2271; Kazi zako ni mbili, pesa na madili…
Kinachofanya biashara nyingi ndogo kutokukua ni wamiliki wa biashara hizo kufanya kazi ndani ya biashara badala ya nje ya biashara.
Kufanya kazi ndani ya biashara ni kufanya kile ambacho hata ukimwajiri mtu anafanya. Yake majukumu ya kila siku ya biashara husika.
Tatizo la kufanya kazi ndani ya biashara ni inamchosha mtu, hivyo anakuwa hana muda wa kuweza kuikuza zaidi biashara hiyo.
Kufanya kazi nje ya biashara ni kuwakabidhi wengine majukumu ya kila siku kwenye biashara, kisha mmiliki anafanya majukumu makubwa yanayopelekea kuikuza biashara hiyo.
Kwa kuwa majukumu ya kila siku hayamchoshi mmiliki na kuchukua muda wake, anaweza kupambana na yale makubwa zaidi.
Swali unaloweza kuwa unajiuliza ni majukumu gani ya nje ya biashara ambayo mmiliki anapaswa kuyatekeleza.
Jibu ni yapo mengi kulingana na aina ya biashara, ila makubwa mawili kwa kila biashara ni pesa na ‘dili’.
Unapaswa kutafuta pesa zaidi kwa ajili ya biashara yako ili kuongeza mtaji na kukuza biashara. Unapaswa kuweka muda kwenye kutafuta kila fursa za kupata fedha zaidi.
Upande wa ‘dili’ni kuhakikisha unapata mipango na makubaliano mazuri kwenye manunuzi au malipo makubwa ambayo biashara yako inaingia.
Kwa kila unachonunua au kulipia, hakikisha unapata dili nzuri zaidi, maana kwenye biashara, faida nzuri unaipata wakati wa kununua na siyo kuuza. Ukinunua au kuzalisha kwa gharama ndogo, kwa kuuza kwa bei ile ile unapata faida zaidi.
Hivyo wewe kama mmiliki wa biashara, kazi za mauzo, masoko, uendeshaji na nyinginezo, ajiri watu bora wazifanye, wewe pambana na kupata pesa zaidi na kupata madili mazuri.
Kocha.