Ni asili yetu binadamu kutaka kupendwa na kila mtu, hivyo huwa tunajitahidi kufanya kile ambacho kitawafurahisha walio wengi.

Lakini kila tunapojaribu kufanya hivyo, tunaishia kufanya kisichokuwa na msimamo na kisichomfurahisha yeyote.

Kama tunataka kupata wafuasi au watu wanaokubaliana na sisi kwenye maisha, lazima tuchague msimamo ulio wazi kwa wote.

Kwa kuchagua msimamo wetu kuna ambao tutawaudhi na hawatataka kutufuatilia kabisa. Lakini kuna ambao tutawaridhisha na watakuwa tayari kwenda na sisi.

Katika kuchagua msimamo tunapaswa kuacha kutangatanga na kila kinachopita mbele yetu ili tu kuwaridhisha walio wengi.

Katika kuchagua msimamo hatuanzi kwa kuwaangalia wengine, bali kwa kujiangalia sisi wenyewe, kuwa wa kweli kwetu wenyewe na kujua wapo wanaoendana na sisi na watasimama na sisi kwenye msimamo tunaochagua.

Chochote unachofanya ambapo unahitaji wafuasi, angalia ubora wa wafuasi hao na siyo wingi wao. Wafuasi bora wanakusikiliza na kufanya kile unachoelekeza, kwa sababu wanakisimamia kweli. Wafuasi wanaokuja kwa wingi wanakuwa hawajajitoa kweli na hivyo siyo watu wa kuchukua hatua.

Mtu mmoja mwenye wafuasi wengi mtandaoni aliwahi kusema wafuasi wa mtandao ni wazuri kabla hujataka kuwatumia kufanya kitu. Hapo alikuwa anaeleza jinsi unavyoweza kufurahia kwamba una wafuasi milioni kadhaa mtandaoni. Lakini ukisema unataka wafuasi hao wafanye kitu fulani, hapo ndiyo  utajua siyo wafuasi kweli.

Chagua unaposimama, ili yeyote anayechagua kusimama na wewe, awe ni aliyejitoa kweli, ambaye unaweza kushirikiana naye na mkafanya kitu. Badala ya kukazana kumfurahisha kila mtu ili uwe na wafuasi wengi, ambao huwezi kuwatumia kwa chochote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha