Muda na nguvu zako ni rasilimali mbili muhimu zenye ukomo kwenye maisha yako.

Kila siku una masaa 24 pekee na nguvu zako ni kwa kiwango fulani.

Kuna mambo mengi kwenye siku yako yanayowinda muda na nguvu zako, usipokuwa makini katika kulinda rasilimali hizo, zitapotea bila ya kufanya chochote.

Moja ya vitu vinavyoshawishi sana kufanya ni kuhangaika na wengine, kuwakosoa wale wanaofanya makosa mbalimbali.

Wanaokosea ni wengi na ni rahisi kuona ni wajibu wako kuwakosoa na kuwasahihisha, lakini kama utatumia nguvu na muda wako mwingi kwenye hilo, hutabaki nazo za kutosha kufanya yale muhimu kwako.

Kumbuka wewe siyo kiranja wa dunia wa kuhakikisha kila mtu yuko sawa na hata ufanye nini, watu wataendelea kukosea kwenye mengi wanayofanya.

Njia bora ya kutumia nguvu na muda wako ni kutekeleza wajibu wako, kwa kufanya yaliyo muhimu na yenye tija, kuzalisha thamani kubwa.

Watu wataendelea kukosea, muda na nguvu zako havitarudi baada ya kuwa umehangaika na mambo ya wengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha