2299; Kupewa, kupata na kutengeneza…

Inapokuja kwenye fedha, maneno hayo matatu yana maana na tofauti kubwa.

Kuna ambao wanaingiza fedha kupitia kupewa na wengine, mfano walioajiriwa.
Watu hawa hawana nguvu kubwa ya kuamua wapewe kiasi gani, kwa kuwa wanategemea kupewa, yule anayetoa ndiye anayeamua kiasi gani awape.
Hii siyo njia nzuri na unayoweza kuitegemea, kwa sababu haikuweki huru.

Kuna ambao wanaingiza fedha kupitia kupata kutoka kwa wengine, mfano ni wafanyabiashara. Wanatoa kitu cha thamani na wengine wanawapatia fedha. Hawa wana uhuru kiasi kwenye kiwango gani wapate, ila wana ukomo unaotokana na ushindani unaokuwa kwenye biashara.

Na kuna ambao wanaingiza fedha kupitia kutengeneza, hawa wanakuja na wazo jipya kabisa ambalo linawapa uhuru wa kuingiza kipato kisicho na ukomo. Mfano hapa ni wajasiriamali, wale wajasiriamali hasa, wanaofanya kile ujasiriamali unamaanisha, ambacho ni kuona fursa ambayo inaweza kuwa na hatari, ambayo hakuna mwingine anaona au anaifanyia kazi na kisha kuwa na ujasiri wa kuifanyia kazi fursa hiyo.
Wajasiriamali huwa wanakuwa mbele zaidi kuliko wengine, wakiona yale ambayo wengi hawaoni sasa. Lakini pia hawabaki kwenye kitu kimoja tu, kila wakati wanaangalia fursa mpya na kubwa zaidi na ndiyo maana huwa hawaathiriwi na ushindani.

Je wewe unaingiza fedha kupitia njia zipi, je ni kupewa kama mwajiriwa, kupata kama mfanyabiashara au kutengeneza kama mjasiriamali?

Kocha.