Huwezi kufanikiwa kama huyaishi maisha yako, kama huwi wewe, ambaye hakuna anayeweza kukushinda kwa kuwa wewe.

Lakini kuyaishi maisha yako ni rahisi kusema kuliko kutenda.

Na hiyo ni kwa sababu jamii imeshakuweka kwenye boksi fulani, inatulia unapokuwa umekaa kwenye boksi hilo.

Lakini siku utakayoamua kutoka kwenye boksi hilo, dunia nzima itakuwa dhidi yako. Utashangaa mpaka watu ambao hukujua kama wanayafuatilia maisha yako watakuwa na cha kusema kuhusu maisha uliyochagua kuishi.

Hutaeleweka, kwa sababu hakuna anayejua nini kipo ndani yako.

Hilo litapelekea usemwe vibaya na kuambishwa utashindwa.

Utakapoendelea kung’ang’ana vikwazo vya wazi na visivyo vya wazi vitawekwa kwenye njia yako.

Na hata utakapovivuka, wapo watakaojaribu kuiga namna unavyoyaishi maisha yako, huku wengine wakishambulia mafanikio yako.

Tambua siku unayochagua kuyaishi maisha yako ndiyo siku umetangaza vita na dunia nzima, vita ambayo haitakuwa na ukomo.

Hivyo unapaswa kujitoa kweli kwamba hutarudi nyuma na utapambana kubaki kwenye kuyaishi maisha yako.

Hili siyo rahisi kwa wengi, kwa sababu wanataka kuwaridhisha wengine, wanataka waonekane wana roho nzuri na wanaona ni bora ukakosea ukiwa kwenye kundi kuliko kukosea mwenyewe.

Kuchagua kuyaishi maisha yako umechagua kuanguka mwenyewe, kuzomewa kwa kuanguka huko, lakini kusimama na kuendelea.

Siyo wengi wanaweza hivyo, ndiyo maana wachache sana ndiyo waliofanikiwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha