. Kila kitu ni nguvu ambayo inafanya wengine tuone maumbo. Kadri unavyotazama kitu ndivyo unavyoweza kukiona kipo na ukiacha kutazama kinapotea katika uhalisia.

2. Ukweli kuhusu Muda: Muda ni kiinimacho kwa mtizamo huu.

Muda ni kiinimacho ambacho cha kundi kubwa la watu. Watu wametengeneza kiini macho hiki katika fikra zao. Hebu umepata nafasi siku unayolala na kuamka unaweza kuona umelala kwa kipindi kifupi japo kwa nje ni masaa 08 au 10 yamepita tu. Ukiondoa kufikiri basi muda haupo.

Katika namna ya mwili muda unaonekana katika jana na ijayo na wakati huo watu wakisahau huwezi kuishi jana kiumbo na huwezi kuishi kesho kiumbo isipokuwa kwa mawazo na hisia zinazozunguka ndani yako ambazo hazizuiliwi na muda wala nafasi. Mwili wako ni kikwazo cha wewe kuweza kusafiri kama yalivyo mawazo na picha unazoweka kichwani kwako.

Mwili upo sasa na muda ulio nao ni sasa. Yote ambayo utawaza na kujenga picha yanatokea sasa. Hata ukikumbuka ya jana na kuiangalia ijayo kwa nafasi ya akili na roho bado kimwili uko sasa.

Hivyo maana halisi ya muda ni sasa. Kila kitu unachokihitaji ukitaka ukiwezee kukivuta basi kione sasa. Ona unacho sasa na jiandae kupata sasa. Dunia haizuiliwi na muda na hivyo wakati wowote kutoka sasa kwa njia ambazo ni za ajabu zilizo juu ya kufikiri kwako vinaweza kutokea kwako.

Hivyo ili uweze kupata unachokitaka maishani basi kione wakati wa sasa. Jiambie wewe ni tajiri, jiambie wewe ni mtu bora, jiambie wewe ni mshindi na andika malengo yote kama umeshayapata sasa.

Wakati sahihi wa kupata chochote ni sasa. Ndani yako huanza kuwa na kisha nje wewe hupata. Huu ndio mtizamo muhimu wa muda unaopaswa kuwa nao sasa. Hata malengo watu wanayopata kuwa matajiri, kuwa watu mahiri basi huanza kujiona tayari wameshakuwa na kwa namna ya ajabu wakati wowote fursa, mazingira hujivuta kuwapa kutokana na hali zao ndani (States of Being)

3. Maisha ni picha unazoruhusu katika fikra zako (The Blueprints of Life)

Picha unazoruhusu kujiona katika maisha yako hazitakuacha pasipo kutaka kuumba katika uhalisia. Picha unazoruhusu kujiona ni kama unajiambia unataka iwe hivyo. Unaporuhusu mawazo ya kujiona u mtu duni, huwezi basi Dunia itakupa mazingira yote ya kukudhibitishia kuwa huwezi kweli. Hili ndilo linalowatokea wengi wanakosa mambo ambayo wanayohitaji wapate.

Picha hizi huanza na mawazo na huvuta hisia. Pale unapojiona u tajiri basi kuna hata hisia zinakujia za kuona u mtu uliye tajiri. Kwa kuwa wenye utambuzi huona umuhimu wa kujiona tayari wamepata walichokihitaji basi hulisha akili zao za picha za kile kitu wanachokihitaji kwa kukiona tayari kimekuwa, tayari wako nacho wanakishika, tayari wanahisi hali ndani yao ya kuwa na hicho kitu kwa wakati wa sasa.

Binadamu ndio kiumbe pekee ambaye bila kupewa uwezo wa kujenga picha (imagination) basi ugunduzi, mabadiliko na ubunifu wa mambo ungekuwa kazi. Kwa njia ya ujenzi wa picha watu huona tumaini la kutokea kwa nyakati nzuri wakati unaonekana ni baadaye lakini huja kuwa sasa.

Hata ukiangalia Maisha yako utaona unachoweza kuelezea miaka 10 ilopita na hapo jana kinakuja ndani yako kama picha tu. Watu, matukio yote ni kumbukumbu za picha.

Ukibadili picha au kuona ndani yako basi umebadili maisha yako ya nje. Shughulika na unachokiona kuanzia ndani ili uvute unachopenda kitokee katika maisha yako.

