Wakati bado nafanya kazi ya kufundisha shule ya sekondari, siku moja tukiwa ofisini na mwalimu mwingine aliyekuwa anasahihisha kazi za wanafunzi alilalamika kuhusu wanafunzi kukosa swali moja kwa majibu yanayofanana.

Nikamwambia kwa utani, kama wanafunzi wote wamekosa swali hilo na majibu yao yanafanana, huenda wewe ndiye uliyekosea kwenye jibu lako. Kweli, akakokotoa upya na kukuta kuna kitu ameruka, hivyo jibu la wanafunzi lilikuwa sawa na lake lenye makosa.

Hapa kuna funzo kubwa tunaloweza kutumia kwenye maisha yetu na likatusaidia sana. Mara kwa mara tunapaswa kujiuliza swali hili; vipi kama mimi ndiye ninayekosea?

Mara nyingi watu huwa hawakubali makosa yao, huwa ni rahisi kuwalaumu wengine kwa kila kitu, lakini hawaangalii mchango wao kwenye kile kilichotokea.

Lakini pia tunajua kila mmoja wetu ana madhaifu yake na siyo rahisi kuyaona na kuyakubali, hivyo inahitaji jitihada za ziada kwa mtu kuyaona madhaifu yake na kuyazuia yasiwe kikwazo kwake.

Tumekuwa tunajifunza pia umuhimu wa kutokufuata kundi, kukimbia mbio zako mwenyewe na kwenda upande wa wachache.

Lakini ni muhimu kuhakikisha uko upande sahihi, siyo tu kupingana na wengi.

Nimewahi kusema, kwa sababu kila mtu anatembelea mguu, basi wewe utembelee mikono.

Kuna wakati kundi linaweza kuwa sahihi, hivyo lengo lako wewe siyo kupingana tu na kundi, bali kuwa upande sahihi.

Mara kwa mara jiulize isije kuwa ni wewe unayekosea, hujiulizi hivyo kujihukumu, bali swali hilo litakusukuma uujue ukweli uko wapi na kuusimamia.

Swali hilo pia litakuondoa kwenye mazoea unayoweza kuwa umeyajenga, yanayokuzuia usijifunze na kuona vitu vipya.

Mtu mmoja amewahi kusema hakuna mtu mwenye akili za kuweza kupatia mara zote au kukosea mara zote. Kila mtu kuna mambo anapatia na kukosea, hivyo usijidanganye, jikague mara kwa mara na unapojikamata umekosea, fanya masahihisho na songa mbele.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha