Changamoto ndiyo kiashiria sahihi cha mafanikio kwenye maisha.
Palipo na changamoto ndipo pia palipo na fursa kubwa ya kufanikiwa.
Hiyo ni kwa sababu changamoto huwa zinawaondoa wale ambao hawajajitoa kweli na kuwaacha wale waliojitoa na walio tayari kupambana.
Ndiyo maana huwa nasisitiza tunapokutana na changamoto tusizikimbie, badala yake tuzikabili na kuzishinda, kwani ushindi huo unatupeleka kwenye mafanikio makubwa.
Changamoto hizo siyo rahisi na ndiyo maana nimekuwa nakuandalia makala hizo za ushauri, ambapo unaeleza changamoto unayokabiliana nayo na kisha nakushauri namna bora ya kupambana nayo.
Kwenye makala hii, mwenzetu ameomba ushauri kwenye mambo matatu, biashara nzuri kwake kufanya, jinsi gani aweke akiba na aweke wapi ambapo panaongeza thamani.

Tunakwenda kujifunza haya matatu kwa kina na hatua za kuchukua ili kupiga hatua. Huenda na wewe unakabiliana na haya, hivyo yapo mengi ya kujifunza na kufanyia kazi.
Mimi nasoma chuo mwaka wa kwanza na ndoto yangu kubwa Ni kufanya biashara, biashara gani nifanye ambayo haitaathiri muda wangu wa masomo, naomba ushauri. Nifanye nini ili mwaka 2021 uwe tofauti katika kutenga akiba? Je niwekeze wapi fedha ninazojilipa ? Na hiyo fedha nataka iwe inaongezeka thamani. – Bakari M. S.
Biashara sahihi kufanya.
Kama alivyoeleza msomaji mwenzetu, anasoma chuo na anapenda sana kufanya biashara, ila hajui biashara ipi nzuri kwake kufanya ambayo haitaathiri muda wake.
Kwanza nimpongeze sana kwa kuchagua kuanza biashara akiwa bado yuko chuoni, anakuwa na nafasi nzuri ya kujifunza biashara mapema, ili anapomaliza chuo, wakati wenzake wanasubiria ajira ambazo haziji, yeye anakwenda kukuza biashara yake zaidi.
Kila mtu anajua jinsi ambavyo hakuna ajira, lakini hakuna anayeonekana kuchukua hatua zozote. Hivyo mwanafunzi yeyote wa chuo anayechagua kufanya biashara akiwa chuoni, anapata elimu mbili muhimu, ya kile anachosomea chuoni na ya kuendesha biashara.
Kuna biashara nyingi ambazo mwanafunzi wa chuo anaweza kufanya, lakini inategemea zaidi mapenzi yake binafsi, kiasi cha muda alionao na mipango yake ya baadaye.
Hivyo sitakutajia biashara moja kwa moja, ila nataka uelewe msingi mkuu wa biashara ambao unapaswa kuuzingatia katika kuchagua ufanye nini.
Msingi mkuu wa biashara ni kuwa na thamani, ambayo wengine wanaihitaji na wanamudu kuipata kisha uwafikie wengi kiasi cha kupata faida inayozidi gharama unazoingia kufanya biashara hiyo.
Nimekupa msingi huo ili uwaze kwa upana na uache kufuata mkumbo, maana unakuta wanafunzi wengi wa chuo wanaposema wanafanya biashara wanauza nguo, viatu na saa na wanaweka tu mtandaoni na kuona wameshamaliza, wanasubiri wateja wawatafute kitu ambacho hua hakitokei au kikitokea kwa nadra.
Kama unachagua kufanya biashara ukiwa chuoni (au ukiwa kwenye ajira) lazima ujitoe kweli, usifanye kwa kujaribu au kufanya kwa kuiga. Lazima ukae chini na kufikiri kwa kina na kuchagua biashara ambayo utaifanya kwa muda mrefu, hata kama utaanzia chini na kuikuza taratibu.
Hivyo nikushauri sana kabla hujaamua ni biashara gani ufanye, soma vitabu hivi viwili;
Kitabu cha kwanza ni ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA, hiki kitakusaidia kuja na wazo la biashara ambalo ni la kipekee kwako badala ya kuiga yale wanayofanya wengine. Lakini pia kitakufundisha kuhusu mfumo mzima wa uendeshaji biashara ili uache kuwa kama wale wanaopost mtandaoni tu halafu wakikosa wateja wanasema biashara ni ngumu.
Kitabu cha pili ni BIASHARA NDANI YA AJIRA, hiki kinakusaidia kuweza kufanya biashara huku pia unafanya kitu kingine, kama ajira au masomo. Kitabu hiki kitakufundisha dhana ya KUWA NA SIKU MBILI NDANI YA SIKU MOJA, siku ya kwanza ni ya kimasomo chuoni na siku ya pili ni ya biashara. Kitabu pia kina mifano ya biashara za kuanzia kutokutumia mtaji kabisa, mtaji kidogo na mtaji mkubwa.
Jinsi ya kuweka akiba.
Kuweka akiba ndiyo hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye utajiri na uhuru wa kifedha. Kama kila kipato unachoingiza unakitumia, jua utakufa masikini.
Lakini kuweka akiba kumekuwa na changamoto kubwa mbili, ya kwanza ni kukosa cha kuweka akiba kwa sababu matumizi yanakuwa makubwa na ya pili ni kutumia akiba pale unapokuwa umeiweka.
Kutatua changamoto hizi mbili kuna hatua mbili muhimu kuchukua;
Hatua ya kwanza ni kuweka akiba kabla ya matumizi. Unapopokea fedha zako, iwe ni mshahara, faida au posho, weka kwanza akiba kabla hujafanya matumizi. Yaani weka pembeni akiba yako kabla hujatumia na siyo kusema utumie ikibaki uweke akiba. Ukishaanza na matumizi pesa huwa hazibaki, kwa sababu matumizi huwa hayaishi mpaka pesa ziishe. Chagua kiwango cha akiba unayotaka kuweka na anza kuweka hiyo kabla ya matumizi.
Hatua ya pili ni kuweka akiba hiyo sehemu ambayo siyo rahisi kuitoa. Ukiificha kama fedha taslimu ukipata shida kidogo tu unaitumia. Ukiiweka kwenye akaunti yako ya kawaida ya benki ukipata shida unaenda kutoa. Hivyo unapaswa kuiweka mbali ambapo hutaifikia. Kwenye kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA kuna dhana nimeiita GEREZA LA KIFEDHA, unapaswa kufungia fedha yako mahali ambapo hutaifikia kirahisi.
Mahali sahihi pa kuwekeza.
Uwekezaji ni hatua ya pili muhimu kuelekea kwenye utajiri na uhuru wa kifedha baada ya kuweka akiba. Kile unachoweka akiba unapaswa kukiwekeza ili kilete faida zaidi.
Kuna vigezo vingi vya kuangalia kwenye uwekezaji, lakini viwili vikubwa ni faida na thamani.
Unapaswa kuwekeza mahali ambapo uwekezaji wako unazalisha faida zaidi. Hiyo ndiyo njia ambayo fedha yako inazaliana na kuleta faida kubwa bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja.
Pia unapaswa kuwekeza mahali ambapo thamani ya uwekezaji wako inakua kadiri muda unavyokwenda. Kwa kuwa mfumuko wa bei huwa unaongezeka na thamani ya fedha kupungua, thamani ya uwekezaji wako inapaswa kuwa inapanda.
Kuna maeneo mengi ya kuwekeza, lakini mahali pa kuanzia kwa wengi huwa nashauri UTT AMIS, kwenye mfumo wa UMOJA. Huu ni mfumo rahisi wa uwekezaji ambao unaweza kuanza kidogo na kufanya uwekezaji endelevu hata kama huna elimu yoyote ya uwekezaji. Uwekezaji huu unaongezeka thamani kadiri muda unavyokwenda na unaweza kujionea mwenyewe.
Kujifunza zaidi kuhusu kuweka akiba na uwekezaji, hasa dhana ya GEREZA LA AKIBA na maeneo mengine ya kuwekeza, soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, hicho kitakupa mwongozo wa kila kitu kuhusu fedha.
Kupata vitabu vilivyotajwa hapa, wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa kitabu popote pale ulipo.
Shika hatamu ya maisha yako, anza kufanyia kazi ndoto zako sasa na siyo kusubiri mpaka uhitimu chuo au ustaafu kazi. Maarifa ya kukusaidia kufanya vyote kwa pamoja yapo, ni wajibu wako kuyapata na kisha kuchukua hatua sahihi katika kufikia ndoto zako.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania
Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp