2275; Mambo sita muhimu kwenye ushawishi…
Mafanikio yako yanategemea sana ushawishi wako, hivyo ni muhimu uwe na ushawishi mzuri.
Katika kuboresha ushawishi wako, zingatia haya sita.
1. Uharaka, watu huwa hawasukumwi kuchukua hatua kama kitu hakina uharaka. Ndiyo maana siku ya mwisho ya kufanya kitu ndiyo wengi hufanya. Hivyo weka hali ya uharaka kwenye kile unachotaka mtu afanye.
2. Upekee, watu huwa wanapenda vitu vya kipekee na wamechoshwa na mazoea, wape kilicho cha kipekee na watashawishika kuchukua hatua.
3. Uhitaji, lazima umuoneshe mtu kwa nini anahitaji sana kuchukua hatua unayomshawishi, ni kwa namna gani anakwenda kunufaika. Kumbuka kila mtu ni mbinafsi na anajali maslahi yake zaidi.
4. Uhusika, hakikisha kitu kinamhusu mtu moja kwa moja, kinamgusa yeye kweli kweli. Bila ya kuona uhusika wake, mtu hashawishiki.
5. Urahisi, watu huwa hawapendi vitu vigumu, hivyo waoneshe jinsi ilivyo rahisi kutumia au kuchukua hatua na watashawishika zaidi.
6. Uhakika, watu wameshadanganywa sana, hivyo wanakuwa waangalifu kabla ya kukubali kitu. Unapaswa kuwapa uhakika kwamba hawatapoteza chochote kwa kukubaliana na wewe. Wape watu uhakika na watasukumwa kuchukua hatua.
Kwa wale watakaokataa.
Kuna ambao utatumia mbinu hizo sita na bado watakataa, watakupa sababu mbalimbali kwa nini hawakubali.
Tumia njia hizo hizo sita kujibu mapingamizi yao.
1. Mtu akisema anahitaji muda zaidi, muoneshe uharaka uliopo ambapo akisubiri atapoteza.
2. Akisema ana kitu husika muoneshe upekee ambao upo kwenye unachomshawishi na hawezi kupata pengine.
3. Akisema hana uhitaji muoneshe changamoto aliyonayo sasa na jinsi unachomshawishi kitaitatua.
4. Akisema haimhusu au kumfaa, muoneshe jinsi inaendana naye.
5. Akisema ni ngumu kwake kuelewa au kutumia, muoneshe ilivyo rahisi.
6. Akisema anahofia kupoteza rasilimali zake, mpe uhakika kwamba hakuna atakachopoteza.
Kwa kufuata mbinu hizi sita, kutakuimarisha kwenye ushawishi na watu kukubaliana na wewe zaidi.
Kocha.