Dunia inabadilishwa na watu walio tayari kubadili mawazo yao kuwa halisia. Hili limejitokeza kwa mtoto Russel Ruge Mutahaba katika miaka yake nane kuweza kuandika kitabu chake cha “Change Your World”. Kitabu kikiwa na tafsiri ya “BADILI DUNIA YAKO”. Ndoto ya kuandika kitabu hutamaniwa na wengi na wachache huifanya kweli kama alivyofanya mtoto Russel Ruge. Ni hatua kubwa ya kupongezwa kwa mtoto kufanikiwa kuandika kitabu.

Kitabu kimeandikwa kwa lugha mbili, kiswahili na kingereza. Kitabu kina kurasa zipatazo 60 ambapo kwa kurasa mbili za mwisho kuna maswali matano ya mjadala ambayo yanafaa kwa wasomaji wote watu wazima na watoto. Mfano swali kwanini kufanya kazi kwa juhudi ni muhimu ? na je, una kipaji gani, na kwa namna gani unakiendeleza kipaji chako?. Maswali haya yanafikirisha kwa kila asomaye. 

Russel Ruge Mutahaba ni mtoto wa Zamaradi Mketema na marehemu Ruge Mutahaba ambaye moja ya watu ambao wanakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika tasnia ya muziki na ubunifu wa kimaudhui kupitia Clouds Media Group. Russel Ruge Mutahaba yupo darasa la nne shule ya Kimataifa ya Feza. Pia ni mwongozaji wa kipindi cha watoto runingani kiitwacho Smart Bees kinachorushwa na Clouds TV.  

Uzinduzi wa kitabu chake ulofanyika Hyatt Hotel tarehe 15 mwezi Machi 2021 uliibua hamasa kwa wazazi wengi kuwahamasisha watoto wao kutimiza ndoto zao wangali ni watoto kwa kupewa tu nafasi ya kufanya. 

Kitabu kinazo sura 14 ambapo kila sura imeambatana na maelezo mafupi, yanayoeleweka na na michoro ambapo kwa usomaji wa watoto huwasaidia kukumbuka walichosoma kirahisi.

Sura ya kwanza anazungumzia; Kipaji chako ni Kazi Yako.

Sura hii nimejifunza namna kipaji ukikiweka nguvu kinavyoweza kumpa mtu kazi. Katolea mfano wa mfanyakazi wa nyumbani ambaye ana nafasi ya kulea watoto, kufua nguo na kazi za jikoni kunakomsaidia kujipatia kipato.

Sura ya pili anazungumzia; Namna ya Kupata Pesa.

Mwandishi anagusia namna matendo mema ni chanzo cha kupata fedha. Mfano dada wa nyumbani anayeangalia nyumba wakati ambao mwenye nyumba hayupo analipwa pesa kwa matendo yake mazuri ya maangalizi. Hivyo ili tujipatie kipato lazima tuambatane na matendo yaliyo mazuri kwa jamii yanayovutia tupate matokeo ya kulipwa pesa. Pesa ni matokeo ya kutenda kitu kinacholeta thamani kwa mtu mwingine

Sura ya tatu anazungumzia; Namna ya kupata Rafiki.

Rafiki wa faida anaweza asifanane na wewe kila kitu ila rafiki ambaye anakupenda na kuwa tayari kuwa msaada kwako. Ili upate marafiki wazuri basi kuwa jasiri, imara na mwenye kujidhibiti.

Sura ya nne anazungumzia; Namna ya Kupata Unachokitaka Maishani.

Hakuna mbadala wa juhudi au kazi ili upate chochote kile utakacho katika maisha. Unaweza kupata chochote ukitacho endapo utaweka juhudi kubwa kukipata. Ikitokea hujakipata Russel anasema huenda dunia inakwambia usiendelee au jaribu tena kwa kuongeza juhudi zaidi.

Sura ya tano anazungumzia; Namna ya Kuwa Mfano wa Kuigwa.

Watu wakuigwa hupendwa na watu sababu ya yale wanayoyafanya yanayoibua hamasa kwa wengine kuchukua hatua. kila mmoja anaweza kuwa kioo au mtu wa kuigwa kwa mazuri au mabaya. Kuigwa kwa mazuri ni alama njema inayopendwa na watu wengi.

Sura ya sita anazungumzia; Namna ya Kufanya Ulichotaka Kufanya.

Wakati mwingine unahitaji kwenda zaidi ya hatua unazofanya ili kupata ulichotakiwa kufanya. Maisha yanahitaji ujasiri wa kujituma ili ufanikiwe kwa mambo utakayo. Unaweza kupata maumivu au magumu kipindi unapojitahidi kufanya ulichotaka kufanya ila mwandishi anasema hupaswi kukata tamaa bali kuendelea kujaribu tena na tena mpaka unapata ulichokuwa unataka ukipate.

Sura ya saba anazungumzia; Nini cha Kufanya inapokukuta hali yeyote.

Utulivu ni kitu cha kwanza unachopaswa kuwa nacho kwa hali zozote utakazokutana nazo. Pili ni usikivu au kusikiliza. Kupitia kufanya haya mawili unaweza kuvuka hali nyingi katika maisha.

Sura ya nane anazungumzia; Namna ya Kuongoza.

Anagusia namna uongozi kunasimama katika misingi mikubwa minne. Moja ni kusikiliza, kusisitiza, kukubali na kujadiliana. Kiongozi mzuri husikiliza, husisitiza, hujadili na hukubaliana na mawazo mazuri kutoka kwa watu wengine.

Sura ya tisa anazungumzia; Unawezaje kuwa Bingwa.

Ubingwa ni matokeo ya kushinda vitu vingi kunakoambatana na kujituma kuliko kawaida. Mfano mashindano ya matamshi ya maneno lazima mtoto ajifunze kusoma sana, au mchezo wa mpira lazima kuwa na mazoezi ya kutosha kabla ya mechi ili kushinda. Mwandishi anasema maisha yana mashindano mengi ila kwa ujumla wake yana kitu kimoja kinacholingana cha ili uwe bingwa au mbobevu wa jambo lazima ujitume zaidi. Anasema watu wengi husema mambo ni rahisi ila wakijaribu unakuta wanafeli.

Sura ya kumi anazungumzia; Unawezaje kuwa mtu Mwema.

Mtu mwema ni rafiki wa watu wengi wanaomzunguka. Mtu mwema hulinganishwa na kusema mtu wa watu sababu ni mtu ambaye anazungumza na kila mtu na kuheshimu watu wote. Kujitoa na kujishusha kunazalisha watu wema katika jamii.

Sura ya kumi na moja anazungumzia; Unawezaje Kuwa Mkamilifu.

Ukweli ni kuwa huwezi kuwa mkamilifu. Watu wote wana upande wa maisha mzuri na mbaya. Ila unaweza kuwa mtu mzuri kwa mambo makubwa matatu. Moja ni matendo yako. Mtizamo na haiba njema. Ukiwa na haya mambo matatu hutaweza kuwa mkamilifu ila utakuwa mtu mzuri kwa wale wanaokuzunguka.

Sura ya kumi na mbili anazungumzia; Unawezaje Kupendwa.

Mwandishi anasema ili watu wakupende lazima kwanza uwe mtu mkarimu, mzuri na mpole. Wapende watu wote ingawa unaweza usipendwe na kila mtu. Unaweza kuwa mkarimu kwa kusaidia wengine, kuwapenda na kuwasemea vizuri.

Sura ya kumi na tatu anazungumzia; Unachohitaji Maishani.

 Unaweza kufikiria mengi unayoyahitaji maishani ila ukikosa vitu hivi vitano maisha hukosa maana. Vitu hivi vitano ni familia, chakula, malazi, marafiki na hisia. Vitu hivi vitano unahitaji kuvipa kipaumbele kabisa maishani maana vinaleta maana ya maisha. Familia ni kila kitu pengine hata kuzidi marafiki, unahitaji chakula ili uishi, malazi ili uwe salama, unahitaji hisia ili ujihisi kuwa na furaha katika maisha.

Sura ya kumi na nne anazungumzia; Nidhamu.

Mwandishi anasema yote aloandika yanaweza yasitokee endapo mtu atakosa nidhamu. Nidhamu ya muda, nidhamu ya kuishi na watu na nidhamu binafsi vinahitajika ili mtu aweza kufanikiwa. Kila kitu kinahitaji nidhamu ili kitokee. Iwe watu wenye vipaji au wasio na vipaji wote wanahitaji kuwa na nidhamu maana bila nidhamu hawawezi kufikia mafanikio makubwa.

Hiki ni kitabu cha kusomwa na rika zote maana mambo yaliyomo yaakisi maisha yetu ya kila siku. Ingawa mwandishi amewaandikia watoto ila watu wazima nao wanaweza kujifunza vitu vingi vya kuyaboresha maisha yao.

Mchambuzi wa Vitabu,

Dkt. Raymond N Mgeni 

+255 (0) 676 559 211 

raymondpoet@yahoo.com