2281; Manne ya kuzingatia kwenye mauzo…

Kila mmoja wetu ni muuzaji.
Kuna kitu unauza kwenye maisha yako, kile unachowashawishi watu wakubaliane na wewe.
Ili ufanikiwe, lazima uwe muuzaji mzuri, kwa sababu kila unachotaka kwenye maisha yako, kinatoka kwa wengine.
Kuna mengi ya kufanya ili kuwa muuzaji mzuri, lakini haya manne tunayokwenda kujifunza hapa, ni ya msingi kabisa.
1. Hamasa.
Unahitaji kuwa na hamasa ya juu sana kwenye kile unachouza. Uwe unakiamini na kukikubali mno wewe mwenyewe.
Wateja wako ni rahisi kujua kama kitu hukiamini na kukikubali. Na hamasa huwa inaambukizwa, kadiri unavyohamasika kuhusu kitu, ndivyo unavyoweza kuwahamasisha wengine.
Hivyo jijengee hamasa kubwa kwenge kile unachouza, na hii iwe halisi kabisa kutoka ndani yako, siyo maigizo.
2. Kuwaelewa unaowauzia.
Kama huwaelewi vizuri wale unaowauzia, itakuwa vigumu kwako kuwashawishi.
Unapaswa kuwaelewa, hasa kwenye changamoto na mahitaji waliyonayo. Lazima uyajue maumivu waliyonayo ambayo kile unachowauzia kinayatatua.
Kila mtu huwa anaweka maslahi yake mbele, unapokuwa unamuelewa mtu na kuweka maslahi yake mbele, atakubaliana zaidi na wewe.
3. Kuelewa unachouza.
Unapaswa pia kuwa na uelewa mkubwa wa kile unachouza, kwa kujua manufaa ambayo mteja atayapata kwa kukitumia na jinsi ya kutatua changamoto mbalimbali zinazotokana na kitu hicho.
Maana wateja watakuuliza maswali mbalimbali na jinsi unavyoyajibu watajua kama unakielewa unachouza au la.
4. Kukabili mapingamizi.
Pamoja na kufanya vizuri kwenye hayo matatu hapo juu, kuna watu hawatakubaliana na wewe, watakuwa na mapingamizi mbalimbali na hata kukataa kabisa.
Kwa mapingamizi unapaswa kuyajibu kwa uelewa ulionao kwa mteja na kile unachotaka kumuuzia.
Kwa wale wanaoelewa na kukataa, jua kwamba hawajakukataa wewe, bali wamekataa kile ulichokuwa unawauzia. Hivyo usiruhusu kukataa kwao kukuumize au kukukatisha tamaa.
Kukataa kwa mmoja kusikufanye uone na wengine watakataa, badala yake jua huyo haijamfaa na nenda kwa mwingine. Pia angalia kama uelewa ulionao kuhusu wateja unaowalenga na uelewa wa unachowauzia ni sawa. Watu wanaweza kukataa kwa sababu hawakuelewi au wanakuelewa vibaya.
Tambua siyo kila mtu atakubaliana na wewe, hivyo unapokataliwa, endelea mbele na siyo kukata tamaa.
Kwa kuzingatia haya manne, utaweza kufanya vizuri kwenye mauzo na kufanikiwa pia.
Kocha.