2279; Maswali matano muhimu ya kukupa mwanga…

Kuna wakati unaweza kujiona kama umepoteza uelekeo katika kufanyia kazi ndoto zako.
Ni katika wakati huo unahitaji kuwa na kitu kinachokupa mwanga ili ujue vipi vipaumbele sahihi kwako.
Hapa kuna maswali matano muhimu ambayo ukijiuliza na kujipa majibu, utapata mwanga mkubwa.
1. Nini hasa ninachotaka.
Kama hujui unachotaka, ni hakika kwamba huwezi kukipata, kama ilivyo huwezi kufika kule ambako hujui unaenda. Hivyo ni muhimu kujiuliza swali hili ili kuhakikisha hujatoka njia kuu.
2. Kipi ni muhimu kwangu sasa.
Pamoja na kujua unachotaka, kuna mambo ambayo ni muhimu kwako kufanya kwa wakati ulionao na yapo mambo yanayoweza kusubiri. Lazima uwe na njia sahihi ya kujiwekea vipaumbele kwa kufanya yaliyo muhimu kwanza kabla ya kuhangaika na mengine.
3. Napataje kile muhimu kwa sasa?
Ukishajua kilicho muhimu, mengine yote yanakaa pembeni na umakini wako wote unakwenda kwenye kile muhimu kwa sasa.
4. Nini kinanizuia kupata ninachotaka sasa?
Kama hujapata unachotaka, kuna kitu kinakuzuia kukipata. Hivyo unapaswa kujua kinachokukwamisha na jinsi ya kukivuka ili upate unachotaka. Inaweza kuwa muda, uzoefu, fedha, ujuzi, watu na kadhalika.
5. Nitajuaje pale nitakapopata ninachotaka?
Unaweza kujua unachotaka, lakini usijue pale unapokipata. Hii imepelekea wengi kukimbizana na yasiyo sahihi kwa kuwa hawajui kama wameshapata wanachotaka. Lazima uwe na njia ya kujua kama umeshapata unachotaka ili usifanye mambo yasiyo sahihi na ukakipoteza.
Mfano mzuri hapa ni mtu anajiambia anataka utajiri au uhuru wa kifedha, anapambana kwa kila njia kuupata, lakini ile tamaa haikauki, anajikuta anashawishika kufanya uwekezaji usio sahihi kwa kuwa anaona atanufaika zaidi kitu kinachopelekea apoteze kila alichopata.
Ukijua wakati umepata unachotaka, utaondoa hatari ya kukipoteza.
Mambo ni mengi, usumbufu ni mkubwa na wanaotaka kututoa kwenye njia zetu ni wengi.
Mara kwa mara ni muhimu ujiulize maswali haya matano ili upate mwanga na kama kuna ulipotetereka basi ujirekebishe.
Kocha.