Nilishakuambia uchaguzi wa kwanza muhimu kabisa kwenye maisha yako ni kujichagua wewe mwenyewe. Kujipigia kura wewe kama kiongozi mkuu wa maisha yako, mtu pekee wa kukutoa hapo ulipo sasa na kukufikisha kule unakotaka kufika.

Naamini hilo ulilielewa vizuri, ilishajichagua na sasa unaweka juhudi kufika unakotaka kufika.

Kuna uchaguzi wa pili kwa umuhimu kwenye maisha yako ambao umekuwa huupi uzito wa kutosha.

Uchaguzi huo ni kuchagua wale wanaokuzunguka, usipofanya uchaguzi huu kwa makini, hutaweza kupiga hatua.

Tumejifunza mara nyingi kuhusu ushawishi wa wale tunaokuwa nao karibu, tunajua jinsi maisha yetu yalivyo wastani wa watu watano tunaotumia nao muda wetu mwingi.

Hivyo kama unataka kupiga hatua kubwa, lazima uchague kwa umakini watu gani unajihisisha nao, uhakikishe ni watu ambao watapandisha wastani wa mafanikio yako.

Ni lazima ujiwekee viwango vya juu kwako binafsi na kwa wale utakaojihusisha na kushirikiana nao. Usipokuwa na viwango, kila mtu atakuja kwako na ataathiri mafanikio unayoweza kufikia.

Kuna watu lazima uwafute kwenye maisha yako kama unataka kupiga hatua kubwa, kwa sababu watu hao wanaweka juhudi kuhakikisha hufanikiwi kuliko wao.

Kama umewasha gari na kuweka gia, kisha unakanyaga mafuta lakini gari haiendi, huhitaji miujiza kujua kwamba kuna kitu kinazuia, huenda umekanyaga breki na mafuta kwa wakati mmoja.

Ndivyo ilivyo kwenye maisha yako, kama unaweka juhudi kubwa sana lakini hupigi hatua, lazima kuna kitu kinazuia na kama siyo wewe mwenyewe, basi kuna wanaokuzunguka ambao wanaweka kikwazo usipige hatua.

Ni wakati wa kukagua wale wote wanaokuzunguka, wale unaotumia nao muda wako mwingi na kupima mchango wao kwenye mafanikio au kushindwa kwako. Safisha wale wote ambao unawaona ni kikwazo na weka viwango vipya na vya juu vya namna unataka wale utakaoshirikiana nao wawe.

Hili ni eneo unalohitaji kuwa na msimamo mzuri maana watu watatafuta kila njia ya kukuteteresha, ila wewe usikubali kutetereka. Watakufanya ujione unakosea kwa kutokuwa nao, lakini lazima ujue ili kupata kilicho bora, lazima upoteze kilicho kizuri.

Kuna watu wanaweza kuwa wazuri, lakini hawatakuwezesha kufikia ubora, hapo unahitaji wale walio bora ndiyo ushirikiane nao kwa karibu.

Hili la kuwasafisha watu kwenye maisha yako haimaanishi ugombane na watu, kuwadharau au kuwachukia. Endelea kuwapenda watu na kuwaheshimu, ila inapokuja kwenye kushirikiana nao, iwe ni kazi, biashara au mahusiano mengine ya karibu, kuwa na viwango ambavyo mtu anapaswa kuwa amefikia ndiyo apate nafasi hiyo.

Unaweza kuona huwezi kupata watu wenye viwango unavyojiwekea, lakini kumbuka dunia ina watu zaidi ya bilioni 7, huwezi kukosa watu watano wa viwango vya juu kabisa ambao watakusukuma kufanikiwa sana.

Fanya uchaguzi huu wa pili muhimu, chagua watu sahihi wa kujihusisha nao na utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha