2290; Endelea kukaa kimya…

Kama mtu alitumia mamlaka yake kukukandamiza au kukuumiza na wewe ukachagua kukaa kimya kwa kuyaogopa mamlaka yake, hupaswi kuanza kulalamika pale mtu huyo anapokuwa hayupo au hana tena mamlaka yale aliyotumia kukuumiza nayo.
Kuja kusema baadaye kwamba mtu alikuumiza, alikosea au hakuwa anafaa baada ya mtu huyo kuondoka kwenye nafasi hiyo, ni kuweka wazi udhaifu na unafiki wako.
Kulinda heshima yako ndogo iliyobaki, kama ulichagua kunyamaza basi endelea kunyamaza. Wasiojua watadhani uliamua kupuuza. Ila unapobadilika na kuanza kusema, unaweka wazi kwamba ni muoga, hujiamini, hujithamini, unategemea upendeleo na huwezi kujisimamia mwenyewe.
Nakubaliana na wewe kwamba kuna wenye mamlaka ambao ukipingana nao wanaweza kukatisha uhai wako na hivyo jambo bora kufanya ni kunyamaza.
Nisichokubaliana nacho ni pale unapokuja kufungua mdomo wako baadaye na kuanza kusema, hapo ndiyo unaharibu zaidi.
Falsafa ya ustoa inatufunza vyema, kila jambo linaweza kuangukia kwenye upande mmoja kati ya hizi mbili;
Moja kuwa ndani ya uwezo wako kuliathiri na hapo unapaswa kuchukua hatua.
Mbili kuwa nje ya uwezo wako na hapo unapaswa kulikubali au kulipuuza.
Kuwa kigeugeu, kwa sasa kuchagua kukaa kimya na kisha baadaye kuja kuongea siyo tu ni unafiki, bali pia inakufanya ujidharau na wengine nao wakudharau.
Kama ulichagua kukaa kimya, endelea kukaa kimya, usianze kusema baada ya hatari kuondoka.
Na kama kweli hukubaliani na kitu, simamia hilo kwa gharama zozote zile.
Hivyo ndivyo unavyoweza kujenga maisha ya heshima kwako.
Kocha.