2285; Watu watabaki kuwa watu…
Soma kauli hii; leo naenda kukutana na watu wasio waaminifu, wenye tamaa, wasiojali na watakaonikwaza na kuniumiza. Lakini hilo halitanisumbua kwa namna yoyote, kwa sababu najua ndivyo watu walivyo.
Unadhani hiyo kauli ilitolewa mwaka gani? Ni miaka zaidi ya elfu 2 iliyopita na aliyekuwa mtawala wa Roma na mwanafalsafa wa Ustoa Marcus Aurelius.
Sasa hebu niambie, nini kimebadilika kwenye kauli hiyo kwa miaka hiyo elfu 2.
Kila siku unakutana na watu wanaokukwaza kwa namna moja au nyingine.
Labda unaendesha gari halafu dereva mwingine anakatisha mbele yako na kutaka kusababisha ajali.
Labda umepanda daladala na abiria mwenzako akakujibu vibaya au kukukanyaga.
Labda ni mtu mlikubaliana kitu lakini hajafanya kama mlivyokubaliana.
Ni vigumu mno kuianza na kuimaliza siku yako hujakwazwa na yeyote.
Lakini je tumekuwa tunachukua hatua gani?
Umekuwa unakasirika, unakata tamaa na hata kupoteza imani juu ya wengine. Fundi mmoja amekusumbua na unasema mafundi wote hawafai.
Lakini majibu ya hilo yapo, yameandikwa mahali, kwa zaidi ya miaka elfu mbili, kwamba wanaotukwaza tutakutana nao kila siku, ila hatupaswi kuruhusu makwazo yao yatusumbue.
Kwa sababu watu wataendelea kuwa watu, hata tufanyeje.
Nakumbuka wakati niko chuo cha udaktari, mwalimu aliyekuwa anafundisha somo la UKIMWI alikuwa anauliza maswali njia zipi za kusaidia kudhibiti kabisa maambukizi ya vizuri vya ugonjwa huo.
Mtu mmoja akajibu kudhibiti biashara ya ukahaba. Mwalimu akamjibu hicho ni kitu kisichowezekana, ukahaba ni tasnia yenye miaka mingi na itaendelea hivyo.
Sikumuelewa vizuri pale, lakini kadiri nilivyokuwa natafakari alichosema, niliona maana yake iko wapi.
Ukweli ni kwamba, binadamu wataendelea kuwa binadamu na kufanya yale ambayo binadamu huwa wanafanya, haijalishi kuna mabadiliko kiasi gani kwenye dunia.
Kwa kujua hili, unapaswa kuwa tayari kukabiliana na ubinadamu na kutokukwazika au kukata tamaa.
Lakini pia ubinadamu na mashaifu yake, ndiyo unafanya maisha yaende na watu wawe na kazi.
Fikiria kama kungekuwa hakuna maovu kabisa, watu wote ni watakatifu, dini zingekuwa za kazi gani?
Fikiria kama afya za watu zingekuwa bora kabisa, hakuna maradhi yoyote, tasnia ya afya ingekuwa ya kazi gani?
Jamii nzima inaendeshwa na maovu na madhaifu yetu wanadamu.
Hilo halikupi wewe uhalali wa kufanya maovu au kuruhusu madhaifu yako yakuangushe, bali linakufanya ujue watu wataendelea kuwa watu na maovu na madhaifu yao hivyo jipange namna utakavyoendana nao ili usikwazike kila wakati.
Kocha.