2282; Kuwa sahihi ni kukosea…

Kabla ya karne ya 21, waliofanikiwa sana ni wale waliogundua mfumo unaofanya kazi, kisha kurudia mfumo huo bila kubadili chochote.
Hivyo ndivyo mapinduzi ya kilimo na viwanda yalivyoendeshwa.
Na hata mfumo wa elimu ulijengwa kwenye msingi huo, ndiyo maana mtu alipohitimu masomo alitegemewa kuwa ameshajua yale yaliyo muhimu ambayo atayafanyia kazi maisha yake yote.
Karne ya 21 imekuja na mapinduzi mapya kabisa, mapinduzi haya ni tofauti na ya nyuma kwa sababu yanaharibu ule mfumo wa mazoea.
Katika mapinduzi haya ya teknolojia, chochote kinachofanyika kwa mazoea, kinatengenezewa programu ya kompyuta na hivyo kompyuta kuweza kukifanya vizuri kuliko hata mtu anavyoweza kufanya.
Hivyo kutumia kanuni ya zamani kwenye karne hii, ni kujipoteza.
Kufanya chochote kwa mazoea ni kujiweka kwenye hatari ya nafasi yako kuchukuliwa na kompyuta.
Ili kufanikiwa katika zama hizi, lazima uwe tofauti na mazoea, lazima kila wakati ufikirie namna mpya na ya kibunifu ya kile unachofanya.
Kompyuta inaweza kuiga, lakini haiwezi kubuni. Hivyo nguvu ya kuishinda kompyuta iko kwenye ubunifu.
Usikubali udadisi wako uzime kwa namna yoyote ile. Hata kama umepata kilicho cha uhakika, usilete mazoea, endelea kuja na ubunifu mpya kila wakati. Hiyo ndiyo namna pekee ya kushinda kwenye zama hizi.
Zamani ilikuwa ni dhambi kuhoji mifumo mbalimbali, ila zama hizi kuhoji ndiyo mpango mzima.
Zamani utii wa kila unachoambiwa ndiyo ilikuwa njia ya kufanikiwa.
Zama hizi uasi wa kutafuta ukweli wewe mwenyewe ndiyo unaokuwezesha kufanikiwa.
Kufanikiwa kwenye zama hizi kunataka sana uwe wewe, ufanye vitu ambavyo hakuna mwingine anafanya. Hilo litafanya uonekane kama unakosea, lakini hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kusimama na kufanikiwa.
Ndiyo maana katika zama hizi, kuwa sahihi, kwa kufanya kilichozoeleka ni kukosea. Na kukosea kwa kufanya ambacho hakijazoeleka ndiyo kuwa sahihi.
Katika kila unachofanya, kuwa na udadisi, hoji, jifunze na jaribu njia mpya za kukifanya ili kompyuta na programu zake zisikuondoe kwenye soko.
Tangu kuanza kwa mapinduzi haya, wataalamu wa kompyuta wamekuwa wakitabiri kwamba programu za kompyuta zitaimeza dunia, na hilo linaenda kasi.
Maroboti (Artificial Ontelligence) yanafanya kila ambacho kinafanyika kwa mazoea na kazi nyingi yanapewa hayo.
Kama hutavunja mazoea na kusimama kwa utofauti, maroboti hayatakuacha salama.
Hebu angalia vitu hivi vinavyofanywa na maroboti ambavyo zamani vilikuwa kazi za binadamu;
1. Kuendesha magari.
2. Kuandika makala na vitabu.
3. Kuandaa, kuimba na kucheza muziki.
4. Kitafsiri lugha mbalimbali.
5. Kupima watu, kutibu na kutibu watu.
6. Kufanya upasuaji.
7. Kufanya mapenzi.
Hapo acha zile kazi zilizozoeleka kama za viwandani.
Unaweza kujionea wazi kwamba kazi zilizoonekana ngumu kwa sasa karibu zote zinafanywa na maroboti, hivyo kama mtu hutasimama tofauti, utakuwa umechagua kuangushwa.
Kocha.