2294; Tatizo la wataalamu…

Tafiti nyingi ambazo zimefanywa kwenye ubashiri, kwa kulinganisha wataalamu wa eneo husika na watu wa kawaida, watu wa kawaida wamekuwa wanafanya vizuri kuliko wataalamu.

Pia mambo mengi ambayo wataalamu hukadiria au kushauri huwa hayaendi kwa namna walivyoeleza kwa utaalamu wao.

Tatizo la wataalamu ni kuwa na ujuzi mkubwa kwenye eneo dogo na kushindwa kuhusisha ujuzi mwingine matika ushauri na maamuzi yao.

Pia wataalamu wamekuwa wanatumia uzoefu wa yaliyotokea nyuma kutabiri au kupangilia yajayo.
Hilo linawafanya wasione uwezekano wa mambo mapya mengi yanayoweza kutokea.

Nasim Taleb kwenye kitabu chake kinachoitwa Black Swan, anaeleza dhana hii kwa kina kwa kutumia mfano wa bata maji. Anasema kwenye jamii ambayo imezoea kuona bata maji weupe tu, watu wanaamini bata maji wote ni weupe. Ni mpaka siku moja wamuone bata maji mweusi ndiyo wanagundua hawako sahihi.

Taleb anatumia mfano mwingine wa bata mzinga anayelishwa kila siku ili achinjwe siku ya krismasi. Bata mzinga huyo ataendesha maisha yake kwa mazoea, akijua kila siku chakula kinakuja kama siku za nyuma.
Ni mpaka siku anakutana na kisu ndiyo anajua kumbe yasiyotegemewa yanaweza kutokea.

Kikubwa sana cha kujifunza hapa ni kutokukubali kukatishwa tamaa na wale wanaojiita wataalamu au wazoefu. Uzoefu walionao ni wa nyuma, wa mambo ambayo yalishatokea. Lakini hawana uzoefu wa mambo ambayo hayajawahi kutokea na hayo yana nafasi ya kutokea.

Tumia hili kuamini kwenye ndoto zako kubwa, kwa kuwa wengi watakukatisha tamaa, wakikuambia hakuna aliyewahi kupata unachotaka. Waambie wanatumia uzoefu wa nyuma, hawajui yajayo ambayo bado hayajatokea.

Utaalamu na uzoefu wa wengine usiwe kikwazo kwako, jua chochote kinaweza kutokea hivyo endelea na mapambano bila ya kukata tamaa.

Kocha.