4. Unachokifikiri na kuongea ni mawimbi unatuma ya mambo kutokea.

Utakuwa umewahi kusikia kuwa maneno huumba basi sio maneno pekee ila hata unachokifikiri kina nguvu ya kuwa umbo. Hivyo mawazo na maneno ni mawimbi unayotuma pasipo kujua yanayokuwa ni maumbo yatokeayo.

Umewahi ona siku unafikiri kitu au mtu ana akatokea au ukasema jambo na likawa ?. Umewahi jiuliza kwanini huwa hivyo?. Basi kwa wenye utambuzi wanajua kuwa mawazo na maneno yanaweza kuwa mlango wa mambo mengi kutokea iwe kwa uzuri au ubaya.

Maisha yako yanaweza kuwa bora kwa ubora wa kufikiri na udhibiti wa unayoyaongea maishani mwako. Unapokosa usawa wa unachofikiri na kuongea basi unakosa kupata kile ulichokuwa unahitaji. Wengi huongea tofauti na kile unachofkiri. Dunia na asili huwa haipendi unafiki. Pale unapokosa kueleweka unachoongea kuwa tofauti na unachokifikiri basi hutoa upenyo wa chochote kije kwako.

Hivyo ukiweza kuwa sawa na unachoongea na ndicho unachokifikiri basi unatuma maelekezo sahihi ya kupata unachotaka upate maishani.

5. Malengo yako yafanane na unachofikiri na kuongea na kutenda. (Goals: The Road map to and in wealth )

Kama ambavyo tumeona hapo awali kuwa kila kitu ni nishati/nguvu yenye kuwa katika maumbo tofauti tofauti. Na hii nguvu ikikosa kuwa na uelekeo maalumu ndio inafanya ubaya pia. Mfano ni umeme unavyoweza kutumika vibaya unaleta madhara makubwa na ukitumika kwa uzuri unaleta manufaa.

Basi ndani ya kila mmoja wetu ana nguvu hizi katika mawazo, hisia na maneno. Nguvu hii ikitumika vibaya ndio huzalisha mawazo mabaya, hisia hasi na maneno hasi yenye kutoa matokeo sawa na fikra na hisia.

Unapoweka lengo basi unafanya hii nguvu ielekezwe sehemu mahususi ya kwenda. Ndo maana malengo utaambiwa upange yenye kuwa uelekeo fulani ili uweze kupata unachokitaka. Wengi wanakosea kupanga malengo wanapoyagawanyisha kuyaona ni malengo yasio sasa.

Malengo yote yaweke kuwa yameshakuwa sasa ili uweze kuruhusu asili kufanya kila nafasi ya kuweza kutokea. Unapojiambia kuwa wewe ni tajiri sasa basi ni kama kutuma mawimbi katika pande zote za utele wa asili kuwa ikupe unachokihitaji.

Malengo yako yashike katika fikra zako na maneno yako. Ndo maana huwa tunahimizwa kuyaandika, kuyafikiri na hata kuyatamka wazi wazi. Kwa njia hizi unaonyesha namna unahitaji malengo hayo yaweze kutimia wakati wa sasa.

Bila malengo hiyo nguvu ndani yako itafanya chochote na hutapata matokeo utakayo. Kuwa na malengo ni kufanya uwezo ulio ndani yako ufuate mkondo wake.

Ni kama vile maji yanayokosa mkondo huenda popote tu. Kuwa na malengo uelekeze nguvu zako kuumba ulichokifikiri na kutamka.

 6. Kuwa (Being) ndio mwanzo wa safari ya kufanikiwa.

Wengi wanakosa kupata kile wanachokitaka hasa eneo la utajiri sababu ndani yao bado hawajakuwa (state of being). Lazima ujione kwanza umeshakuwa mtu mwenye furaha kabla ya kuwa na furaha. Ujione utajiri kabla ya kuwa tajiri ( kwa maana kabla hujapata/kudhihirika katika umbo ).

Ukiangalia watu wote wanaoweza kupata vitu kirahisi basi huanza kujiweka hizo hali ndani yao kuwa tayari wameshakuwa au kupata kile ambacho wanataka kukipata. Ndo maana utahimizwa kuwa na imani kuwa tayari ulichokiwaza kimeshakuwa. Kufanya hivi ni kufanya urahisi wa kupata chochote unachokitaka kwa kuanza na kuwa katika hali hiyo.

Kuna vitu utaweza kupata mpaka uwe kwanza ndani yako na kisha vitokee. Wengi hawapati wanayotaka kupata sababu ndani yao hawajioni wameshakuwa katika hali hizo.

Kitu chochote ukitaka upate kirahisi kianzie kwa kujitengenezea hali ya kuwa tayari. Kuwa tajiri ndani yako, kuwa na furaha ndani yako, kuwa mbunifu ndani yako na kisha chochote kile ulichokuwa tayari kitavuta mazingira nje sawa na ndani yako ulivyo.

Utakuwa umewahi sikia aonavyo mtu nafsini mwake ndicho alivyo. Basi huu ni ukweli kabisa. Unaofanya wengine wafanikiwe sana sababu huanza ndani kujiona wamefanikiwa tayari.

Anza kuwa ndani yako. Jione tayari mambo unayotaka uwe nayo yameshakuwa na kisha ondoa hofu. Weka imani na hilo kisha muda wowote kutoka eneo lolote itakuwa nje ( umbo la kitu au umbo la hicho ulichokuwa )

7. Chukua hatua upate ulichokifikiri na kuongea au kuwa (Actions: That which receives)

Kuchukua hatua ni ngazi ya mwisho ya kupata ulichofikiri na kukiwekea lengo lako. Bila kuchukua hatua huwezi kupata. Haitoshi kufikiri, haitoshi kuwa au kuongea bila kuonyesha hatua za kufanya. Kuchukua hatua ni hatua ya mwisho ya kupata kitu kwa uhalisia wake.

Watu wote ambao wamefanikiwa sana basi wanatambua kuchukua hatua ndio kitofuatishi kati ya wanaopata na wasiopata. Watu watafikiri lakini huwa hawachukui hatua ndo maana hawapati wanachotaka.

Kuchukua hatua ni sehemu ya uhalisia wa maneno. Hivyo mawazo, hisia na maneno yote hutafuta njia ya kujionyesha kiumbo lakini bila kuchukua hatua hayo mawazo, hisia za kitajiri haziwezi kuzaliwa  likawa umbo.

Kuchukua hatua kunazalisha uwezekano Mkubwa wa kufungua utele katika maisha yako. Anza kuchukua hatua maana hujui hizo hatua zitakufungulia mlango gani katika maisha yako

8. Ukijua namna ya vitu hutokea basi utaamini. Imani ni kiungo muhimu kufanya mambo yatokee.

Walimu wengi wa kiroho na hata maandiko Matakatifu yanahimiza juu ya imani. Kuamini ni muhimu sana katika kufanya vitu unavyofikiri vitokee. Imani huja kuwa kubwa pale unapojua kilicho nyuma ya Pazia huwa kinaendaje. Sheria kama ya kupanda na kuvuna mtu anavyoelewa basi huamini katika kupanda kutakuwa na kuvuna. Hivyo ataweka udhibiti mzuri wa upandaji wake.

Kila kitu kitaweza kutokea na kuwa na umbo kulingana na ngazi ya kuamini na kukua kiimani.

Unapokuwa na imani na kitu unahitaji kuondoa mashaka na hofu kuwa ulichofikiri hakiwezekani. Wengi wamefeli kupata wanachofikiri au kutenda sababu ya kujaa mashaka na hofu kuwa itakuwa kweli au kutokea kweli ?

Kila kitu kinaweza kutokea pale unapokuwa umekomaa katika kukiamini kutokea kwake na ukiwa umejiondoa na mashaka na hofu zinazoletwa na ngazi ya mwili ambayo huwa ina ukomo wakati wote na kuwa kikwazo.

Unapoamini usiache kuchukua hatua ya kitu na kufanyia kazi. Maana wanasema imani iso na matendo imekufa. Lazima pawe na utendaji kisha mambo yatatokea

9. Sheria mama ya Ulimwengu: Kisababishi na matokeo (Law of Cause & effect)

Hii ni sheria mama ya ulimwengu inayofanya kazi hata sasa. Matokeo ya kitu husababishwa na kitu. Hivyo hakuna kitu kinatokea bahati mbaya hapana sema watu huwa hawana utambuzi wa juu wa vitu vyake ndo maana utaona wengine wakishindwa kujua inakuaje. Lakini kila kitu kina sababu au chanzo chake kabla ya matokeo.

Kwa wanaotambua hili basi ili wapate matokeo wanayoyataka huanzia na chanzo kisha chanzo kikibadilika basi matokeo yatabadilika. Wengi wanakosea wanapotaka kubadili matokeo huku chanzo ni kile kile. Hapa ni kujiumiza kwa watu wengi sana.

Kila kitu chenye matokeo kina chanzo. Chanzo kina nguvu na ndipo penye mwanzo wa mambo mengi. Chanzo cha kufanikiwa wengi wanakosea kujua na kutafuta nje yao wasijue ndani yao ni mwanzo wa mambo ya nje.

Yote ambayo yanatokea nje huanza na chanzo cha mawazo na hisia. Hapo ndio mwanzo wa mambo mengi kuanza na wakati wowote huzaliwa Katika umbo. Mawazo ni mbegu inayoota na kuzaa.

Hivyo ili upate kuwa na kupata utajiri lazima ushughulike na chanzo chako. Mawazo, hisia, picha unazoruhusu ili upate matokeo ya kitajiri. Bila hivyo huwezi kufanikiwa kama chanzo cha mawazo ni yale yale siku zote.

10. Ulishafanywa kuwa na utajiri kiroho unahitaji kutambua na kuamka sasa

Utakuwa umewahi kusikia vitabu vingi vya kusema umezaliwa tajiri (You were born rich) lakini kwanini watu hawahi matajiri ?. Jibu dogo ila kubwa ni kuwa wamekosa utambuzi huo kuwa ndani yao wana utajiri.

Utajiri huu ulio kwa kila mmoja mpaka aamke na kutambua ni utele usoweza kuelezea. Unapoweza kufikiri sasa na kutembea katika ulimwengu wa fikra pasipo kukoma ndivyo ilivyo sehemu ndogo ya utele unaoweza kuona ulivyo. Hapo hujaja jinsi pia ulivyo kiumbe wa Kiroho uliye na muunganiko na Nguvu ya Kiungu ilivyo kubwa kusaidia kukufanikisha kupata vitu katika mwili.

Ulimwengu wa fikra na roho hauna mipaka kama ulivyo mwili. Mwili unachoka, unakufa lakini nafasi ya kiroho ina Nguvu ya kuishi mbali na muda na nafasi (Beyond space & time).

Ndo maana watu wote wanaoona vitu katika picha ya ndani kwa maana ya kifikra na kiroho huona namna hakuna kitu kinaweza kuwa ni changamoto maana nafasi hizi za Fikra na roho hazina ukomo. Ukitaka kuona hili hebu jaribu kuishi wakati wa sasa kimwili maeneo 7 tofauti na ukawepo kama utaweza. Ikiwa huwezi hilo na fikra na roho zinaweza kusafiri maeneo zaidi ya 7 huoni ndani yako huu ni utajiri mkubwa na utele ?

Kuna nukuu moja inasema kuwa watu kama watatambua uwezo mkubwa ndani yao basi watajiogopa ilivyo na ukuu wa ajabu.

11. Changamoto, kufeli ni sehemu ya hadithi za mafanikio. Kusema kufanikiwa ina maana kuna kitu umeshinda.

Wengi hutoa maana mbaya ya kufeli au kushindwa katika maisha. Watu wanasahau pasipo kushindwa kusingekuwa na mafanikio Katika maisha yao. Kushindwa kwao ndiko kulitoa nafasi kwao wafikiri njia bora za kufanya vitu. Hivyo changamoto, kufeli ni vipande vya mafanikio bila hivyo hakuna mafanikio.

Mafanikio ni ushindi fulani. Lazima pawe na kitu ambacho umeshinda iwe kuanzia ndani kufikiri, kuhisi hadi kutenda. Lazima ngazi zote ukabiliane na vikwazo ili kufanikiwa.

Hivyo watu wanaotaka kufanikiwa halafu wanakimbia changamoto wanayakimbia mafanikio. Mafanikio na changamoto ni pande mbili za shilingi. Ukitatua changamoto unafanikiwa.

12. Unataka nini maishani?. Usisahau unavyofikiri, maneno, matendo na hali yako ya kuwa (states of being) husema unachohitaji pasipo wewe kujua?

Moja ya swali gumu kwa watu wengi ni juu ya nini wanachokitaka maishani. Nini shauku wanayotaka kuifikia maishani. Hapa ndo penye matatizo mengi ya wengi kupata ambavyo hawakutaka wapate sababu hawakujua wanataka nini.

Akili zetu zina nguvu kubwa sana. Na unapokosa kuwa na uwazi (clarity) basi huchukua mawazo unayowaza au hisia ulizonazo na kukufanya pasipo kujua uchukue hatua ambazo matokeo yake si yale uloyataka.

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa wazi maishani kuanzia mawazo, hisia, maneno na matendo yako kuwa hiki ndicho nikitakacho na si kingine. Bila hivyo kupata unachokitaka na unawaza vingine huwezi kupata.

Njia rahisi kujua kipi unachokitaka basi andika usivyovitaka na vile vinavyobakia ndo unavyovitaka. Basi viumbie picha, hisia, mawazo na vichukulie hatua katika maisha yako.

Ukifanya hivi unakua huchanganyi taarifa Katika Asili na hivyo utapata unachokitaka. Hata Kiroho himizo hili lipo la kuwa wazi unapoomba kwa Mungu unataka atende nini

13. Kwanini upo Duniani?. Nini kusudi lako kuu la Maisha? (Hata wewe unajiuliza swali hili)

Kusudi ni kazi. Hivyo uwepo wa kitu chochote chenye umaana basi lazima utaelezea katika mlengo wa kazi. Kazi ndio mhimili wa kusudi lolote la kitu. Uwepo wako upo kufanya kazi gani ?. Au kwa maana rahisi unachangia nini kuifanya Dunia iendelee.

Sisi binadamu ni viumbe wa kiroho na uwepo wa roho ndio unatusukuma kuishi katika kusudi hilo la kuchangia kadri tuwezavyo kuonyesha vitu vilivyo katika ulimwengu usoshikika wa fikra na roho uonekane katika umbo. Nafasi hii ya kazi hufanya fikra na roho zitafute kuishi katika umbo na maumbo ndo maana nafasi ya kuumba vitu iko ndani yetu.

Uumbaji ni sehemu ya kazi na kusudi la Maisha yetu kuwa tubuni, kuumba kwa uendelevu wa Dunia. Hivyo vipaji, ujuzi, uzoefu wote una hatma moja ya uendelevu wa vitu katika nafasi ya maumbo ya mwili yaliyo asili ya roho na fikra.

Hivyo rejeo la kusudi kutoka katika asili ni muhimu sana maana vyote vinavyoonekana visingeweza kuwa pasipo visivyoonekana kuwepo.

Upo hapa kuwa sababu ya kuchangia uendelevu wa vitu na utele uliopo. Hakuna siku eneo lolote litaweza kujaa lisiendelee. Ndo maana kwa kila maeneo bado watu watakuwepo wasiokoma. Walikuwepo waandishi, wapo na watakuwepo pasipo uhaba. Hivi ndivyo Dunia hufanya kazi.

Utambuzi wa kazi unayotakiwa ufanye katika ujenzi wa Dunia iwe bora basi huambatana na zawadi ya Upendo wa kufanya hicho kitu, utoshelevu wa hali ya juu na furaha isowezwa kuelezewa.

14. Huwezi kujijua ikiwa wewe hutoi vilivyo ndani yako. Ubinafsi huzua utajiri

Sheria nyingine mama ya kukuletea utajiri na kukuonyesha wewe ulivyo basi ni kwa njia ya utoaji. Maisha ni mwangwi hivyo unavyotoa ndivyo kioo chako ulivyo.

Kuna msemo huu wa kingereza nimeona katika hiki kitabu by taking care of society and nature, you take care of yourself. Share with and give to nature and society often kwa maana kwa kujali jamii yako na asili basi ndivyo unavyoweza kujisaidia mwenyewe katika jamii yako. Huu ni ukweli kabisa maana maisha ni mwangwi.

Kile unachokifanya kinakurudia kama kilivyo. Umewahi kukaa eneo la pango kisha ukaita sauti basi sauti hiyo hiyo ndio inayorudiwa. Hivyo ni sawa maishani ukifanya kitu ni mwitikio wa kile utakachokuwa umetoa.

Kadri unavyotoa muda wako, ujuzi, maarifa ndivyo na wewe unavyoweza kupata zaidi maana ndio asili iko hivyo. Umewahi ona ukifundisha wengine ndivyo unavyokijua kitu kwa undani. Hili ni moja yako mengi sana.

Hata katika utajiri kadri unavyoweza kuwasaidia wengine wawe na utajiri basi na wewe wakati huo una nafasi ya kuwa na utajiri wa mali. Asili ni nishati na hivyo nishati hurudi kadri inavyozunguka.

Kadri unavyotoa kwa wengine unaongeza kasi ya mzunguko wa nishati Duniani na hivyo unapata zaidi. Jaribu katika Biashara zako utaona kadri wateja wanavyopata huduma nzuri toka kwako ndivyo habari zako zinavyoenea zaidi.

Epuka u binafsi na anza kutoa kadri uwezavyo kuisaidia Dunia na wakati huo unajisaidia mwenyewe.

Hii ndio zawadi yangu siku hii ya kumbukizi ya kuzaliwa kwangu. Nitatoa maarifa kadri Ninavyoweza najua kuna mtu mmoja atasaidika na kusaidia wengine wengi

15. Utapata vitu vilivyo katika ngazi ya utambuzi wako (You experience what you are awake to)

Utakuwa umewahi kusikia mbuzi hula urefu wa kamba yake. Hili haliko katika methali pekee lisiwe katika uhalisia wake. Ni kweli katika maisha utapata vitu vilivyo katika ngazi ya utambuzi wako. Ikiwa mwingine hatatambua kuwa Dunia ni tele ni kazi kuelewa wengine wanaposema Dunia ni tele kwa kuwa hilo hana utambuzi nalo.

Ukikosa utambuzi maishani ni sawa na kuwa na macho lakini usiweze kuona au ni sawa na kutembea katika usingizi mzito usijue mambo yakoje. Utambuzi ni njia ya mafanikio na wale wote wenye kufanikiwa basi hujisukuma kutambua uwezo mkubwa ndani yao.

Utambuzi wa utajiri ni muhimu kwa kila mtu ambaye anataka kuona utajiri ukidhihirika. Ukikosa huu utambuzi basi umaskini huwa unakuwa kama ukungu usione uhalisia.

Hivyo kadri unavyowasaidia wengine wawe na utambuzi wa kitajiri (Wealth Consciousness) basi hujisaidii wewe ila unasaidia mamia ya watu Duniani. Maana utambuzi wa vitu ni utele mkubwa!..

Je ni furaha ilioje kama haya maarifa ya kitabu hiki iwe imewafikia watu wote milioni 50 Dunia ingekuwa wapi ?. Maana kadri mtu anavyojitambua na kutambua uwezo mkubwa ndani yake huwa ni sawa na mtu aliyelala ndo anaamka na kuanza kuishi.

Kuwa sehemu ya mabadiliko chanya ya kusaidia wengine kutambua kuwa Dunia ni tele na haina uhaba

14b. Utoaji una bonasi. Wasaidie wengine kupata ulichopata wewe. Ikiwa umepata kuona njia waonyeshe wengine

Kwa njia ya utoaji ndivyo tunavyoweza kuwasaidia wengine wengi. Dunia hutegemezana siku zote.

Umejua kitu fulani basi wasaidie wengine wakijue pia. Umeona njia bora ya kufanya kitu wasaidie wengine nao wajue. Kufanya hivi utoaji wako unakuwa na bonasi kubwa mno.

Umesoma kitabu kizuri kama hiki basi naandika na wewe usome kisha usiwe mbinafsi ujue mwenyewe msaidie mwingine naye ajue. Dunia haijawahi kuwa bora kwa watu wenye umimi isipokuwa kwa wale ambao walijisahau wao kwa muda na kutoa muda wao, nguvu zao na mali kusaidia wengine.

Unapotoa kilicho ndani yako utaona jinsi ulivyokuwa tajiri lakini hukutambua mpaka pale ulipotoa. Ndani ya mtu hapana ukomo na kama utasema uandike huwezi kuandika ukamaliza. Kama hujui nini ulichobeba hebu angalia maisha yako ya utoaji yakoje

16. Wewe ni msanii wa maisha yako. Maisha ni sanaa ya mikono yako. Acha kulaumu watu shughulika na Wewe awe bora kwanza.

Ni rahisi sana kuona tuonewe huruma kuwa kushindwa kwetu, umaskini na magumu ni kwa sababu ya mtu au watu fulani. Huwa tunasahau kuwa maisha ni sanaa na sisi ni wasanii. Uchaguzi wa sanaa iwe nzuri au mbaya ni sisi wenyewe na sio wao au yule.

Wewe ni msanii wa kila ambalo linalotokea ujue umelichangia kwa kujua au kutokujua ( kukosa utambuzi). Hivyo wenye utambuzi hujua kuwa yote yalotokea na wao wamo kuchangia

Ikiwa maisha ni sanaa ( matokeo) na msanii ( chanzo ) ndio muumbaji basi sanaa ikiwa mbaya tatizo liko kwa msanii. Hawa wasanii ni wengi hata wewe ni msanii wa maisha yako.

Ikiwa hupendezwi na sanaa basi zungumza na msanii. Zungumza na wewe na jiboreshe ili maisha yako kifedha, ki mahusiano, kiafya yawe bora sababu msanii akiwa bora sanaa yake itakuwa bora.

17. Usigawanye hivi vitu 3; Mwili, roho na akili yako. Ukiviunganisha pamoja safari ya kufanikiwa ni nyepesi.

Kuona vitu kama vina uwili ni kiinimacho. Yaani kuona usiku na mchana ni vitu viwili tofauti ni kiinimacho maana hakuna usiku isipokuwa ulikuwepo mchana. Basi hili lipo hata ndani yetu unapoona ndani na nje.

Watu wengi hukosa matokeo ya kitu sababu wanajua mwili na roho au akili vinatofautina wasijue ni mamoja. Unapoweka umoja kazi ya kudhihirisha (manifestations) mambo au vitu huwa rahisi. Kwa kuwa kila kitu kinahusiana na kuungana pamoja. Hivyo unapokuwa umefikiri ndani basi mwili hujitahidi kujionyesha katika umbo la kile ulichofikiri.

Hivyo watu wenye utambuzi hujua kuwa kilicho ndani huja nje. Hivyo huwaza wanachokitaka kitokee nje kwa kubadili kilichopo ndani kwa ngazi ya akili, hisia na roho ili kitokee mwilini.

Umoja huu ni muhimu katika utatu wa mafanikio. Maana mafanikio huanzia ndani kuja nje. Na ndani huanzia katika mambo 2 kwa maana akili, roho na nje eneo la mwili

16b. Kuwa kiutambuzi ili uwe na sanaa itakavyovutia.

Msanii asiyeweza kujiboresha sanaa yake huwa mbaya. Mwimbaji asiyeweza kujiboresha uimbaji wake huwa mbovu. Mchongaji asiyejiboresha basi kinyago chake kitakuwa cha ovyo. Hili haliko katika hawa watu lipo katika maisha yetu pia. Ukikosa maboresho ya kiutambuzi basi unachokifanya kitakutana na ubovu, kisichovutia na wakati mwingine duni.

Kujitambua na kutambua hitaji la kukua ndani kuja nje ni muhimu linakupa hatua kubwa ya kuumba maisha unayotaka yawe.

Hivyo ili upate kutambua lazima ujue na kujiboresha kupitia maarifa. Ndipo hitaji la kujifunza, kutafakari, kutazama huja katika maisha ili uongezeke kiutambuzi. Bila utambuzi hata ukiwa umeishi miaka mingi bado kuna hatua fulani  za maisha utazikosa kujua sababu utambuzi wako utakuwa mdogo.

Jiboreshe na ukue ndani yako kiutambuzi kuwa Dunia ni tajiri na wewe ndani yako una utajiri.

18. Tumeunganishwa kuwa kitu kimoja. Kila kitu kinahusiana na kingine hivyo unachofanya kina mchango wa athari kwa mwingine.

Ukitibua maji labda kwa kurusha kipande cha mbao basi utaona mawimbi ya maji yakitawanyika pande nyingi. Hili linatokea katika maisha yetu pia kuwa kitu kimoja kinaweza kuathiri kingine sababu kinahusiana kama kitu kimoja.

Hivyo unapopuuza kitu kimoja basi umepuuza vingine pia. Kwa kuwa unapokuwa na utambuzi mtu ajua kuwa jambo dogo lina athari kubwa kwa mtu au huenda Dunia nzima. Uwepo kama “interneti” na kuwa kama kijiji ni dhahiri maisha yetu ni muunganiko wa mamoja.

Hivyo chochote unachokifanya kina nguvu ya kipande cha mbao kile kilichorushwa majini na maji yakasambaa.

Mawazo yako, hisia zako ni mamoja na mawazo ya watu wengine. Hivyo ukisambaza mawazo hasi unaathiri wengine pia kwa kuwa sote tuna umoja na kitu kimoja.

19. Utele- Vyote unavyotafuta unavyo ndani yako (amka na utambue)

Uwepo wa nafasi sisi binadamu kama viumbe wa Kiroho basi tuna nafasi kubwa ya kuwa karibu na chanzo. Maana roho ni chanzo cha vitu vyote vyenye umbo. Huu ni utajiri mkubwa ndani yetu ambao viumbe wengine hawajaweza kupata licha kupewa mwili.

Utele upo kwa wanaotambua kuwa Dunia haishiwii kuwa na vitu na watu. Watu wanazidi kuwepo, vitu vinazidi kutengenezwa kila siku. Huu ni uwazi kuwa Dunia ni tele na hakuna uhaba ambao wengi wamefundishwa hivyo.

Asili na Dunia ina utele wa biashara, utajiri kwa kila mtu anayetambua hilo ( aliye amka akajua kuwa Dunia ni tele ). Utajiri wa Dunia uko katika utambuzi wa mtu na utambuzi hauna ukomo.

Utele huu ni haki ya kila mtu na zawadi yetu ya kuitumia lakini ni mpaka kutambua kuwa upo ndipo tutaweza kuona na kupitia hali hizo.

Umaskini ni pamoja na kuwa na upofu wa ufahamu au utambuzi huu. Hivyo mtu huyu lazima aone kwanza au atambue upya ndipo umaskini utatoka kama kiinimacho

20. Maisha ni furaha na furaha ni maisha. Furaha ni hitaji kubwa Duniani kote

Vile sheria za asili zinavyoweza kusaidia wengi kupata utajiri basi sheria ya kupanda na kuvuna hufanya hivyo katika maisha ya furaha. Si hiyo tu hata sheria ya utoaji inafanya kazi kuwa kile unachotoa kitakurudia tena. Kwa maana ukitaka upate furaha basi wasaidie wengine kuwa na furaha.

Unapokuwa katika kusaidia wengine basi unajisaidia wewe. Waonyeshe wengine njia, fanya unachokipenda ndivyo furaha itakuwa na kujengeka kwako.

Kwa kuwa Furaha ni zao la ndani la mtu basi karibisha mawazo chanya, hisia chanya na jenga Picha nzuri na kisha dhibiti maneno yako. Kwa njia hii maisha yatakuwa furaha na furaha yatakuwa maisha

20b. Maisha ni sherehe. Kila yanayokutokea yaone kwa jicho la furaha. Ukitulia kila linakutokea lina sehemu ya wewe kuona kwa uzuri.

Maisha ni sherehe pale ambapo utatambua wewe ni daraja kwa wengine. Huja kuwa sherehe pale ambapo unatambua unaishi sababu kuna kazi ya kuchangia kuifanya Dunia iwe bora. Kufanya hivyo ni kufurahia maisha wakati wote.

Kuna wakati yatakutokea mambo ambayo utaona ni magumu sababu unaruhusu kuona hivyo. Hivyo ukibadili kuona na kufikiri basi kwa kila jambo kuna uwazi wa kuona na kupata furaha na kushukuru katika hayo.

Shukuru kadri uwezavyo maana ndivyo nishati inavyoweza kuwa kubwa na uponyaji ndani yako.

21. Fedha ni alama mojawapo ya utajiri. Utajiri una mifumo mingi kama umeamka kiakili na kiroho. Fedha ni mkondo wa mawasiliano ya nishati/nguvu

Fedha pekee kama fedha kama noti au sarafu haina thamani bila uwepo wa utambuzi wa watu. Je fedha yako sasa ukichukua bila kubadilisha pahala ukaenda nchini zingine je utaweza kutumia kupata unachotaka ?.

Je ukichukua fedha ambayo wengi wanajua hizi noti, sarafu kisha ukaziacha hapo miaka 10 je zitaongezeka ?. La hasha kama ni noti basi utaona zimeshaoza baada ya muda fulani. Sasa fedha ni nini ?

Fedha ni makubaliano ya kiutambuzi ya kuwasiliana baina ya watu kuhitaji nishati au vitu kutoka upande mwingine. Hivyo kama utaweza kushawishi mtu kupata unachohitaji bila fedha inawezekana pale yanapokuwepo makubalinao baina ya watu wawili.

Hujawahi ona kuna sehemu unaweza kupata vitu bila fedha ?

Hujawahi ona kuna sehemu watu wanatumia tu nafasi ya mabadilishano ya wao watambulike tu badala ya fedha kama alama ?.

Hivyo ukielewa hivi utaona fedha ni kiinimacho kingine cha watu kutojua fedha ni nini.

Fedha si karatasi wala noti ni thamani ya nishati inayosambaa toka eneo moja kwenda eneo lingine. Wale wenye udhibiti wa nguvu hii huwa na nguvu kubwa ya kupata mabadilishano ya vitu wanavyovitaka.

Ukikuza utambuzi wako wa kitajiri utaona fedha ni sehemu ndogo ya utajiri au kutumika kama njia ya mabadilishano. Kuwa zaidi ya makubaliano ya kawaida ya alama kama noti au sarafu. Ni makubaliano ya fikra baina ya watu ili kuweza kuwasiliana

Naamini mtizamo huu ukitulia utaona hatua kubwa ya maisha yako.

Nakutakia mafanikio makubwa katika maisha yako. Hiki kitabu ni moja ya vitabu bora sana vya kuvisoma.

Malenga wa Ubena

+255 676 559 211

raymondpoet@yahoo.com