Kama kuna kitu unajiambia unataka kuanza kukifanya mapema iwezekanavyo, basi jua mapema hiyo ni sasa.

Kama utajiambia kuna mapema nyingine zaidi ya sasa, jua hutafanya hicho ulichopanga kufanya au utachelewa sana kuanza kiasi kwamba unapokuja kukifanya, fursa inakuwa imekuacha.

Hivyo unapaswa kubadili kauli zako, kwa yale muhimu, badala ya kujiambia utaanza mapema iwezekanavyo, jiambie utaanza sasa na angalia popote unapoanza kufanya.

Kanuni ya fizikia ya mwendo inasema kitu kitabaki kwenye hali ambayo kipo mpaka pale nguvu ya nje itakapobadili hali hiyo. Ina maana kitu kilichosimama kitaendelea kusimama na kilicho kwenye mwendo kitaendelea na mwendo.

Unapokuwa mtu wa kuanza sasa, hata kama unaanza kwa kidogo, unajiweka kwenye mwendo wa kufanya na hilo litakuwezesha kubadili sana matokeo unayoyapata.

Mara ngapi umepata wazo zuri la kufanya kitu, ukajiambia utafanya baadaye halafu baadaye hiyo usikumbuke tena? Badilika kwenye yale muhimu. Kwa kuwa huwezi kuwa unafanya kila unachowaza, ila kwenye yale muhimu kabisa, yale yanayobeba mafanikio yako, unapopata wazo zuri la kufanya kitu, acha mengine yote yasiyo muhimu na anza kutekeleza wazo hilo.

Nitaanza sasa ni kauli yenye nguvu mno, inayokuwezesha kupiga hatua kubwa kwenye maisha, hata kama unaanza kwa hatua ndogo ndogo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha