Nakumbuka wakati tuko shule ya msingi, kama mwalimu alitoa kazi na hujaifanya, ulikuwa unatafuta kisingizio ili kukwepa adhabu. Kisingizio rahisi ilikuwa ni kuangalia mwanafunzi ambaye hajaja shule siku hiyo na kusema alichukua daftari yako.
Watu wasiokuwepo na ambao hawawezi kujitetea, huwa wanasingiziwa vitu vingi mno. Vingi ya hivyo huwa siyo vya kweli, ila kwa kuwa hawapo basi kila mzigo wanabebeshwa wao.
Nimekuwa naona hilo pia kwenye misiba, baadhi ya mambo yanafanyika kwa kisingizio kwamba marehemu kabla hajafa alisema hivi au vile.
Vingi katika hivyo marehemu wanakuwa hawajasema kabisa na vichache ambavyo walisema, hawakumaanisha ni amri, bali yalikuwa mapendekezo, hivyo wale wanaobaki wanapaswa kutumia busara zao katika kufanya maamuzi sahihi.
Kwani huenda marehemu angekuwepo, angebadili maamuzi yake ya awali.
Kuna mawili ya kuondoka nayo hapa;
Moja kuwa makini na mambo ambayo yanasemwa kuhusu wasiokuwepo na wasioweza kujitetea, hasa wanapotumika kama sababu ya vitu fulani. Usikubali tu kirahisi, jua ni rahisi watu kusingizia wale wasiokuwepo.
Mbili inapokuja kwenye swala la marehemu, alichosema hakipaswi kuwa sheria isiyobadilika, badala yake busara lazima itumike kuangalia kipi sahihi kufanya. Kwa kuwa marehemu hayupo tena na hawezi kufanya maamuzi, mnaobaki ndiyo mnafanya maamuzi kwa niaba yake.
Kila mmoja wetu kuna maamuzi mengi anafanya na kubadili kwenye maisha yake pale mambo yanapokuwa tofauti na alivyotarajia, sasa kwa nini maamuzi ya marehemu yasibadilishwe pale mambo yanapokuwa tofauti?
Watu wengi wamekuwa wanajificha nyuma ya kauli marehemu alisema…. Usikubaliane na kauli hiyo kirahisi, chunguza usahihi wake na hata kama itakuwa sahihi, busara lazima itumie kwa muktadha uliopo kwa wakati huo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Sana kocha.
Inachekesha na ina funzo kubwa pia
LikeLike
Karibu.
LikeLike