Napenda kukusihi sana kwamba ndoa au mahusiano yanahitaji kazi sana kama vile kazi nyingine kwa mfano, kazi unayoiweka kutafuta fedha.

Na mara nyingi mahusiano yakiwa vizuri na mambo mengine yanakuwa mazuri. Ukishavurugwa kwenye mahusiano ya ndoa hata vitu vingine vinavurugika kabisa. Ukajitahidi kuweka sawa mambo yako ya kimahusiano maana yatakumaliza nguvu kubwa na kushindwa kufanya vitu vingine.

Changamoto ya wanandoa wengi ni kila mwandoa kushindwa kutambua thamani ya mwenzake.

Swali muhimu la kujiuliza ni hili;
Je, Ninapenda mwenzi wangu wa ndoa anioneje?

Mahusiano yanakufa au kuchakaa kwa sababu ya kimazoea. Watu walioko kwenye ndoa wanajua kwamba kama akishaoa au kuolewa basi amemaliza kazi kumbe ndiyo kazi inaanza.

Ukiona ndoa yako ina shida basi umeshindwa kuendeleza kazi fulani ya kimahusiano. Ukiwa ni mtu wa kujiuliza na kujiwekea malengo je ninapenda mwenzi wangu wa ndoa anioneje utakua na dira ya mahusiano.

Ukishindwa kuwajibika katika ndoa yako, jibu ni rahisi sana watu wengine watakusaidia kuwajibika kwa adhabu ya riba kubwa.

Kuna mambo ambayo mke au mume wako anayatamani kutoka kwako. Ni muda sasa wa kila mmoja wa kujiuliza maswali ya kujitathimini hivi je, ninapenda mwenzi wangu wa ndo anioneje mwaka huu mpya 2021.

Kila eneo la maisha yako linahitaji kukua. Maarifa yapo yatumie kuboresha huduma yako. Mahusiano yakiwa vizuri kila kitu kinaenda vizuri.

Pambana mahusiano yako yawe na afya ili uweze kufikia malengo yako. Huwezi kufikia malengo makubwa kama mahusiano yako hayana afya. Vitu vinavyoendeshwa na hisia huwa vina kazi ndiyo maana mahusiano yanaumiza watu wengi kwa sababu ya kushindwa kufikiri sana katika kufanya maamuzi na kukubali kuongozwa na hisia.

Mke au mume wako ni mteja wako. Sasa ili uweze kumteka mteja wako jua kile anachotaka mteja wako yaani mke au mume wako na mpatie kile anachotaka.

Tumetofautiana hivyo kanuni ya almasi itumike. Ambayo kanuni ya almasi inasema mtendee mtu mwingine kama vile anavyotaka yeye. Kwani kanuni ya dhahabu inasema mtendee mwingine kama vile unavyotaka wewe kutendewa. Unaweza wewe kupenda kusoma vitabu, lakini mke wako asipende kusoma vitabu.

Na ukitaka kushika umakini wa watu au kuwashawishi ni kukubaliana na kile ambacho wao wanataka. Usiwalazimishe kile unachotaka wewe bali kile wanachotaka wao.

Hatua ya kuchukua leo; Kaa chini na jiulize swali hili je, ninapenda mwenzi wangu wa ndoa anioneje mwaka huu?

Inawezekana mwenza wako ana majibu hivyo muulize je, mke/ mume wangu unapenda unioneje katika mahusiano yetu ya ndoa? Atakuambia kwa sababu kuna kitu yeye anakitaka kukiona kutoka kwako.

Kwa hiyo, maswali ya tathimini yanasaidia kuwarudisha watu kwenye mstari. Yanasaidia kujua kama mahusiano yenu yanaenda mbele au yanarudi nyuma.

Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.

Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog ,vitabu nakwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana