Kwenye kitabu cha Things Fall Apart kilichoandikwa na Chinua Achebe, mhusika mkuu ambaye ni Okonkwo ni shujaa wa kijiji cha Umuofia.

Alianzia chini kabisa bila ya urithi kutoka kwa baba yake, lakini akapambana na kuweza kujijengea mafanikio makubwa katika umri mdogo.

Lakini pia amejijengea sifa kwenye kijiji chake kama mpiganaji mieleka bora na shujaa wa kivita ambaye amerudi na vichwa vitano vya watu kwenye vita mbalimbali walizoshiriki.

Licha ya mafanikio hayo makubwa ambayo Okonkwo amefikia, ndani yake kuna hofu kubwa. Kwa kuwa ameanzia chini kabisa, anahofia kama akianguka atarudi tena chini na kuwa si mtu wa heshima kwenye jamii yake.

Hivyo hofu hiyo ya kuanguka na kupoteza kila kitu, imekuwa inamsukuma afanye vitu kuonesha ushujaa wake hata kwa wakati ambapo haihitajiki kufanya hivyo.

Kwenye kisa kimoja, Kijiji cha Umuofia kilikuwa na mgogoro na kijiji kingine baada ya mwanamke wa Umuofia kuuawa kwenye kijiji hicho. Umuofia ilikipa kijiji hicho machaguo mawili, kulipa fidia ya mwanamke bikira na kijana wa kiume au kuingia vitani.

Kwa kuwa Umuofia iliogopeka kwa ushujaa wa kivita, kijiji hicho kilikubali kulipa fidia. Mwanamke bikira aliozwa kwa mume aliyepoteza mke, na mtoto wa kiume aliachwa aishi nyumbani kwa Okonkwo, mtoto huyo aliitwa Ikemefuna.

Okonkwo alimpenda sana Ikemefuna na kumchukulia kama mtoto wake, Ikemefuna naye alimuita Okonkwo baba. Maisha yalikwenda na baadaye kijiji kikaamua Ikemefuna atolewe kafara ya kuuawa.

Mzee wa kijiji anapeleka taarifa kwa Okonkwo kuhusu maamuzi hayo, lakini pia anamtahadharisha, anamwambia; “Huyo kijana anakuita baba, usijihusishe kwenye kafara yake.”

Okonkwo hasikii tahadhari hiyo, anaambatana na wanaume wanaoenda kutoa kafara kwa sababu hataki kuchukuliwa ni dhaifu. Lakini alikuwa amepanga asihusike yeye kumtoa kafara.

Aliyapangwa kumkata Ikemefuna anashindwa kufanya hivyo mara moja, Ikemefuna anakimbilia kwa Okonkwo na kumwambia; “baba nisaidie, wanataka kuniua.”

Okonkwo anachukua panga lake na kumkata shingo Ikemefuna ambaye anafariki hapo hapo. Okonkwo aliona asipofanya hivyo angechukuliwa ni dhaifu, siyo mwanaume shujaa.

Lakini tangu siku hiyo, hakuwahi kupata amani ya moyo wake, hakuweza kulala usiku, tukio hilo lilimjia kila mara na hata mahusiano yake na mtoto wake wa kwanza aitwaye Nwoye yalikuwa mabaya zaidi.

Huwa tunaonesha udhaifu wetu pale tunapokazana kutumia nguvu kubwa kuonesha kwamba sisi ni mashujaa au tuko imara sana.

Na binadamu wote wanajua, ukiona mtu anatumia nguvu kubwa kwenye jambo, jua kuna kitu anachokificha kwenye jambo hilo.

Usiishi maisha yako kwa kutumia nguvu kuonesha uimara au ushujaa ulionao, kama wewe ni imara au shujaa kweli, watu wataona hilo kupitia maisha yako ya kila siku, jinsi unavyokabiliana na mambo mbalimbali unayokutana nayo kwenye maisha.

Wale wanaotaka kukutega kwa namna ya kujinufaisha binafsi, huwa wanaangalia udhaifu wako uko wapi na kuutumia huo. Na wakishajua sehemu unayoweka nguvu kubwa kulinda, hapo hapo ndipo wanapatumia kupata wanachotaka.

Mfano kama mtu anataka upate hasira na ufanye maamuzi ya hovyo ambayo yatamnufaisha yeye, anaangalia ni eneo gani unalificha zaidi kwenye maisha yako na kisha kuliweka wazi.

Watu wanajua kuitafuta sehemu inayokuuma na kuiumia hiyo ili waweze kupata kile wanachotaka kutoka kwako.

Kuondokana na hili, jitambue wewe mwenyewe, jua uimara wako uko wapi na madhaifu yako ni yapo na kisha jikubali vile ulivyo. Usitake kufanya maigizo yoyote yale ili kuwafanya watu wakuchukulie kwa namna fulani ambayo haupo. Wala usitumie nguvu kubwa sana kuwathibitishia watu vile ulivyo, wewe ishi maisha yako na vile ulivyo itaonekana na walio sahihi watakuheshimu kwa namna ulivyo.

Njia nyingine tunayoitumia kuonesha madhaifu yetu ni kupitia kuongea sana.

Kwenye kitabu hicho hicho cha Things Fall Apart, kuna nahau nyingi za Kiafrika ambazo zinabeba ujumbe mkubwa.

Moja ya nahau hizo inasema ogopa sana mtu aliyekaa kimya na huna cha kuhofia kwa anayepiga kelele.

Wazee wanaeleza hadithi kwamba mama mwewe alituma watoto wake wakatafute kitoweo, wakarudi na vifaranga. Mama mwewe akawauliza wanae mama wa hao vifaranga alisema nini wakati wanawachukua, wakajibu hakusema chochote. Mama mwewe akawaambia warudisheni hao vifaranga kwa mama yao. Wakarudi na vifaranga wengine, mama akawauliza mama yao na vifaranga alisemaje, wakajibu amewarushia maneno makali na kuwalaani, mama mwewe akawaambia hicho ndiyo kitoweo.

Ukweli ni kwamba watu wanaoongea sana huwa siyo watu wa kuchukua hatua, wakishaongea ndiyo hasira zao zimeishia hapo na hawahangaiki tena na jambo ambalo wameshaliongelea.

Ila wale wanaokaa kimya, ni watu hatari, kwa sababu kwanza hujui ni hasira kiasi gani wanayo na hujui wanapanga nini kwenye akili zao. Wale wanaoongea sana wanaweka wazi kila kitu, hivyo unajua kabisa mpango wao ni upi na unaweza kujitahadhari. Ila wanaokaa kimya, hujui chochote na hivyo huwezi kujiandaa kitu kinachokuweka kwenye hatari zaidi.

Kuongea sana ni kitu kinachoonesha udhaifu wako ulipo na watu wanaweza kukukadiria na kujipanga jinsi ya kukabiliana na wewe. Pia kuongea sana kunaleta mazoea ambayo yanaleta dharau, watu hawawapi uzito wale wanaoongea sana.

Ila unapokuwa mkimya, watu wanakuwa hawawezi kukuelewa wala kukukadiria, wanakuheshimu kwa kuwa hawajui mengi kuhusu wewe.

Kuepuka kuweka udhaifu wako hadharani na wengine wakautumia kujinufaisha, chunga mdomo wako, usiwe mwongeaji sana.

Upo usemi kwamba mpumbavu akikaa kimya anaweza kudhaniwa ni mwenye hekima, ila anapofungua mdomo wake ndiyo anadhihirisha kila kitu. Usiwe mwongeaji sana kama hutaki watu wayajue madhaifu yako na kuyatumia kujinufaisha wenyewe.

Rafiki, karibu usome kwa kina uchambuzi wa kitabu hicho cha THINGS FALL APART kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua; www.t.me/somavitabutanzania

Karibu pia upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.