Huwa situmii kabisa mitandao ya kijamii, hivyo ninapokutana na watu wakilalamikia yale wengine wanafanya kwenye mitandao hiyo huwa nawashangaa.
Unakuta mtu analalamika kwamba hapendezwi na yale wengine wanafanya kwenye mitandao hiyo. Mimi huwa nina swali moja kwao, mtu huyo unayemlalamikia amekuja nyumbani kwako na kufanya kitu hicho? Au amekulazimisha umfuatilie mtandaoni?
Mtu na maisha yake, ana simu yake, anatumia fedha zake kupata mtandao wa kuingia mitandaoni, anaweka alichochagua yeye, halafu wewe unakasirishwa nacho?
Hivi hapo unafikiri mwenye tatizo ni nani? Anayechagua kutumia mtandao kwa namna anavyotaka au anayekasirishwa na namna mwingine amechagua kutumia mtandao?
Huu ni mfano mmoja, lakini ipo mingi kwenye maisha, jinsi ambavyo huwa tunajisumbua kwa yale wengine wamechagua kufanya.
Huwa tunajipa ukiranja wa dunia, tukitaka kila mtu afanye kama tunavyotaka sisi, kitu ambacho hakiwezi kuja kutokea. Kwani hata raisi wa nchi, hakubaliki na watu wote.
Jifunze kuacha kujisumbua mwenyewe, jifunze kuwaacha watu wachague maisha wanayotaka kuishi na jifunze kuishi kwa misingi yako na kuisimamia bila kujali wengine wanaishije.
Kwa njia hiyo utapata utulivu mkubwa mno, hutakasirishwa na mambo madogo madogo na pia utapunguza chuki.
Kuna watu wengi wenye magonjwa ya akili, wewe unaweza kuwa unakasirishwa nao, kumbe kinachowasumbua ni ugonjwa walionao. Ukilifikiria hilo mara kwa mara, utaepuka kusumbuka na mengi.
Lakini pia epuka kuwa mtu wa kuhukumu kila kitu, hili ni gumu kwa sababu sisi binadamu huwa hatuoni kitu, bali tunakiona kwa namna tunavyokihukumu. Utapishana na mtu, lakini hutamuona kama mtu, bali utamhukumu kwa mwili wake (mwembamba au mnene) kwa mavazi yake (amependeza au hajapendeza) na mengine mengi.
Hili la kuhukumu watu kwa tunavyowaona ndiyo linafanya tuzidi kujisumbua na yasiyo muhimu. Ukiacha kuwaona watu kwa hukumu ulizonazo na kuanza kuwaona kama walivyo, utaondokana na changamoto nyingi.
Hata hali za kutoelewana na wengine, nyingi huanza na wewe mwenyewe, kwa namna unavyowachukulia wengine au vile unavyotaka wawe. Ukitambua hilo na kujidhibiti, utazipunguza changamoto nyingi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha kwa makala hii nzuri, hakika hili limenisaidia kupunguza baadhi ya Mambo mengi naendelea kufumua baadhi ya mfumo wa vitu ktk maisha yangu.
LikeLike
Vizuri.
LikeLike